Hesperian Health Guides

Tatizo la taka maji yenye kinyesi

Katika sura hii:

Mifumo ya kusafirisha na kuhudumia maji taka yenye kinyesi hutumia maji kusafirisha kinyesi kupitia kwenye mabomba. Mifumo hii inaweza kuboresha afya ya jamii, hasa katika maeneo yenye msongamano wa watu mijini. Lakini ili kuzuia matatizo ya kiafya, maji taka yenye kinyesi yanapaswa kutibiwa ili yaweze kuwa salama, na ikibidi kurudishwa kwenye njia za maji na kutumika tena kwa ajili ya shughuli mbalimbali kama vile kumwagilia bustani.

Usafishaji wa maji taka yenye kinyesi, hata hivyo, ni ghali na mara nyingi maji taka hayo huondolewa na kumwagwa hovyo bila kutibiwa. Hali hii husambaza maji taka yenye kinyesi katika mazingira, vijidudu vya magonjwa, minyoo na kemikali zenye sumu ambazo zinaweza kuwa ndani, na hatimaye kusababisha matatizo ya kiafya kama vile kipindupindu, homa ya matumbo,na homa ya manjano (ugonjwa wa ini).

Pamoja na gharama kubwa inayotumika kusafisha maji taka hayo, njia ya kutumia maji kusafirishia kinyesi mara nyingi siyo endelevu na inaweza kusababisha matatizo mengi yakiwemo:

  • Uchafuzi wa vyanzo vya maji ya kunywa vilivyopo maeneo ya chini ya sehemu maji hayo yanapotibiwa na kuachiwa kurudi kwenye njia za maji juu ya ardhi.
  • Uchafuzi wa ardhi ambayo huitumia kwa ajili ya kilimo na uhai wao.
  • Kupoteza virutubisho muhimu (mbolea) kwa ajili ya kilimo.
  • Uchafuzi wa vyanzo vya maji ya kunywa, kuoga na kilimo.
  • Uchafuzi wa hali ya hewa na harufu mbaya.


Mifumo ya kusafirisha na kuhudumia maji taka yenye kinyesi pia husababisha matatizo ya kiafya pale ambapo aina tofauti za taka zinapochanganywa, kama vile viwanda kutupa kemikali zenye sumu kwenye mfereji wa maji taka. Uchafuzi huu huufanya usafishaji na matumizi tena ya maji taka yenye kinyesi kuwa mgumu sana.

In a village, a man carries water near a polluted stream.
Watu wanaoathirika zaidi na kuzagaa kwa maji taka yenye kinyesi ni wale waishio katika maeneo ambapo maji taka hayo humwagwa au kutiririshwa hovyo.

Njia salama na yenye gharama nafuu zaidi ya usimamizi wa maji taka yenye kinyesi ni kuyatibu palepale yanapozalishwa, na baada ya hapo kuruhusu maji hayo kunyonywa na udongo na kustawisha mimea. Njia ya kawaida ya kufanikisha jambo hili ina sehemu kuu mbili:

  • tanki la chini ya ardhi la kukusanya kinyesi na kukiwezesha kuoza taratibu.
  • eneo maalum linaloruhusu mchuruziko kutoka majitaka yaliyotibiwa kuingia au kunyonywa na udongo.


Njia hii, hata hivyo, inahitaji usanifu wa kiuhandisi.

Mifumo ya maji taka yenye kinyesi hutumia maji mengi, kazi ambayo hata hivyo ingeweza kawaida kufanyika kwa kutumia maji kidogo au bila maji kabisa. Jamii zenye uhaba wa maji, au zile ambazo haziwezi kumudu gharama ya mifumo hii, zinaweza kutumia aina nyingine ya vyoo.


Ukurasa huu ulihuishwa: 04 Juni 2022