Hesperian Health Guides
Vyoo kwa ajili ya watoto
HealthWiki > Mwongozo wa jamii juu ya afya ya mazingira > Sehemu ya kwanza: Ujenzi wa vyoo na matumizi yake > Vyoo kwa ajili ya watoto
Watoto wanapokuwa na vyoo ambavyo vinafaa hali zao, hujisikia salama kuvitumia, hubaki wasafi, na matukio ya kuugua hupungua. Vyoo vya shimo vinaweza kuwa hatari na kuwaogopesha watoto wadogo kwa sababu ya giza na tundu kubwa la choo. Watoto wengi, hasa wasichana, huacha shule kwa sababu ya ukosefu wa vyoo salama.
Kuwaruhusu watoto kusaidia katika ujenzi wa vyoo na kuwafundisha kuhusu magonjwa yatokanayo na huduma duni ya vyoo, huchangia kuwajengea tabia njema za afya.
Kuwasaidia watoto wadogo kubaki wasafi
Kinyesi cha aina yoyote kina vijidudu vya magonjwa, na kushika au kugusa kinyesi kunaweza kusababisha magonjwa mabaya kwa watoto na watu wazima. Katika maeneo ya vijijini, wazazi wanaweza kuwasaidia watoto wadogo kujisaidia kwa usalama kwa kuchimba shimo karibu na nyumba na kumwaga viganja viwili vya udongo juu ya kinyesi ndani ya shimo, kila mara mtoto anapomaliza kujisaidia. Ni muhimu pia:
- Kuwasafisha watoto wachanga na wadogo kila baada ya kujisaidia.
- Kunawa mikono yako na sabuni baada ya kuwasafisha watoto wachanga, au kugusa kinyesi.
- Kufukia kinyesi au kutumbukiza chooni.
- Kufua nguo zilizochafuliwa na kinyesi mbali na vyanzo vya maji.
Wafundishe wavulana na wasichana kujifuta au kujitawaza kwa uangalifu, na kunawa mikono yao kila baada ya kutumia choo. Wasichana hasa wanapaswa kufundishwa kujifuta kwa kuanzia mbele kwenda mgongoni.
Kujifuta kuelekea mbele kunaweza kueneza vijidudu kwenye tundu la mkojo na ukeni, na kusababisha maambukizo kwenye kibofu cha mkojo na matatizo mengine ya kiafya.