Hesperian Health Guides
Kunawa mikono
1. Mimina maji juu ya mikono yako. | 2. Tumia sabuni na kusugua mikono pamoja. Msuguano huo ndiyo utaondoa vijidudu hivyo.Hakikisha unasugua katikati ya vidole na kuzunguka kucha za vidole pia. |
3. Mimina maji safi juu ya mikono yako na kusuuza vizuri. |
4. Kausha mikono yako kwa kitambaa kisafi. |
Ni bora zaidi kutumia sabuni kuondoa uchafu na vijidudu vya magonjwa. Kama sabuni haipo, unaweza kutumia mchanga au majivu.
Nawa mikono yako kila:
- Baada ya kujisaidia au kumtawaza mtoto.
- Kabla ya kuandaa chakula au kula.
- Baada ya kukamata wanyama.
- Baada ya kupiga chafya au kukohoa.
- Unapokuwa unaumwa.
Afya yako iko mikononi mwako. Nawa mikono kila baada ya muda mfupi.
Kibuyu chirizi (The tippy-tap)
Zana hii rahisi ya kunawa mikono hukuwezesha kunawa mikono kwa kutumia maji kidogo sana. Pia hukuwezesha kusugua mikono yako pamoja huku maji yakimiminika juu yake, hali ambayo huondoa vijidudu vya magonjwa. Weka zana hii kila mahali ambapo watu huhitaji kunawa mikono yao, kama vile sehemu chakula huandaliwa, karibu na choo, au sokoni.
Kutengeneza kibuyu chirizi unahitaji 1) chupa ya plastiki yenye mfuniko unaofungwa na kukaza kwa kuzungushwa, kama vile chupa ya maji ya kunywa, na 2) mrija wa bomba la peni au mrija wowote mdogo na mgumu.
1. Safisha chupa. | |||
2. Kwa kutumia waya wenye moto, toboa shimo dogo sehemu ya chini ya chupa hiyo. | |||
3. Ondoa mrija wa bomba la peni na kuusafisha.Chonga ncha na kuuchomeka kwenye tundu ulilotoboa kwenye chupa. Mrija unapaswa kuingia na kukaza vizuri. | |||
4. Jaza chupa na maji na kufunga mfuniko. Mfuniko unapokaza, hakuna maji ambayo yanaweza kupita kwenye mrija. Mfuniko unapokuwa umelegezwa, maji yanapaswa kutiririka nje vizuri. Unapokuwa na uhakika kwamba zana inafanya kazi vizuri, iweke mahali ambapo watu wataitumia kunawa mikono.Weka sabuni karibu, funga kipande cha sabuni kwenye zana hiyo. | 5. Jinsi ya kutumia kibuyu chirizi: Legeza mfuniko kiasi cha kutosha kuruhusu maji kuchurizika nje. Lowesha mikono yako, ongeza sabuni na kusugua mikono yako pamoja ikimiminikiwa na maji hadi itakapotakata. Funga mfuniko baada ya kumaliza. |