Hesperian Health Guides

Kuhifadhi vyanzo vya maji

Katika sura hii:

Kuna aina kuu mbili za akiba ya maji duniani:

  • Maji yaliyo juu ya ardhi, mathalan katika mito, vijito, maziwa, na mabwawa.
  • Maji yaliyoko chini ya ardhi - yaliyojikusanya chini ya ardhi kwenye miamba na ambayo hupatikana kupitia chemchemi na visima.


Kwa vile maji yaliyoko juu ya ardhi mara nyingi huwa siyo salama, hayapaswi kutumika kwa ajili ya kunywa bila kwanza, kutibiwa. Maji yaliyoko chini ya ardhi mara nyingi hayana vijidudu vinavyosababisha magonjwa kwa sababu hujichuja yanapopita kwenye tabaka la mchanga na udongo. Hata hivyo, maji chini ya ardhi yanaweza kuchafuliwa na madini yaliyoko kwenye udongo kama vile floridi au aseniki, bomba za maji machafu kutoka vyooni ambazo zinavuja, mashimo ya vyoo au tenki za kuhifadhi vinyesi, dampo za taka, au hata kemikali zenye sumu kutoka viwandani na mashambani.

4 women and a child fill water vessels at a pump.

Pale ardhi na hifadhi za maji zisipotunzwa vizuri, kiasi cha maji chini ya ardhi kinaweza kupungua sana, na hata kuhatarisha uhai wa binadamu. Mahali ambapo miti na uoto wote juu ya ardhi umefyekwa, maji ya mvua ambayo yanapaswa kuingia ardhini na kuhifadhiwa yanaweza kutiririka na kuishia kwenye mito na bahari.

Mikakati muhimu ya kulinda maji yaliyo chini ya ardhi na juu ya ardhi ni pamoja na:

  • Kuzingatia kilimo endelevu.
  • Kujenga na kutumia vyoo salama.
  • Kuhifadhi maeneo yanayokusanya maji, kama vile maeneo-oevu, mabwawa na misitu.


Kadri watu wanavyozidi kuweka makazi yao karibu na vyanzo vya maji na matumizi ya vyanzo hivyo kuongezeka, kazi ya kuhifadhi vyanzo hivyo pia inazidi kuwa ngumu. Katika sehemu zenye viwanda, maji yanaweza kutumika kupita kiasi na kuchafuliwa. Lakini watu wa kawaida ambao ndiyo wahitaji zaidi wanaweza kukosa uwezo wa kuzuia tatizo hilo. Matatizo kama haya yanahitaji jamii nzima kujipanga na kuishinikiza serikali kuweka na kusimamia sheria na kanuni zinazofaa kuhusiana na viwanda na vyanzo vingine vya uchafuzi.



Ukurasa huu ulihuishwa: 04 Juni 2022