Hesperian Health Guides

Chunguza dalili za kiafya

Katika sura hii:

Chunguza dalili za kiafya za mama kila anapohudhuria.

 • Chunguza uzito wake na shinikizo la damu.
 • Kama anajisikia kuumwa au hajisikii vizuri, pia chunguza hali joto yake, mpwito wa mshipa unaotoa damu moyoni, na upumuaji. Jifunze jinsi ya kuchunguza dalili hizi za afya kupitia Kumchunguza mgonjwa (kinaandaliwa).
 • Chunguza ukuaji wa mtoto na mkao wake tumboni na sikiliza mapigo yake ya moyo.

Uzito

Iwapo una mzani, chunguza uzito wa mama kila anapohudhuria. Anapaswa kuongezeka uzito, kidogo kidogo kwa wakati katika kipindi chote cha ujauzito. Kwa ujumla, mwanamke mjamzito mwenye afya nzuri huongezeka kilogramu kati ya 12 na 16 wakati wa ujauzito. Kuanzia miezi 4, ni jambo zuri kiafya kuongezeka chini kidogo ya nusu kilogramu kila wiki. Kiwango cha kuongezeka kinaweza kuzidi kama ameanza ujauzito akiwa na uzito chini ya kiwango, na kupungua kama ameanza ujauzito akiwa amenenepa.

Kama mama haongezeki uzito, msaidie kupata chakula zaidi na kula zaidi.

Ugonjwa wa kisukari unaweza kusababisha uzito kuongezeka ghafla. Ongezeko ghafla la uzito katika wiki za mwisho za ujauzito nao unaweza kusababishwa na mapacha au hali inayotangulia kifafa cha mimba.

Shinikizo la Damu

Shiniko la damu la kiwango cha 140/90 au zaidi siyo salama kiafya. Kama kiwango cha shinikizo la damu kinazidi kupanda kila mara unapopima, hiyo pia ni dalili ya hatari kiafya.

Shinikizo la juu la damu mwanzoni katika ujauzito huashiria tatizo la kiafya ambalo husababishwa na ongezeko la shinikizo la damu kwenye mishipa inayotoka kwenye moyo. Tatizo hili hujulikana kama haipatensheni (angalia Magonjwa yasiyopona - kinaandaliwa). Ujauzito na kujifungua huwa ni hatari kwa mama mwenye tatizo la haipatensheni. Anahitaji msaada wa daktari.

Mafanyakazi wa afya akimpima shinikizo la damu mama mjamzito, na chati ikionesha tarehe na kiwango cha shinikizo la damu kila mwezi
Andika kiwango cha shinikizo la damu kila mara mama mjamzito anapohudhuria. Je kiwango kinapanda?

Shinikizo la juu la damu baada ya wiki 28 au miezi 6½ ya ujauzito linaweza kuashiria hali inayotangulia kifafa cha mimba. Hili ni tatizo la hatari ambalo linaweza kusababisha shambulio la kifafa cha mimba na hata kupoteza maisha. Mama mjamzito atahitaji msaada wa daktari haraka.

Kifafa cha mimba

Kifafa cha mimba ni ugonjwa hatari ambao hujitokeza katika siku za mwisho wa ujauzito. Hakuna njia ya kuizuia. Dalili zake kubwa ni shinikizo la juu la damu ambalo huzidi kuongezeka kila wakati, na hatimaye mama kuanza kupata mashambulio-matikishiko ya maungo ya mwili. Unaweza kuponya maisha yake kwa kuwa mwangalifu kutambua dalili za hali hii katika kipindi kizima cha ujauzito na kumpatia matibabu haraka anapoonesha dalili hizo.

Iwapo shinikizo lake la damu litapanda sana,au kama ataanza kupatwa na mashambulio, dawa zinaweza kusaidia. Lakini tiba pekee ya kuondoa tatizo hilo ni kwa mtoto kuzaliwa.

Dalili za kifafa cha mimba
 • Kiwango cha shinikizo la damu cha 140/90 au zaidi baada ya mimba kufikisha wiki 28 (takriban miezi 3 ya mwisho ya ujauzito) na
 • Protini kwenye mkojo (angalia Kumchunguza mgonjwa - kinaandaliwa).


Kama utakuta shinikizo la juu la damu katika kipindi cha mwisho cha ujauzito, chunguza protini kwenye mkojo. Kama ana shinikizo la juu la damu, na protini kwenye mkojo, mama atakuwa katika hali inayotangulia kifafa cha mimba na anahitaji msaada au hali yake inaweza kubadilika haraka kuwa mbaya zaidi.

Kama hakuna protini kwenye mkojo, endelea kumwangalia kwa karibu na kupima shinikizo lake la damu angalau mara moja kwa wiki. Pata msaada wa daktari pale utakapoona dalili za hali inayotangulia kifafa cha mimba.

Dalili kali za hali inayotangulia kifafa cha mimba au kifafa cha mimba chenyewe
 • Maumivu makali ya kichwa.
 • Kiwango cha shinikizo la damu cha 160/110 au zaidi.
 • Kuona giza-giza-mauzauza.
Mwanamke ameanguka chini baada ya kupata shambulio
 • Maumivu katikati tumboni.
 • Kuvimba sana kukiwemo kuvimba usoni.
 • Kuchanganyikiwa akili.
 • Mitikishiko ya maungo.
Matibabu

Iwapo wakati wowote ule mama ataonesha dalili kali za hali inayotangulia kifafa cha mimba, tafuta msaada wa daktari haraka. Maisha ya mama yanakuwa katika hatari na anatakiwa kujifungua haraka iwezekanavyo.

Mishale ikionesha mahali pa kuchoma sindano kwenye sehemu ya juu ya kila kalio
Choma sindano ya magneziamu salfeti gramu 5 katika kila kalio kama inavyoonyeshwa na mishale:
 • Kuwa mtulivu.
 • Kama mama anapata shambulio, mgeuze alalie upande wake mmoja. Hii humlinda asikose pumzi kwa kuzibwa na matapishi au mate mdomoni.
 • Kama unayo, mpatie oksijeni.
 • Kusimamisha mashambulio, mchome sindano ya magneziamu salfeti gramu 5 katika kila kalio. Rudia hii baada ya saa 4. Usimpe magneziamu salfeti kama pumzi zake ni chini ya 12 kwa dakika. (Magneziamu salfeti huja katika vipimo mbalimbali, hivyo kuwa na uhakika una kiwango sahihi.) Soma zaidi hapa.

Ukuaji wa mtoto katika tumbo la uzazi

Mishale ikionesha kitovu cha tumbo la mama mjamzito na mfupa wa kinena
Ujauzito unapotimiza miezi 5, tumbo la uzazi linapaswa kukaribia kwenye kitovu.

Baada ya miezi 3 ya ujauzito unapaswa kukaribia sehemu ya tumbo la chini la mama, juu kidogo ya mfupa wa kinena. Katika hatua hii inawezekana kuhisi mtoto aliyepo ndani ya tumbo la uzazi. Mimba inapofikisha miezi 5 mtoto katika tumbo la uzazi atakuwa ameongezeka na kufikia kwenye kitovu, na kundelea kukua kwa kiwango cha wastani wa upana wa kidole kimoja kila wiki.

Kama tumbo la uzazi litakuwa kubwa zaidi au kuongezeka haraka, mwanamke anaweza kuwa na ujauzito wa muda mrefu kuliko na matarijio yako. Au anaweza kuwa na mapacha. Au anaweza kuwa na kisukari au tatizo lingine la kiafya.

Kama ukubwa wa tumbo la uzazi na mtoto ndani yake vitakuwa vikiongezeka polepole mno kuliko matarajio yako, inawezekana mama hana ujauzito mkubwa kama unavyofikiria. Baadhi ya sababu zingine za uongezekaji mdogo wa tumbo la uzazi na mtoto ndani yake ni kutokula chakula cha kutosha, au mama kupatwa na madhara ya moshi au kemikali zenye sumu.

Mkao wa mtoto tumboni

Mtoto mwanzoni wa ujauzito huhamahama ndani ya tumbo la uzazi. Mwishoni mwa ujauzito, mtoto huingia katika mkao wa kuzaliwa.

Ukipata uzoefu, unaweza kugusa na kuhisi iwapo kichwa cha mtoto kinaangalia chini (mkao salama) au makalio ndiyo yanaangalia chini (uzazi wa kutanguliza makalio, mkao ambao mara nyingi huwa wa matatizo).

Tumia mikono miwili na kukaza mikono kiasi. Mwambie mama apumue nje polepole na kumaliza pumzi yake yote, wakati ukiminya vidole vyako ndani kumhisi mtoto aliyeko ndani.

Gusa juu ya tumbo la mama na mikono yako miwili. Je unahisi kichwa kigumu cha mtoto chenye uwezo wa kujisogeza au kujitembeza? Au makalio laini laini?
Mikono ikishika, kuhisi na kutembeza kichwa cha mtoto aliyeko tumboni
Kamata sehemu ya mfupa wa nyonga. Ni ngumu au laini? Unapokamata, unaweza kukitembeza kilichomo sehemu zingine za mwili kwa uhuru?
Mikono ikigusa na kuhisi kichwa cha mtoto ndani ya eneo la mfupa wa nyonga
Tumbo la mwanamke mjamzito, mtoto akionekana akiwa amelalia upande katikati ya njia ya uzazi

Kama mtoto atakuwa ametanguliza makalio wakati wa muda wa kujifungua, ni salama zaidi kujifungulia hospitali. Lakini kama unajikuta na mama ambaye anakaribia kujifungua mtoto ambaye ametanguliza makalio, bonyeza hapa.

Mtoto aliyelala katikati ya njia ya uzazi (ambaye hajakaa wima) hawezi kuzaliwa kupitia ukeni. Kama mtoto atakuwa amelalia upande wakati uchungu wa uzazi unaaza, apelekwe hospitalini haraka. Huenda operesheni ikahitajika.

Mapigo ya moyo wa mtoto

Zifikapo wiki 20 (takriban miezi 4½) ya ujauzito, unapaswa kuwa katika hali ya kusikia mapigo ya moyo wa mtoto kwa kutumia kifaa maalum cha kusikilizia-fetoskopu, na wiki chache baadaye kwa kutumia kifaa kingine cha stesoskopu. Moyo wa mtoto mwenye afya huongeza na kupunguza kasi ya mapigo lakini mapigo hubaki kati ya 120 na 160 kwa dakika. Hii inakaribia mara 2 mapigo ya mtu mzima. Mapigo yanaweza kupungua mtoto anapokuwa amelala. (Kama utasikia mapigo ya moyo kati ya 60 na 80, huenda unasikiliza mapigo ya mama, na siyo ya mtoto). Tumia saa yenye ulimi wa pili unaohesabu sekunde, au yenye uwezo wa kurekebishwa na kuhesabu mapigo ya moyo kwa dakika moja.

Sikio la mfanyakazi wa afya likiwa kwenye kifaa cha fetoskopu kilichowekwa juu ya tumbo la mama
mtoto akiwa tumboni, mshale ukionesha sehemu ya juu mgongoni mwa mtoto mahali ambapo mapigo ya moyo husikika zaidi
Kichwa chini
Mapigo ya moyo wa mtoto husikika zaidi katika hatua hii
mtoto akiwa tumboni kichwa chake kikiangalia juu; mshale unaonesha sehemu ya juu mgongoni mwa mtoto ambapo mapigo ya moyo husikika zaidi
Kutanguliza
makalio
Mfanyakazi wa afya akimsikiliza mtoto kwa kutumia Fetoskopu kupitia tumbo la mama yake Baada ya wiki 20 za ujauzito,mapigo ya moyo wa mtoto huweza kuonesha jisi mtoto alivyokaa kwenye tumbo la mama yake.

Kama mapigo ya moyo yatabaki chini ya 120, au kwenda kasi zaidi ya 160, au wakati wote kuonekana kuwa katika kasi ile ile bila mabadiliko, huenda mtoto ana matatizo na anahitaji msaada zaidi wa daktari.

Mwisho, kama utagundua kuwepo mapigo ya moyo mawili tofauti, huenda kuna mapacha.

Andaa mpango kwa ajili ya dharura

Kila dharura inayojitokeza wakati wa kujifungua inatibika. Kuvuja damu, mashambulio ya kifafa cha mimba, maambukizi, uchungu unaoendelea muda mrefu, vyote vinaweza kudhibitiwa kwa matumizi ya dawa sahihi, au wakati mwingine kwa njia ya operesheni kwenye hospitali zenye vifaa na watalaam wa kutosha.Tatizo hapa ni kupata huduma hii wakati inapohitajika. Kumbuka ni nadra kupata tahadhari ya kutosha kabla jambo baya halijatokea wakati wa uzazi. Fedha, usafiri, na ushirikiano kutoka kwa wanafamilia na majirani vinahitaji kuandaliwa mapema hata kabla uchungu wa uzazi haujaanza.

mama mjamzito akibebwa kutoka nyumbani kuelekea kwenye gari ili aweze kupelekwa hospitalini akisindikizwa na mfanyakazi wa afya

Wakutanishe mama mjamzito na watu wake wa karibu: mume wake, mama mkwe, au mwingine yeyote yule, na kuamua kipi kitahitajika iwapo dharura itatokea. Mahitaji yanaweza kujumuisha:

 • Kutumia gari la mtu Fulani au gari lingine.
 • Fedha za kulipia huduma za hospitali.
 • Kupata ruhusa mapema kutoka kwa wanaofanya maamuzi katika familia.

Kama upo mbali na kituo cha afya au hospitali, kwa wiki chache zitakazokuwa zimebaki kujifungua, fikiria kuhamia kwa ndugu au jamaa anayeishi karibu na hospitali.



Ukurasa huu ulihuishwa: 10 Mei 2024