Hesperian Health Guides
Vyoo vya kumwaga maji kuondoa kinyesi
HealthWiki > Mwongozo wa jamii juu ya afya ya mazingira > Sehemu ya kwanza: Ujenzi wa vyoo na matumizi yake > Vyoo vya kumwaga maji kuondoa kinyesi
Kizibo cha maji kwa ajili ya kuzuia harufu. |
Kizibo cha maji kwa ajili ya kuzuia harufu ambacho kimejengewa ndani ya sakafu. |
Vyoo vya kumwaga maji kuondoa kinyesi hutumia maji kusukuma kinyesi hadi kwenye shimo.Vyoo vya aina hii hupatikana sana katika maeneo ya mjini na hata vijiji vyenye huduma ya maji inayoridhisha, na mahali ambapo watu hutumia maji kutawazia.
Kwa sababu vyoo vya kumwaga maji kuondoa kinyesi ambavyo vimejengwa vizuri huzuia harufu, vinaweza kujengwa ndani au karibu na nyumba. Vyoo hivi hutumia chombo cha kujisaidia kilichotengenezwa kwa plastiki, udongo mgumu, au saruji chenye umbo la bakuli kubwa (kwa ajili ya kukaa), au chenye umbo la sahani ambacho kimesimikwa katika sakafu ya saruji (kwa ajili ya kuchuchumaa).
Choo hiki kawaida huwa na kizibo cha maji ambacho huzuia harufu na wadudu kuzaliana katika mashimo hayo yenye unyevunyevu. Sakafu ya saruji imejengwa moja kwa moja juu ya shimo. Au inaweza kuunganishwa na bomba kwenye shimo 1 au mashimo 2.
Jinsi ya kutumia choo cha kumwaga maji kuondoa kinyesi
Kama kuna shimo moja, shimo hilo hutumika hadi litakapojaa, na baada ya hapo taka hizo zinapaswa kutolewa kabla halijaanza kutumika tena. Mahali penye mashimo 2, kuna boksi la maunganiko ya njia panda, ambalo lina mfumo wa kuelekeza taka kwenye shimo ambalo linatumika kwa wakati huo. Shimo la kwanza hutumika hadi litakapokaribia kujaa. Halafu taka huelekezwa kwenye shimo la pili.
Mambo muhimu ya kuzingatia katika kujenga choo cha kumwaga maji kuondoa kinyesi chenye mashimo mawili
Kwa kutegemea hali ya udongo na tabaka maji, choo cha aina hii kamwe kisijengwe ndani ya mita 3 kutoka kwenye visima. Katika hali ya udongo wenye majimaji, choo cha aina hii kijengwe angalau mita 20 kutoka kwenye visima.
Utunzaji
Lazima maji yamwagwe ndani ya choo kila baada ya kujisaidia. Kumwaga maji kidogo kabla ya kujisaidia pia husaidia kutunza usafi wa choo. Safisha choo kila siku au kila inapohitajika. Katika kusafisha choo cha kuchuchumaa, tumia sabuni au dawa za kawaida za kutakasa na brashi yenye mkono mrefu.
Choo kinaweza kufurika iwapo:
- Kizibo cha maji kimeziba. Hili likitokea, choo hakitafanya kazi.
- Tabaka maji ipo juu sana - ndani ya mita 3. Kama hii ni kweli, kuna hatari ya uchafuzi wa maji yaliyo chini ya ardhi.