Hesperian Health Guides

Watu wanahitaji nini kutokana na vyoo?

Katika sura hii:

Mara nyingi, afya siyo hitaji kuu pekee la watu katika juhudi zao za kujenga vyoo bora. Watu vilevile wanataka:

  • Faragha: Choo kinaweza kuwa ni shimo refu tu la kawaida bila kibanda juu yake. Lakini kutokana na hitaji la faragha, ni muhimu choo kuwa na uzio au ukuta, paa na mlango kumstiri mtumiaji. Uzio au ukuta na paa bora vinaweza kuwa ni vya kawaida, ambavyo vinatokana na rasilimali zilizomo ndani ya jamii husika.
  • Usalama: Ili choo kiwe salama, lazima kijengwe vizuri na mahali salama. Kama choo kimejengwa vibaya, kinaweza kuwa hatari kukitumia. Na iwapo choo kiko mbali na nyumba, au sehemu iliyojitenga, inaweza kuwa hatari kwa wanawake kukitumia kutokana na uwezekano wa kubakwa.
  • Ubora: Watu kawaida watapendelea zaidi kutumia choo ambacho kina sehemu nzuri ya kukaa au kuchuchumaa, na nafasi inayoruhusu mtu kusimama kwa faragha. Watu pia wanaweza kupendelea kutumia choo ambacho kiko karibu na nyumba, kikiwa na kuta na paa zuri la kuzuia upepo, mvua, jua, au baridi.
  • Usafi: Kama choo ni kichafu na kinatoa harufu mbaya, hakuna atakayependa kukitumia. Kawaida kazi ya usafi wa choo huachiwa watu wa hali ya chini katika jamii. Hii haifai; watumiaji wakishiriki katika kufanya usafi wa choo husaidia kuhakikisha matumizi sahihi na utunzaji wa choo.
  • Heshima: Choo kisafi ambacho kinatunzwa vizuri humwongezea heshima mmiliki wake. Hii inaweza kuwa sababu muhimu ya watu kutumia fedha na juhudi zao zingine kujenga vyoo bora.
illustration of the below: A woman leads a child to a sheltered pit toilet; a man pours water for a child washing his hands; a woman pushes a wheelbarrow; a mop and bucket; a cooking pot and covered container.
MAZINGIRA SAFI KUHUSIANA NA CHOO
=
+
+
+
+
Mahali salama pa kujisaidia (haja ndogo na haja kubwa).
Njia ya kujisafisha baada ya kujisaidia.
Kubadilisha kinyesi na mkojo kuwa rasilimali salama.
Kuhakikisha kuwa usafi na usalama wa vyoo unadumishwa wakati wote.
Uhakika wa chakula na maji kutochafuliwa na mkojo au kinyesi.



Ukurasa huu ulihuishwa: 04 Juni 2022