Hesperian Health Guides
Kuandaa na kuhifadhi chakula
HealthWiki > Toleo Jipya: Mahali Pasipo na Daktari > Maji na usafi wa mazingira > Kuandaa na kuhifadhi chakula
Maradhi yanaweza kuenezwa kupitia vijidudu na minyoo ambayo huingia miili yetu kupitia vyakula tunavyokula. Ili kuepuka kuugua kupitia chakula:
- Nawa mikono yako kabla ya kukamata chakula au kuandaa chakula.
- Pika vizuri bidhaa za nyama kabla ya kula. Osha vizuri vyombo na vifaa vyote vinavyotumika kutayarisha nyama, vyakula vya baharini, mayai ili vijidudu kutoka kwenye vyakula hivyo ambavyo havijapikwa visienee kwenye chakula ambacho tayari kimepikwa au vyakula vingine ambavyo huliwa bila kupikwa.
- Osha au menya matunda na mbogamboga, au pika kabla ya kutumia. Hii huua vijidudu vya magonjwa kutoka udongoni mahali vinapolimwa, na vijidudu vingine ambao huingia wakati wa usafirishaji au hifadhi.
- Kula chakula moja kwa moja baada ya kupikwa, au hifadhi chakula kilichokwisha kupikwa kikiwa kimefunikwa vizuri na salama dhidi ya nzi na uchafu hadi kitakapoliwa.
- Pasha au kuchemsha tena chakula kinachouzwa mitaani, au chakula chochote ambacho kimeachwa nje, hadi kitakachokua cha moto. Hii inaweza kusaidia kuua vijidudu ndani ya chakula hicho kabla ya kuliwa.
- Hifadhi chakula kwa njia ambayo huhakikisha usalama wake dhidi ya wadudu na wanyama wadogo ambao wanaweza kueneza vijidudu vya magonjwa.
- Tunza eneo la kupikia katika hali ya usafi. Osha vyombo vya kupikia na kulia, sehemu za kukatia, na vifaa kila mara baada ya kutumia na uruhusu kukauka vizuri.
- Mabaki ya chakula wapewe wanyama, au yakusanywe sehemu maalum kwa ajili ya kutengeneza mboji.
- Chakula kihifadhiwe kwenye hali ya ubaridi, ili kusaidia kisiharibike haraka.
Unaweza kutengeneza chombo cha kuhifadhi chakula kikiwa na ubaridi kwa kutumia vyungu 2 vya udongo vyenye ukubwa tofauti. Weka chungu kimoja kidogo ndani ya kingine na kujaza nafasi ya katikati na mchanga. Mchanga uloweshwe kwa kuongeza maji mara 2 kila siku. Weka chakula ambacho unataka huhifadhi katika ubaridi kwenye chungu kidogo, na kuhakikisha vyungu vyote 2 vimefunikwa wakati wote.
Zuia nzi wasitue kwenye chakula
Nzi hueneza vijidudu vya magonjwa kwa kutua kwenye kinyesi cha binadamu na wanyama, na baadae kwenye chakula. Funika chakula na kutengeneza mitego ya kuwanasa nzi ili kuzuia wasieneze magonjwa.
Jinsi ya kutengeneza mtego wa kunasa nzi
- Unganisha karatasi kwa gundi au tepu kutengeneza zana yenye muundo wa koni ikiwa na uwazi kwenye nchaa yake ya juu, halafu ingiza koni hiyo ndani ya jagi au chupa.
- Ziba mdomo wa chupa ili pasiwe na nafasi yeyote kati ya koni na chupa.
- Ning’iniza chupa kwenye kamba au funga kwenye kijiti kilichosimikwa kwenye ardhi.
- Weka tunda, samaki au chambo yeyote chini ya mtego. Nzi watatua kwenye chakula, halafu kuruka kwa kupitia koni hadi kwenye chupa.
- Kuondoa nzi kutoka kwenye chupa, geuze mdomo wa chupa juu, ondoa koni, jaza maji kuhakikisha kuwa nzi wote wanakufa halafu tupa mahali panapostahili.