Hesperian Health Guides
Uchungu wa uzazi na kujifungua
HealthWiki > Toleo Jipya: Mahali Pasipo na Daktari > Ujauzito na kujifungua > Uchungu wa uzazi na kujifungua
Kila jamii ina utaratibu wake wa kuwahudumia wanawake wanapokuwa katika uchungu wa uzazi. Utaratibu salama zaidi pengine ungekuwa ni kuruhusu mpangilio wa asili kwa ajili ya binadamu kuchukua mkondo wake, lakini wakati huo kubaki makini kuangalia dalili zozote za hatari. Kumbuka:
- Sehemu kubwa ya uzazi huwa ni salama na yenye afya.
- Mtie moyo mama mjamzito. Shika mkono wake, ongea naye taratibu, muonyeshe jinsi ya kupumua pumzi nzito zinazokwenda polepole.
- Msaidie kumgeuza, kutembea, kubadilisha ukaaji, na hata kutoa sauti.
Kama kuna dalili za matatizo, usichelewe- wezesha mama kupelekwa hospitali mara moja.
Dalili za hatari wakati wa ujauzito |
|
Yaliyomo
Sehemu ya kujifungulia
Kwa ajili ya kujifungua salama, andaa vifaa vifuatavyo:
Sabuni na maji kwa ajili ya kunawa mikono mara kwa mara, kumsafisha mama, na kusafisha vifaa tiba. | Viwembe vipya au mkasi wenye makali kwa ajili ya kukata kiungamwana. | ||
Dawa kwa ajili ya kusimamisha uvujaji damu: oksitosini, misoproso. | Jozi nyingi za mipira ya kuvaa mikononi au glovu kulinda afya ya mama, mtoto na mkunga. | Kamba zilizotakaswa na dawa au kuchemshwa, au riboni au kibanio maalum kwa ajili ya kufunga au kubana kitovu. |
Familia au mfanyakazi wa afya anatakiwa pia kukusanya:
Nguo nyingi safi au taulo kwa ajili ya kumfuta na kumfunika mtoto ili apate joto la kutosha. | Tochi kwa ajili ya kumulikia wakati mtoto akizaliwa na kumwangalia mtoto mwenyewe. |
Maji kwa ajili ya kunywa na usafi. | Bakuli kubwa au benseni kwa ajili ya kunawia na kupokea kondo la nyuma. |
Vifaa vingine muhimu kwa ajili ya mfanyakazi wa afya au mkunga:
- Taarifa au kumbukumbu za kiafya za mama
- Kifaa kipya kwa ajili ya kuvuta kamasi kutoka kwenye mdomo na pua za mtoto.
- Kifaa cha fetoskopu, stesoskopu, na kifaa cha kupima shinikizo la damu.
- Sindano na nyuzi maalum kwa ajili ya ushonaji wa sehemu zilizochanika wakati wa kujifungua.
Mwanzo wa kujifungua
Uchungu wa uzazi
Uchungu wa uzazi ni kubana na kuachia, kwa kurudiarudia, kwa misuli katika tumbo la uzazi. Misuli inavyobana na kuachia, taratibu husababisha kufunguka kwa mlango wa tumbo la uzazi. Baada ya mlango mzima kufunguka, mtoto anaweza kutoka nje ya tumbo la uzazi na hatimaye nje kupitia uke wa mama.
Kubana na kuachia kwa misuli huanza polepole wakati wa siku za mwisho wa ujauzito. Mkazo au mbanano wa tumbo la uzazi mwanzoni hauchukui muda mrefu - huachia mama anapopumzika. Lakini uchungu wa uzazi wa ukweli huja kwa nguvu. Ukianza, huja mara kwa mara, na kwa utaratibu, kila baada ya dakika chache. Hauachii hata mama akilala chini au kupumzika.
Kuvunjika kwa mfuko wa maji ya uzazi
Mfuko wa maji ya uzazi unaweza kuvunjika na kuachia maji mengi ghafla au kuachia maji kidogo kidogo. Kuachiwa kwa maji ya uzazi kunaweza kuwa ndiyo dalili ya kwanza ya uchungu wa uzazi kabla ya misuli haijaanza kubana au kukaza na kuachia. Au huenda maji mengi yakaachiwa ghafla wakati wa uchungu wa uzazi. Wakati mwingine, mtoto huzaliwa kwenye mfuko wa maji bila mfuko huo kukatika. Hali zote hizi ni kawaida.
Ndani ya tumbo la uzazi, mfuko huo humlinda mtoto dhidi ya vijidudu vinavyosababisha magonjwa. Baada ya mfuko kuvunjika, vijidudu hivyo vinaweza kusababisha maambukizi kwenye tumbo la uzazi na kwa mtoto. Kwa sababu hiyo, hatari ya maambukizi huongezeka kutegemea na urefu wa muda ambao mfuko huo utabaki ukiwa umevunjika. Usiweke chochote ukeni baada ya mfuko wa maji ya uzazi kuvunjika. Kama mfuko utavunjika na saa 12 – siku 1 au usiku 1 ukapita bila uchungu wa uzazi kuanza, nenda hospitali mahali ambapo uchungu unaweza kuanzishwa kwa kutumia dawa.
Kusaidia kuanzisha uchungu wa uzazi
Unaweza kusaidia uchungu wa uzazi uanze, au kuuongeza kasi kama umekuja polepole mno katika hali zifuatazo:
- Ujauzito ambao umepitiliza siku. Ujauzito wa zaidi ya wiki 41 unaweza kusababisha matatizo kwa mtoto.
- Mfuko wa maji ya uzazi kuvunjika. Baada ya mfuko wa uzazi kuvunjika, saidia kuanzisha uchungu wa uzazi ili kuepuka maambukizi.
- Uchungu wa uzazi ambao unaendelea taratibu mno. Saidia kuanzisha au kuongeza kasi ya uchungu wa uzazi ili mama asiishiwe nguvu.
Anza na njia ya kwanza na kama haitafanikiwa, jaribu inayofuata:
- Mhimize atembee, kucheza, au kupanda ngazi za ghorofa au kupanda mlima.
- Singa chuchu zake kama vile unakamua maziwa, au anyonyeshe mtoto. Hayo yanapaswa kusisimua misuli kuanza kubana na kuachia.
- Changanya ¼ kikombe cha chai cha mafuta ya mbarika, nyonyo au mbono na aina yoyote ya juisi ya matunda na kumpatia mama kunywa. Hii mara nyingi husababisha kuharisha kukiwa na maumivu, lakini pia inaweza kuchochea mwenendo wa misuli kwanza kubana na kuachia.
¼ kikombe cha mafuta ya mbarika au nyonyo au mbono
Juisi ya matunda
|
Huenda kukawa na dawa za mitishamba ambazo hutumika katika jamii yako kuchochea uchungu wa uzazi kuanza. Baadhi ya dawa hizi zinaweza kuwa salama, lakini zingine siyo salama. Kabla hujazitumia jiulize kwanza: mimea hii iliwahi kuwasaidia wanawake wengine kuanzisha uchungu wa uzazi?. Wanawake wamewahi kupata matatizo ya kiafya baada ya kutumia dawa hizi? Je dawa hizi zimekuwa zikitumika kwa muda mrefu au zimeanza kutumika hivi karibuni? Angalia Dawa, vipimo na matibabu (kinaandaliwa) kwa mawazo zaidi kuhusu jinsi ya kujua iwapo dawa ya mitishamba ni salama.
- Usijaribu kuanzisha uchungu wa uzazi kama mtoto amekaa upande katikati ya njia ya uzazi.
- Usipoteze muda kujaribu kuanzisha uchungu wa uzazi kama upo mbali na hospitali. Badala yake, tumia muda wako kwenda hospitali.
- Kamwe usimpe mama mjamzito dawa za oksitosini, misoprosto, au dawa zingine za kiasasa kuanzisha uchungu wa uzazi nyumbani. Dawa hizi ni kali mno –zinaweza kusababisha kifo.
Kumsaidia mama mjamzito akiwa kwenye uchungu wa uzazi
Msaada mkubwa zaidi ambao unaweza kumpa mama mjamzito ajifungue kwa usalama ni kumtia moyo kwa upendo. Epuka kuingiza vidole vyako ukeni kuchunguza mlango wa kizazi. Hakuna ulazima wa kufanya hivyo katika hali ya uchungu wa uzazi wa kawaida. Hii inaweza kusababisha maambukizi kwa mama na mtoto. Usiminye au kubonyeza tumbo la mama au kutumia nguo au kitambaa kumvuta mtoto nje.
Katika hali nyingi za uchungu wa uzazi, bora kuangalia tu kuliko kuingilia kati.
Wakati wa mwanzo wa uchungu wa uzazi, mfanyakazi wa afya anapaswa tu kumtia moyo mama. Mkumbushe:
- Kupumua pole pole, kupuliza au kuhema, au kuachia sauti zozote zile kupunguza maumivu wakati misuli inabana na kuachia.
- Kunywa kidogokidogo vinywaji laini kila baada ya muda mfupi, na kula kiasi kidogo cha chakula.
- Kojoa kila baada ya saa kadhaa. Kibofu kilichojaa mkojo huchelewesha kujifungua.
Chunguza dalili za afya ya mama na mtoto
Kama unajua jinsi, pima shinikizo la damu la mama, mpwito kwenye mshipa unaotoa damu kutoka kwenye moyo, halijoto ya mwili, mkao wa mtoto katika tumbo la uzazi, na mapigo ya moyo, mara baada ya uchungu kuanza. Endelea kufanya uchunguzi mara kwa mara wakati wa uchungu wa uzazi. Dalili hizi zinaweza kukuambia iwapo mama anapata maambukizi au yupo hatarini kupata kifafa cha mimba, au mtoto ana matatizo.
Chunguza uwezekano wa kifafa cha mimba: Pima shinikizo la damu. Kiwango cha shinikizo la damu cha 160/110 na zaidi kinaonesha hali inayotangulia kifafa cha mimba. Tafuta msaada haraka.
Chunguza uwezekano wa maambukizi: Pima halijoto ya mwili wa mama. Kawaida huwa inapanda wakati wa uchungu wa uzazi, lakini nyuzijoto 38 sentigredi au zaidi kawaida huashiria uwepo wa maambukizi. Wakati uambukizo (kama vile malaria au kwenye njia ya mkojo) huweza kutokea wakati wa uchungu wa uzazi,zingatia zaidi maambukizi yanayoweza kutokea ndani ya tumbo la uzazi. Dalili zingine za maambukizi ndani ya tumbo la uzazi ni:
- Mpwito wa mshipa wa mama unaosafirisha damu kutoka kwenye moyo ni zaidi ya 100 kwa dakika.
- Mapigo ya moyo wa mtoto ni zaidi ya 180 kwa dakika.
- Uke wa mama unatoa harufu mbaya.
- Tumbo la kawaida la mama lina vidonda au ni laini laini linapoguswa.
Tibu mara moja maambukizi ndani ya tumbo la uzazi kwa kutumia ampisilini na jentamaisini na endelea kutoa tiba hiyo baada ya mtoto kuzaliwa. Kama dalili za maambukizi ni mbaya sana, mpe pia metronidazoli. Bonyeza hapa kwa maelezo zaidi juu ya dawa hizi. Pia tafuta msaada.
Chunguza iwapo mtoto yupo katika hali nzuri: Mapigo ya moyo wa mtoto ambayo hubaki katika 120, au kwenda chini ya 100, ni dalili kwamba mtoto hapati hewa ya oksijeni ya kutosha na yupo hatarini. Mtoto anaweza kupoteza maisha, lakini hakuna lingine la kufanya isipokuwa kusaidia mtoto kuzaliwa.
Muda wa uchungu wa uzazi
Kila mwanamke ana uchungu wa uzazi tofauti na hii ni kawaida. Uchungu wa uzazi wenye afya unaweza kuwa wa haraka sana au kuchukua saa nyingi. Hata hivyo, baadhi ya watoto hukwama na hawatazaliwa bila matibabu au operesheni. Fikiria utachukuwa muda gani kufika hospitali. Kama upo mbali sana na uchungu wa uzazi umeendelea kwa saa kadhaa, anza mapema kuelekea kwenye kituo cha afya au hospitali.
Kusukuma mtoto
Mara mama mjamzito anapohisi haja ya kusukuma, anaweza kufanya hivyo kwa usalama. Mara nyingi, wanawake hujua jinsi ya kusukuma wakati wa kujifungua bila msaada. Usimkaripie mama.
Kuchuchumaa, kupiga magoti na kuegemea mikono, na kupanua miguu ukiegemea mito mgongoni - yote ni mikao mizuri ya kusukuma mtoto. Kama mkao mmoja hauwezi kumtoa mtoto nje, jaribu mkao mwingine. |
Hatua ya kusukuma mtoto kawaida huonekana kuwa nafuu kwa mama kuliko hatua za awali katika uchungu. Kama uchungu wa uzazi umechukua muda mrefu, mama anaweza kuibiwa na usingizi kidogo ghafla katikati ya minyukano ya misuli na akiamuka huanza kusukuma tena. Kama usukumaji utakuchukua muda mrefu:
- Mtie moyo mama abadilishe mkao.
- Mwambie mama akakojoe. Kibofu kilichojaa mkojo hupunguza kasi ya uchungu.
- Mwambie apumzike katikakati ya minyukano hiyo ya misuli, halafu apumue pumzi zito la ndani na kusukuma tena kwa nguvu kadri awezavyo.
Baada ya saa 2 za kusukuma kwa nguvu bila mafanikio, tafuta msaada wa daktari. Huenda operesheni ikahitajika kumtoa mtoto.
Kama mtoto ametanguliza makalio: Unaweza kuhisi mtoto ambaye ametanguliza makalio au miguu kwa kugusa tumbo la mama la kawaida. Kama utaona kinyesi kingi cha awali cha mtoto mchanga kikitoka nje ya uke wa mama wakati wa uchungu wa uzazi, mtoto anaweza kuwa ametanguliza makalio au miguu. Bonyeza hapa kujua jinsi ya kusaidia watoto kama hao kuzaliwa.