Hesperian Health Guides
Wanaume na wanawake wana mahitaji tofauti
HealthWiki > Mwongozo wa jamii juu ya afya ya mazingira > Sehemu ya kwanza: Ujenzi wa vyoo na matumizi yake > Wanaume na wanawake wana mahitaji tofauti
Yaliyomo
Kupanga ujenzi wa vyoo ambavyo vinazingatia mahitaji ya wanawake
Kutowashirikisha wanawake katika maandalizi ya mipango ya vyoo huwaweka katika hatari kubwa ya matatizo ya kiafya, kwa sababu kuna uwezekano mkubwa wa mahitaji yao kutozingatiwa. Wanaume wanapaswa pia kukumbuka mahitaji ya wanawake pale mabadiliko yanapofanyika katika huduma ya vyoo katika jamii ili mabadiliko hayo yawe na manufaa ya kiafya kwa kila mtu.
Ili kurahisisha ushiriki wa wanawake katika maandalizi ya mipango ya vyoo kwa jamii bila kuwaongezea mzigo zaidi:
- Andaa mikutano katika muda ambao utawawezesha wanawake kushiriki.
- Hakikisha wanawake wamealikwa na wanajisikia huru kutoa maoni yao.
- Andaa mikutano maalum kwa ajili ya wanawake pekee iwapo hii itawawezesha kuwa huru zaidi.
- Kila mtu achangie katika kufanya maamuzi.
Kawaida wanawake huwafundisha na kuwalea watoto. Pale ambapo mahitaji ya wanawake hayakutimizwa, mahitaji ya watoto pia yanaweza kutotimizwa. Hivyo, wanawake wasiposhirikishwa katika maandalizi ya mipango ya vyoo nyumbani na katika jamii, jamii nzima huathirika.
Kuondoa vizuizi kwa wanawake kunufaika na huduma ya vyoo bora
Lengo la zoezi hili ni kuwezesha kikundi kuamua mababiliko ambayo yanaweza kuwa yanahitajika ili kuboresha afya kwa kila mtu.
Zoezi hili husaidia watu kujadili maswala mbalimbali ambayo yanaweza kuwazuia wanawake kutumia vyoo bora na salama. Baada ya zoezi hili kufanywa na wanawake pekee, zoezi linaweza kufanywa tena na wanawake na wanaume kwa pamoja.
Muda: saa 1.00 hadi 1.30.
Vifaa: Karatasi kubwa za kuchorea, kalamu na gundi ya karatasi.
- Andika kauli kadhaa juu ya vyoo kwenye karatasi kubwa. Halafu soma kila kauli kwa wanakikundi, na kuuliza kila mtu iwapo anakubaliana na kauli hiyo au la. (Waambie wanakikundi kunyosha juu mkono iwapo wanakubali au kutonyoosha iwapo hawakubali). Kwa kila jibu la ndiyo, weka alama pembeni ya kauli hiyo. Zifuatazo ni baadhi ya kauli ambazo zinaweza kutumika:
- Hesabu alama pembeni ya kila kauli. Chagua matatizo ambayo yalitajwa sana na anzisha mjadala juu ya masuala hayo. Nini chanzo cha tatizo hilo? Ugonjwa gani unaweza kutokana na tatizo hilo? Nini kinaweza kufanyika kuboresha hali hiyo? Kuna vikwazo gani katika kuboresha hali hiyo?
- Hitimisha kwa kuwezesha kikundi kuamua hatua kadhaa ambazo zinaweza kuchukuliwa na wanawake pamoja na wanaume kuhakikisha kwamba mahitaji ya kila mtu yanatimizwa.
Kufanya vyoo viwe rahisi kutumika
TKuna njia nyingi za kufanya vyoo viwe rahisi kutumika kwa watoto, watu wazima, na wenye ulemavu. Vyoo vinatakiwa kurekebishwa kutegemea na hali zao. Hivyo ni muhimu kuhusisha makundi hayo katika kupanga huduma ya vyoo. Ubunifu unahitajika ili kutafuta njia zinazokidhi mahitaji ya kila mtu.
Kama mtu ana matatizo ya kuchuchumaa, basi itengenezwe sehemu ya kushika kwa mkono, au kiti kilichoinuliwa ili aweze kukaa.
Au, iwapo choo kimefungwa sakafuni, tengeneza tundu kwenye kalio la kiti au meza ndogo (stuli) na kuiweka juu ya choo.
Iwapo mtu atakuwa na matatizo ya kudhibiti mwili wake, tengeneza sehemu ya kuegemeza mgongo wake, mbavu na miguu na mkanda wa kiti au chuma cha kuzuia asianguke.
Tumia kamba au jenga uwa au ukingo kuongoza watu wenye upofu kutoka kwenye nyumba hadi chooni.
Kama mtu ana matatizo ya kuvaa nguo, rekebisha nguo zake ziwe pana au mtafutie nguo zenye asili ya kuvutika. Tengeneza sehemu safi na kavu kwa ajili ya kulala chini na kuvaa. Kama mtu ana matatizo ya kukaa, anaweza kutengenezewa papi za ngazi za kujishikizia.
Kumbuka mtu mwenye ulemavu ana mahitaji sawa ya huduma ya choo, pamoja na faragha, kama watu wengine.
Choo kilichorekebishwa kwa ajili ya kiti cha magurudumu