Hesperian Health Guides

Kero wakati wa ujauzito

Ujauzito unaweza kusababisha matatizo mengi ambayo ni kero lakini siyo hatari. Epuka kutumia dawa kuondoa kero hizi. Unaweza kuondoa kero hizi nyingi kwa urahisi kwa kutumia ufumbuzi wa nyumbani.

Kichefuchefu

Tumbo tupu huchangia kichechefu cha mimba kuzidi. Kula vyakula vidogo vidogo, mara nyingi kwa siku. Jaribu kula vyakula vyenye protini kama vile njugu, karanga, jibini, au nyama kabla ya kwenda kulala ili kubaki na chakula tumboni usiku wote. Kula kitu kikavu, kwa mfano wali au mkate asubuhi hata kabla ya kutoka kitandani.

Vyakula vyenye mafuta, viungo (vikolezo kwenye chakula), na vyakula vyenye harufu kali huzidisha kichefuchefu. Chai yenye tangawizi, chai ya rangi na ndimo vinaweza kusaidia.

Tindikali ya tumboni ikiwa ikipanda kifuani ndani ya mwanamke mjamzito
Mabadiliko ya homoni na mtoto ambaye anazidi kukuwa husukuma tindikali ya tumboni kifuani, na kusababisha kiungulia na maumivu.

Kiungulia

Kiungulia ni jambo la kawaida katika ujauzito. Bonyeza hapa kwa mawazo zaidi kuhusu kuzuia na kutibu kiungulia.

Kupata choo kigumu na kwa shida, na bawasiri

Wanawake wajawazito mara nyingi hupata taabu katika kujisaidia haja kubwa. Kufunga choo huwasabishia kero kubwa.

Kusukuma sana ili kutoa kinyesi kigumu huweza kusababisha bawasiri. Bawasiri ni mishipa iliyovimba inayozunguka unyeo. Bawasiri husababisha muwasho, maumivu, au kuvuja damu yenye rangi nyekundu inayon’gaa. Jifunze kuzuia na kutibu tatizo la choo kufunga na bawasiri.

Uchovu

Wanawake husikia uchovu zaidi wanapokuwa na ujauzito kwa sababu miili yao inahitaji kupumzika zaidi. Hii ni hali ya kawaida. Pumzika na kusinzia kidogo kila unapoweza.

Hata hivyo, uchovu kupita kiasi unaweza kuwa dalili ya anemia, jambo ambalo hutokea sana ila ni hatari kwa afya katika ujauzito. Kula vyakula vyenye kiwango kikubwa cha madini chuma kama vile nyama, maharagwe, mbogamboga, nafaka za jamii ya choroko, dengu nk. Pia tumia dawa ya kuongeza madini chuma mwilini.

Mwanamke mjamzito akiwa amekaa kwenye kiti, miguu yake ikiwa imeinuliwa kwenye kimeza kidogo

Kuvimba miguu na mikono

Pumzika na kuinua miguu yako juu kila siku, hasa iwapo utakuwa unatumia muda mwingi ukiwa umesimama au ukitembea. Epuka vyakula vilivyofungashwa au kufungwa kwenye makopo viwandani — mara nyingi huwa na chumvi nyingi, ambayo huzidisha uvimbe.

Unapoamka asubuhi au ukijikuta umevimba kila mahali, pamoja na usoni, huenda hizi ni dalili za hali inayotangulia kifafa cha mimba. Pima shinikizo la damu mara moja, na hata kama ni salama, endelea na utaratibu wa kupima angalau mara moja kwa wiki kwa kipindi chote cha ujauzito.