Hesperian Health Guides

Wiki zinazofuata baada ya kujifungua

Katika sura hii:

Katika wiki zinazofuata baada ya kujifungua, hakikisha mama yu salama, amepumzika, anakula vizuri, na kuna mtu wa kumsaidia kila anapohitaji msaada. Pia angalia Watoto wachanga na unyonyeshaji.

Uvujaji damu

Uvujaji damu kawaida huendelea kwa wiki kadhaa. Mwanzoni kiasi cha damu ambacho hutoka ni sawa na hedhi nzito lakini baada ya hapo hupungua, huwa majimaji zaidi, na hatimaye husimama baada ya wiki 2 hadi 3. Kujaza kitambaa au padi nzito ya hedhi na damu katika saa 1 (au kabla ya hapo) ni uvujaji damu mkubwa sana kuliko inavyotarajiwa.

Kama uvujaji damu utaongezeka siku zinazofuata kujifungua, mama atahitaji kusaidiwa na shughuli zake za kawaida pamoja na kuwahudumia watoto wake wengine ili aweze kupumzika. Lakini wakati mwingine uvujaji damu kupita kiasi husababishwa na kitu kilichoachwa tumboni, na pia maambukizi.

Mwanamke amelala chini, anavuja sana damu na anasinga au kupapasa tumbo lake

Kusaidia kusimamisha uvujaji damu, kwanza msaidie mama kunyonyesha. Hii hulifanya tumbo lake kubana au kukaza. Pia mkumbushe kukojoa mara kwa mara. Muonyeshe mama jinsi ya kusinga tumbo lake ili liweze kuwa gumu. Kama hayo yote hayatasaidia, mpatie dawa ya oksitosini au misoprosto na kutafuta dalili yoyote ya maambukizi.

Maambukizi

Halijoto ya mwanamke mara nyingi hupanda siku 3 baada ya kujifungua maziwa yanapoaza kuzalishwa. Lakini homa inayoendelea kwa muda au homa ya kipimo cha 38 sentigredi ni dalili ya maambukizi.

Mfanyakazi wa afya akichunguza halijoto ya mama kwa kuweka mkono wake kwenye paji la uso

Ni jambo la kawaida kwa majimaji yanayotoka ukeni kuwa na harufu kali kwa siku kadhaa baada ya kujifungua. Lakini harufu mbaya au yenye shombo baada ya kujifungua ni dalili ya maambukizi ndani ya tumbo la uzazi. Dalili zingine ni pamoja na kuhisi baridi inayotetemesha, mpwito wa haraka kwenye mshipa unaotoa damu moyoni,au maumivu au tumbo laini.

Tibu dalili zote za maambukizi tumboni na ampisilini, jentamaisini na metronidazoli. Kama inawezekana tibu kwa sindano za antibiotiki angalau kwa siku 2 za mwanzo. Kama huna antibiotiki, au kama mama hajaanza kupata nafuu ndani ya saa 24, tafuta msaada zaidi.