Hesperian Health Guides

Mshituko

Katika sura hii:

NWTND fa Page 10-2.png

Mshituko ni hali inayotishia uhai ambayo inaweza kutokana na kuvuja sana damu, kupungukiwa na maji mwilini, vidonda na majeraha makubwa kutokana na moto, mzio, au maambukizi kwenye damu (sepsisi). Aina hii ya mshituko ni tofauti na mshituko kutokana na kitisho au fadhaa. Mwili huanza kudorora, ukipoteza uwezo wa kufanya kazi zake za msingi. Mara dalili za mshituko zinapoanza, hali huzidi kuwa mbaya haraka. Tibu mshituko haraka ili kuokoa maisha ya mgonjwa.

Dalili
  • Woga na mfadhaiko, halafu kuchanganyikiwa, kukosa nguvu, na kupoteza fahamu
  • Jasho baridi: ngozi ya mwili hupauka, kuwa baridi na yenye unyevunyevu
  • Kukosa nguvu na mapigo ya moyo kwenda haraka
  • Kiwango cha shinikizo la damu kushuka
Matibabu

Tafuta msaada. Ukiwa njiani:

  • Tibu chanzo cha mshituko haraka iwezekanavyo: kusimamisha uvujaji damu tumia njia ya mgandamizo. Kwa ajili ya mwili kupungukiwa maji, mpe kinywaji maalum cha kuongeza maji mwilini. Kama chanzo cha mshituko ni maambukizi kwenye damu (sepsisi), dawa za antibiotiki zitahitajika haraka.
  • Mwezeshe mgonjwa kubaki katika hali ya vuguvugu (au mpunguzie baadhi ya nguo iwapo anasikia joto).
  • Inua miguu, ukisaidia kuyaimarisha magoti.
  • Kama mgonjwa anaweza kukamata kikombe mwenyewe, mpe maji ya kunywa au hata kinywaji maalum cha kuongeza maji mwilini
  • Kuwa mtulivu na mpe matumaini.
  • Mwongezee maji mwilini kupitia njia ya haja kubwa au dripu ya kawaida kupitia mshipa wa damu. Angalia Stadi za mfanyakazi wa afya (kinaandaliwa) wakati ukiendelea kutafuta msaada wa kiafya.


NWTND fa Page 11-1.png