Hesperian Health Guides

Jinsi ya kuendelea kuwa na afya bora wakati wa ujauzito

Katika sura hii:

Mama na mtoto wake wanaweza kuendelea kuwa na afya bora kwa:

  • Kupata chakula cha kutosha chenye virutubishi.
  • Kupumuzika sana kila siku.
  • Kuepuka kemikali, pombe, moshi, na sehemu kubwa ya madawa.
  • Kupata huduma kutoka kwa mkunga au mfanyakazi wa afya mwingine ambaye anaweza kutibu, au kusaidia kupata matibabu kwa ajili ya tatizo lolote la kiafya ambalo linaweza kujitokeza.
  • Upendo na huruma.

Kula chakula cha kutosha chenye virutubishi

Mchanganyiko wa chakula chenye virutubishi kitamfanya mwanamke awe na nguvu na afya; aweze kupata nguvu za kujifungua na kumhudumia mtoto. Kama mwanamke mjamzito hali chakula cha kutosha, inawezekana anawachia chakula wana familia wengine, au mama mkwe kwa nia njema katika uelewa wake amemwambia asile baadhi ya vyakula au asiongezeke uzito ili aweze kujifungua kwa urahisi. Kumbuka mwanamke analazimika kula chakula cha kumtosha yeye na mwanae. Hivyo anahitaji kula chakula zaidi kuliko watu wazima wengine na siyo kidogo kuliko wao.

Wanawake wajawazito, kama watu wengine, wanahitaji mchanganyiko wa protini, mbogamboga,matunda, na wanga. Pia wanapaswa kula mara nyingi zaidi, wakipata vyakula vidogo vidogo kati ya milo ya kawaida siku nzima. Kwa ushauri kuhusu ulaji bora, angalia Lishe bora hutengeneza afya bora.

Vyakula mbalimbali tunavyohitaji kwa ajili ya afya bora, vikiwemo vya wanga, protini, na matunda na mbogamboga zenye vitamini nyingi

Vyakula mchanganyiko hulinda afya ya mama na mtoto.


Zuia upungufu wa chembe nyekundu za damu (anemia)

Anemia (upungufu wa chembe nyekundu kwenye damu) hutokea sana wakati wa ujauzito. Husababisha kujisikia mchovu kila mara. Anemia ni hatari zaidi hasa kwa akinamama wajawazito kwa sababu damu hupotea wakati wa kujifungua. Hii inaweza kuzidisha upungufu huo na kusababisha mama kupoteza maisha. Zuia anemia kwa kula vyakula vyenye protini na wingi wa madini chuma, na pia kutumia dawa ya kuongeza madini chuma mwilini. Bonyeza hapa kwa ajili ya taarifa zaidi juu ya madini chuma na njia zingine za ziada za kuongeza madini chuma mwilini.

Malaria (angalia Baadhi ya magonjwa hatari ya kuambukiza (kinaandaliwa) na minyoo ya safura) vinaweza kusababisha anemia na hivyo hutakiwa kutibiwa mara moja.

Vyakula vyenye wingi wa madini chuma vikiwemo molasi (sukari guru), maini, samaki, mayai, mboga za majani
Akina mama wajawazito wanahitaji vyakula vyenye wingi wa madini chuma.

Asidi ya foliki

Ukosefu wa asidi ya foliki (au vitamini ya foleti) kunaweza kusababisha hitilafu katika umbaaji wa mtoto na hata ulemavu. Chagua dawa za kuongeza madini chuma mwilini ambazo zinajumuisha asidi ya foliki, au dawa za kuongeza foliki mwilini. Bonyeza hapa kwa taarifa zaidi juu ya asidi ya foliki.

Vitamini A

Matunda na mbogamboga yakiwemo karoti na nyanya Mbogamboga za kijani na matunda ya rangi ya chungwa huwa na vitamini A, kirutubishi ambacho kinahitajika kwa ajili ya afya ya macho. Mwanamke mjamzito anahitaji mbogamboga za kijani na matunda ya rangi ya chungwa zaidi kwa sababu vitamini A anayokula hutumika kwanza kukidhi mahitaji ya mtoto. Ukosefu wa vitamini A unaweza kusababisha kutoona usiku au upofu kwa ujumla.

Kupumzika

Wahimize wanafamilia na majirani kumsaidia mama mjamzito katika kazi na majukumu yake. Mkumbushe, hasa ujauzito unapozidi kukua, kupumzika na kuinua miguu yake juu mara kadhaa kwa siku au kulala chini wakati wa alfajiri. Kulea ujauzito ni kazi kwa mwili; nao mwili unahitaji kupumzika.

Epuka Matumizi ya Bidhaa Hatari

Mwanaume akiongea na mwenzake ambaye anakaribia kuwasha sigara

Usivute sigara ndani rafiki yangu, dada yangu ni mjamzito!

Moshi na sigara

Sigara na tumbaku huathiri mapafu ya mama na vinaweza kusabisha saratani na hata kifo. Moshi unaweza kusababisha mtoto kuzaliwa kabla ya muda wake au akiwa na uzito mdogo sana, au akiwa amekwisha kufa. Akina mama na watoto wao wanaweza hata kudhurika kutokana na watu wanovuta sigara karibu nao. Ikumbushe familia na wengine kuepuka kuvuta sigara katika chumba kimoja au kweye gari wanapokuwa na mama mjamzito au watoto.

Pombe na madawa ya kulevya

Mama mjamzito anapokunywa pombe, pombe hiyo huenda kwa mwanae na inaweza kusababisha hitilafu za kudumu kwenye ubongo wa mtoto na mwili wake. Kadri anavyozidi kunywa pombe nyingi ndivyo madhara kwa mtoto yanavyongezeka. Vivyo hivyo, madawa ya kulevya yakiwemo kokeni, bangi, unga na madawa mengine ni hatari kwa akinamama wajawazito na watoto wao. Angalia Madawa ya kulevya, pombe na tumbaku (kinaandaliwa) kwa msaada zaidi juu ya madawa na pombe.

Madawa ya kawaida

Dawa nyingi anapozitumia mwanamke mjamzito pia humfikia mtoto wake. Kwa sababu watoto tumboni wanakuwa wadogo sana na wakiendelea kuumbika, dawa ambazo ni salama kwa mtu mzima zinaweza kusababisha hitilafu wakati wa kujifungua na hata madhara kwa mtoto. Hivyo akina mama wajawazito wanapaswa kuepuka kutumia dawa holela. Kupumzika na vinywaji laini — siyo dawa — ndiyo tiba bora zaidi kwa matatizo madogo madogo kama vile maumivu ya kichwa, maumivu ya tumbo, na mafua.

Chupa za dawa na vidonge
Isipokuwa tu kama una uhakika yanahitajika, ni bora zaidi kuepuka madawa wakati wa ujauzito.

Lakini baadhi ya magonjwa ni hatari sana kuyaachia bila kuyatibu katika kipindi chote cha ujauzito. Ugonjwa unaweza kuwa hatari pia kwa mtoto. Magonjwa kwa wanawake wajawazito ambayo yanapaswa kutibiwa na dawa ni pamoja na:

  • malaria. Angalia pia Baadhi ya magonjwa hatari ya kuambukiza (kinaadaliwa).
  • VVU na UKIMWI. Angalia VVU na UKIMWI (kinaadaliwa).
  • maambukizi ya njia ya mkojo. Angalia pia Matatizo katika utoaji mkojo (kinaadaliwa).
  • maambukizi kupitia ngono kama vile klamidia, kisonono, na kaswende. Angalia pia Matatizo na maambukizi ya via vya uzazi (kinaandaliwa).

Ili kujua iwapo dawa yeyote ile ni salama kutumia wakati wa ujauzito na wakati wa unyonyeshaji, muulize mfanyakazi wa afya mwenye uzoefu. Angalia pia sehemu ya dawa mwishoni mwa sura hii, au rejea miongozo mingine juu ya matumizi ya dawa. Kwa dawa ambazo zinahitajika lakini siyo salama, kawaida huwa kuna dawa nyingine mbadala ambayo inaweza kutumika.

Dawa za asili na mimea/mitidawa zinaweza kusababisha madhara zaidi kuliko kutoa tiba. Kitabu kiitwacho Dawa, vipimo na matibabu (kinaandaliwa) kimependekeza njia za kuzingatia unapotaka kufanya maamuzi juu ya matumizi ya dawa za asili.

Epuka kukutana na wagonjwa

Mtoto wa kike mwenye upele usoni na mwili mzima

Kuugua wakati wa ujauzito ni taabu kubwa. Ugonjwa unaweza kusababisha taabu kubwa katika kula, na kutokula chakula cha kutosha humunyima mwanamke mjamzito nguvu. Epuka kukutana na wagonjwa kupunguza uwezekano wa kuambukizwa.

Ugonjwa wa Rubella ambao ni aina ya surua kawaida siyo hatari sana. Lakini unapompata mwanamke mjamzito unaweza kusababisha hitilafu katika viungo na hata ulemavu kwa mtoto akiwa tumboni. Katika kumlinda mtoto, mwanamke mjamzito anapaswa kuepuka watu wenye upele, hasa watoto, ambao mara nyingi hupatwa maambukizi hayo. Hata watoto wengine wa mama mjamzito ambao wanaumwa wanapaswa kuhudumiwa na wanafamilia wengine au marafiki. Kampeni ya chanjo kwa jamii nzima ndiyo kinga bora zaidi kwa wanawake wote.

Huduma ya mkunga au mfanyakazi mwingine wa afya

Mkunga mzoefu au mfanyakazi wa afya mwingine anaweza kumshauri mwanamke mjamzito jinsi ya kuishi na afya nzuri na salama, kutibu magonjwa yote ya kawaida na kupunguza kero, na kutambua lini mwanamke mjamzito anapohitaji kutafuta msaada kwenye hospitali au kituo cha afya. Wanawake wote wanapaswa kuhudumiwa na mfanyakazi wa afya mwenye huruma na ueledi wakati wa ujauzito, pale wanapojifungua na katika wiki zinazofuata.

Chanjo

Mwanamke mjamzito anapaswa kuchanjwa dhidi ya pepopunda (tetanasi) mapema iwezekanavyo katika ujauzito. Anatakiwa kupewa chanjo nyingine wiki 4 baadaye iwapo atakuwa hajapata chanjo zote. Hii husaidia kuwalinda wote wawili-mama na mtoto wake. Kwa taarifa zaidi angalia Chanjo (kinaandaliwa).

Vipimo vya Maabara

Vipimo rahisi vinaweza kugundua baadhi ya magonjwa mengi ambayo ni hatari kwa wanawake na watoto wachanga. Vipimo hivi huwatahadharisha mama na mfanyakazi wa afya kuanza matibabu mara moja, hatua ambayo inaweza kuzuia matatizo makubwa wakati na baada ya kujifungua. Ni busara kufanya vipimo dhidi ya:

  • anemia (kwa kutumia kipimo maalum cha himoglobini).
  • kaswende.
  • malaria (kwa kutumia vipimo ambavyo hutoa majibu haraka kwa maeneo ambapo malaria ni ugonjwa wa kawaida).


Kipimo cha VVU kinatakiwa kutolewa kwa akina mama wote wajawazito. Mwanamke anapogundua ana VVU, anaweza kuanza kutumia dawa ya kumsaidia afya yake na kumlinda mtoto asiambukizwe VVU. Sura ya VVU na UKIMWI (kinaandaliwa) inajumwisha taarifa juu ya upimaji na dawa ambazo wanawake wajawazito wenye VVU wanapaswa kutumia.

NWTND pab Page 6-1.png

Kuna aina mpya ya vipimo vya VVU ambavyo havihitaji maabara na hufanyika kwa urahisi kwa kutumia kifaa kidogo kupangusha ndani ya mdomo au ukeni, au kuchukua tone la damu kutoka kwenye tundu dogo kwenye kidole. Ulizia kwenye kituo cha afya kilichoko karibu iwapo vipimo hivi hutolewa na serikali, au kama kuna shirika lolote ambalo linatoa huduma hiyo.