Hesperian Health Guides

Baada ya kujifungua

Baada ya kujifungua, msaidie mama kutoa kondo la nyuma na kudhibiti uvujaji damu. Angalia Watoto wachanga na unyonyeshaji kwa taarifa zaidi juu ya kumhudumia mtoto na kuanza unyonyeshaji.

Uvujaji damu

Fuatilia kwa karibu uvujaji damu wa mama na kumkagua mara kwa mara. Inua nguo na vingine vinavyotumika kumfunika kukagua kama damu inajikusanya chini yake. Kawaida damu kidogo hutoka kwa kasi baada ya kondo la nyuma kutoka. Hii ni sawa. Lakini damu ikitoka nyingi kwa kasi au kuendelea kuchuruzika kidogo kidogo kwa muda ni hatari na inahitaji hatua za dharura. Katika hali ya kuvuja sana damu:

 • Msaidie kulitoa kondo la nyuma
 • Msaidie kukojoa
 • Kanda au pangusa pangusa tumbo
 • Mpe dawa kusimamisha uvujaji damu
Mama amekaa kitandani wakati mama mwingine akimsaidia kusinga au kupangusa tumbo

Kusinga au kukanda tumbo

Singa au kanda tumbo la mama ambaye ametoa kondo la nyuma kila baada ya takriban dakika 15 au, wakati wote utakapoona dalili ya damu kutoka. Kanda kwa nguvu na ndani, hadi tumbo la uzazi litakapokuwa kama mpira mgumu katikati ya tumbo la kawaida, chini ya kitovu. Kama tumbo la uzazi limekaa upande mmoja, hii inaashiria kuwa kibofu cha mkojo kimejaa na mama anapaswa kuutoa mkojo.

Kama uvujaji damu utaongezeka, kanda zaidi, ukikanda tumbo la uzazi kwa kutumia mikono yako miwili. Itauma lakini itasaidia.


Tumbo la mama, mkono mmoja ukiwa umejipinda kama kikombe ukikanda juu ya tumbo na mkono mwingine ukiwa umekunjwa kama ngumi sehemu ya chini ya tumbo la uzazi.
Kanda tumbo la uzazi hadi litakapokuwa gumu. Baada ya hapo kunja mkono mmoja uwe kama kikombe na kukanda sehemu ya juu ya tumbo la uzazi. Kunja mkono wako mwingine kama ngumi na weka sehemu ya chini ya tumbo la uzazi.
Kunja mkono wako mwingine kama ngumi na weka sehemu ya chini ya tumbo la uzazi.

Kama uvujaji damu hautasimama, unaweza kuingiza mkono mmoja ukeni, kunja ngumi na baada ya hapo tumia mkono mwingine ulioko nje kukanda tumbo kuelekea ule wa ndani uliokunjwa kama ngumi.

Dawa za kusimamisha uvujaji mkubwa wa damu

Uvujaji damu mara nyingi husimama kwa kutumia dawa ya oksitosini na misoprosto.

 • Choma vipimo 10 vya oksitosini kwenye msuli wa upande mmoja wa paja la mama. (Kwa taarifa zaidi juu ya jinsi ya kuchoma sindano angalia Dawa, vipimo, na tiba - kinaandaliwa.)


AU

 • Mpe makrogramu 800 za misoprosto ziyeyuke chini ya ulimi kwa dakika 30.


Uvujaji damu nyingi unaweza pia kuzuiwa kwa kutumia dawa hizi. Kwa sababu hii, baadhi ya wafanyakazi wa afya huwapatia akina mama aidha dozi moja ya mikrogramu 600 ya misoprosto mara moja tu au sindano moja ya oksitosini mara baada ya kujifungua, hasa kama wanaweza kuzipata dawa hizo kwa urahisi. Kama unahisi uwezekano wa uvujaji damu nyingi na unao uwezo wa kutoa dawa moja wapo, endelea.

Dalili za uvujaji damu mkali
Mama mgonjwa amebebwa na mwanaume, mwanamke mwingine akiwa amesaidia kumbeba mtoto wake

Tafuta msaada wa daktari haraka utakapoona dalili zifuatazo na, ukiwa njiani, saidia kumpunguzia mgonjwa mshtuko (angalia Huduma ya kwanza).

 • Kupepesuka
 • Mwili kukosa nguvu
 • Kuzirai
 • Kuchanganyikiwa
 • Ngozi baridi, yenye unyevu au inayonata
 • Mpwito kwenye mshipa unaotoa damu kutoka kwenye moyo kwenda kasi au kuongezeka
 • Shinikizo la damu la chini au kupungua

Chunguza sehemu zilizochanika au kujeruhiwa

Sehemu ndongo ikichanika hupona bila dawa. Lakini sehemu kubwa ikichanika, hasa kwa kwenda ndani, hupona kwa kushonwa mishono michache. Mshono husaidia pia kusimamisha uvujaji damu iwapo kuna mshipa wa damu ndani ya uke ambao umechanika.

Uke, sehemu yake ya chini ikiwa imechanika
Kwa uangalifu unganisha sehemu mbili zilizochanika kabla ya kuanza kushona.

Taratibu weka kidole cha mkono uliovalishwa glovu ndani ya sehemu iliyochanika kuona kina chake. Kama unajua jinsi ya kushona, tumia mishono michache tu. Kama sehemu ilichanika kwa kwenda ndani sana, kwanza tumia mishono miwili inayoyeyuka polepole kwenye msuli kabla hujashona ngozi na kuiunganisha pamoja. Usiache mwanya ambao unaweza kusababisha usaha kujikusanya. Kwa taarifa zaidi juu ya ushonaji, angalia Huduma ya kwanza. Lakini kama huna uzoefu na ushonaji, ni heri kuacha kidonda kikapona chenyewe.

Kama mchaniko umeenda hadi kwenye njia ya kutolea kinyesi, msulibanifu kwenye unyeo lazima ushonwe pamoja kwanza kabla mchaniko mzima haujashonwa. Daktari mwenye uzoefu wa kutosha wa kuunganisha tishu au maungio ya mwili baada ya majeraha ndiyo anapaswa kuifanya kazi hii au huenda mama asiwe na uwezo tena wa kudhibiti kinyesi kutoka.