Hesperian Health Guides

Magonjwa yanayoambukizwa kupitia kinyesi

Katika sura hii:

Utupaji hovyo kinyesi, kujisaidia vichakani, maeneo ya wazi au hata kwenye maji ni miongoni mwa njia kuu za uchafuzi wa mazingira. Kawaida kinyesi cha binadamu huwa na vijidudu vinavyoweza kusababisha magonjwa. Magonjwa haya yanaweza kuenea taratibu au kuibuka kama mlipuko na kusababisha vifo na madhara mengi ya kiafya, kijamii na kiuchumi.

Namna kinyesi kinavyoweza kuingia katika mwili wa binadamu kupitia mdomo

Sw EHB Ch7 page 140-1.png

Baadhi ya magonjwa, hususan kipindupindu, husababishwa na ‘kula kinyesi’. Je, ni mzaha au ukweli kwamba mtu anaweza kula kinyesi? Mtu anaweza kula kinyesi bila kukusudia. Pia anaweza kulishwa kinyesi kutokana na tabia zake na za wengine zisizozingatia kanuni za afya na usafi.

Mtu anaweza kula chakula kilichochafuliwa na kinyesi wakati wa utayarishaji, upakuaji, au kwenye vyombo vya kulia. Wakala wa magonjwa hasa nzi, mende n.k. akitua kwenye kinyesi kawaida hubeba kiasi fulani cha uchafu huo kwenye miguu na mdomo wake. Nzi au mende huyu akitua kwenye chakula mezani au sehemu yeyote ya kulia, anaweza kuacha sehemu ya uchafu huo kwenye chakula hicho. Hata baada ya nzi huyu kufukuzwa, uchafu hubakia kwenye chakula.

Mtayarishaji wa chakula anapokwenda chooni, na baada ya kujisaidia kuendelea kutayarisha chakula hicho bila kunawa mikono yake na sabuni, kuna uwezekano wa kuchafua chakula hicho iwapo aligusa au kushika kinyesi au vifaa vya chooni wakati akijisaidia.

Wanyama wafugwao kama vile mbwa na paka pia wanaweza kuchafua chakula na kinyesi. Pia ndege kama vile kuku, bata na kunguru ni wachafuzi wakubwa ambao wanapaswa kudhibitiwa wasikaribie chakula na maji ya kunywa ya wanadamu.

Sw EHB Ch7 page 141-1.png

Maji ya kunywa pia yanaweza kuchafuliwa na kinyesi kinapotupwa karibu au kwenye chanzo cha maji ya kunywa hususan kisima, chemchemi au mto. Pia mchuruzo kutoka chooni unaweza kupenya ardhini na kuingia kwenye chanzo cha maji kilichoko karibu, mathalan mita 10. Vyombo vya kubebea, kuchotea au kunywea maji vinaweza kuchafuliwa na kinyesi na kuingiza uchafu huo kwenye maji. Watoto wadogo pia wana mazoea ya kuingiza mikono au vidole vyao kwenye maji ya kunywa kwa kutojua. Lakini baadhi ya watu wazima pia huonekana wakiingiza mikono au vidole vyao ndani ya glasi au chombo kilichojaa maji ya kunywa.

Tabia za kuingiza vitu mbalimbali mdomoni ambavyo vinaweza kuwa vimechafuliwa na kinyesi pia huchangia watu kula uchafu. Tabia hizo ni pamoja na kulamba au kunyonya vidole, kutafuna kucha, kulamba kalamu, ufunguo nk.


Ukurasa huu ulihuishwa: 04 Juni 2022