Hesperian Health Guides
Kuandaa mpango kwa ajili ya vyoo
HealthWiki > Mwongozo wa jamii juu ya afya ya mazingira > Sehemu ya kwanza: Ujenzi wa vyoo na matumizi yake > Kuandaa mpango kwa ajili ya vyoo
Mpango wowote ambao huacha wanawake, kundi lingine au mtu yoyote bila huduma ya choo katika jamii husika hauwezi kuzuia magonjwa katika jamii hiyo. |
Kila mtu na kila jamii wanao utaratibu wa kushughulikia kinyesi cha binadamu, hata kama utaratibu huo ni kujisaidia porini, vichakani au baharini. Hata hivyo, watu wote katika jamii hawatumii njia zinazofanana, na siyo kila mtu hutumia njia hiyo hiyo kila wakati anapotaka kujisaidia. Baadhi ya watu wanaweza kupenda kubadilika na wengine kutopenda. Hata kama ni kujenga aina mpya ya choo, au kuongeza matumizi ya vyoo salama, au mabadiliko mengine yoyote, karibu kila njia ya kushughulikia kinyesi inaweza kuboreshwa.
Hatua ndogo ndogo za mabadiliko ni rahisi kuliko mabadiliko makubwa ya mara moja. Mifano ya mabadiliko madogo ambayo yanaweza kuwa na matokeo makubwa kwa afya, usalama na faraja kwa mtumiaji wa choo ni:
- Kuwepo maji ya kunawa na sabuni karibu ya choo.
- Kuwepo bomba la kutolea harufu, ambalo limefungwa wavu juu yake kunasa na kuzuia nzi kuingia.
- Kujenga sakafu au jukwaa imara juu ya shimo la choo.
Wakati wa kupanga jinsi ya kushughulikia kinyesi katika jamii yako, kumbuka kwamba kila njia inapaswa:
- Kuzuia magonjwa: kuzuia uchafuzi wa chakula, maji na watu kutokana na kinyesi na nzi ambavyo kawaida ni vyanzo vya magonjwa.
- Kulinda huduma na vyanzo vya maji: njia hiyo isichafue maji ya kunywa, maji yaliyopo juu ya ardhi na hata maji yaliyoko chini ya ardhi.
- Kulinda mazingira: vyoo ambavyo hugeuza kinyesi kuwa mbolea husaidia kutunza na kulinda maji, kuzuia uchafuzi na kuurudishia udongo virutubisho.
- Kuwa teknolojia rahisi na yenye gharama nafuu: iwe rahisi kwa watu kusafisha na kutunza vyoo hivyo, na kuvijenga wenyewe kwa kutumia vifaa ambavyo vinapatikana katika maeneo yao.
- Kukubalika kiutamaduni: njia hiyo izingatie mila, desturi na mahitaji ya watu husika.
- Kuwafaa watu wote: izingatie mahitaji ya kiafya ya watoto, wanawake na wanaume, wazee na wenye ulemavu.
Maamuzi juu ya vyoo yanapaswa kuwashirikisha wale watakaovitumia
Maamuzi kuhusu vyoo yakiwashirikisha watu watakaovitumia huchangia uwezekano mkubwa wa kukidhi mahitaji tofauti ya watu kutokana na huduma hiyo, na afya ya kila mtu kuboreka.
Ushiriki wa jamii unaweza kuwa ndiyo kigezo kikubwa zaidi katika kufanikiwa au kushindwa kwa mradi pale serikali, programu au asasi yoyote inapojaribu kuboresha huduma ya vyoo katika jamii.
Kisa mafunzo: Vyoo visivyofaa?
Mwaka 1992, Serikali ya El Salvador, barani Amerika ya Kusini ilitumia zaidi ya dola za Marekani milioni kumi kujenga maelfu ya vyoo. Vyoo hivi vilitarajiwa kugeuza kinyesi cha binadamu kutengezeza mboji, lakini vilihitaji matunzo na usafi zaidi kuliko vyoo vya zamani ambavyo watu walikuwa wamevizoea. Serikali haikushirikisha mtu yoyote kwenye jamii kusaidia ujenzi, na hakuna mafunzo yaliyotolewa juu ya matumizi yake. Hivyo watu hawakujifunza jinsi vinavyofanya kazi.
Baada ya mradi kukamilika, serikali ilifanya uchunguzi kujua jinsi gani vyoo hivyo vilikuwa vikitumiwa. Iligundulika kwamba vyoo vingi vilikuwa havitumiki vizuri na vingine vilikuwa havitumiki kabisa.
Lazima awepo mtu wa kusafisha choo
Hakuna mtu anayependa kusafisha choo. Lakini ni lazima awepo mtu wa kufanya usafi chooni.
Mara nyingi kazi ya kuandaa, kujenga na kufunga vifaa vya vyoo hudhaniwa kuwa kazi ya wanaume au wataalamu. Kazi isiyopendeza na inayohitaji kurudia kila siku, au hata baada ya saa chache, ya kusafisha vyoo mara nyingi inakuwa ya wanawake au watu wengine wanaohisiwa kuwa na hadhi ndogo. Siyo haki kwa kazi zisizopendeza kila mara kuangukia wanawake na watu maskini ambao kawaida hata hawafanyi maamuzi husika.
Kushirikiana katika kufanya kazi ambazo hazipendezi ni njia ya kuhakikisha kazi hizo zinafanyika, ingawa kawaida husababisha migogoro ya kijamii.