Hesperian Health Guides

Uchafuzi wa maji kutokana na sumu

Katika sura hii:

Shughuli za kilimo, uchimbaji madini, uchimbaji mafuta na viwanda vingi zimethibitika kutupa taka za kemikali zenye sumu kwenye vyanzo vya maji. Jambo hili hatari huathiri usalama wa maji, kiasi cha kutofaa kunywa, kupikia, kuoga au kumwagilia mashamba. Katika baadhi ya sehemu, usalama wa maji unaweza kuathiriwa na madini ya asili kwenye udongo yenye sumu, kama vile aseniki na floridi, ambayo husababisha mabaka ya kahawia kwenye meno na udhaifu wa meno kwa ujumla. Akiba ya maji chini ya ardhi inapozidi kutumika, hatari ya sumu za asili pia huongezeka kwa sababu ya ukali wa kemikali hizo za asili kwenye maji yanayobakia.

Hata kama kemikali zenye sumu zitakuwa zinatoka viwandani au kwenye ardhi yenyewe, kemikali hizo kawaida hazionekani kwa macho na ni vigumu kuzigundua. Hivyo, maji yanapaswa kupimwa kwenye maabara kuchunguza uwezekano wa kuwepo sumu za madini ya asili na sumu kutokana na kemikali za viwandani.

Kemikali zenye sumu huingiaje kwenye maji?

In a landscape where a stream flows through fields near a factory, people fish and get water as a man sprays pesticide.

EHB Ch5 Page 59-2.png

Angalia na kutafakari mchoro huu.

  • Ni njia gani umeona ambazo zinaingiza kemikali zenye sumu majini?
  • Nini kinaweza kufanyika ili kulinda maji dhidi ya uchafuzi kutokana na kemikali zenye sumu?
  • Je kunywa maji hayo au kula samaki kutoka maji hayo kunaweza kuathiri afya za watu kwa njia zipi?

Kuzuia uchafuzi kutokana na sumu

Njia pekee ya kulinda maji yasichafuliwe na kemikali zenye sumu ni kuzuia uchafuzi kwenye vyanzo vya maji. Iwapo unadhani maji yenu yamechafuliwa, mnaweza kuihamasisha jamii yenu kuchunguza vyanzo vya maji na kutafuta matatizo yanayochangia uchafuzi na hatimaye kuchukua hatua kukomesha uchafuzi huo. Lakini njia ya kujua kwa uhakika ni kemikali gani zipo kwenye maji ni kipimo cha maabara.

MUHIMU! Kumbuka kwamba kutibu maji dhidi ya vijidudu vya magonjwa na minyoo hakuondoi hatari zinazotokana na kemikali. Na kuyalinda maji dhidi ya kemikali hakutayafanya salama kutokana na vijidudu vya magonjwa pamoja na minyoo.

Ili kuzuia uchafuzi kutokana na kemikali za sumu:

  • Barabara na madaraja vinaweza kujengwa pasipo kuelekeza mifereji yake ya uchafu kwenye mito au njia za maji.
  • Kupanda miti pembeni mwa barabara pia husaidia kuzuia uchafuzi wa vyanzo vya maji kwa sababu miti hunyonya baadhi ya uchafu kutoka hewani.
  • Viwanda ni lazima vipunguze uchafuzi. Viwanda vinaweza kusafisha na kutibu taka zake, na biashara zingine - ndogo na kubwa kutumia mbinu safi za uzalishaji.
  • Uchimbaji madini na mafuta haupaswi kufanyika mahali ambapo utahatarisha ubora na usalama wa maji.
  • Wakulima wanatakiwa kupunguza au kuacha kabisa kutumia viuatilifu na mbolea za kemikali zenye sumu, na kuhakikisha kemikali haziingii kwenye vyanzo vya maji. Wanaweza kutumia njia za asili za kuzuia wadudu na mboji badala ya kemikali zenye sumu.
  • Serikali zinaweza kutunga na kusimamia sheria za kuzuia uchafuzi wa maji.


Kazi ya kudhibiti uchafuzi wa maji kutokana na kemikali zenye sumu inahitaji jamii, serikali na viwanda kuchukuwa hatua za muda mfupi na muda mrefu.

A village sits across a river from a factory spewing dark smoke.
Madini yenye sumu ya Aseniki kwenye maji “salama

Kwa karne nyingi, watu wengi nchini Bangladesh walikunywa maji kutoka kwenye visima vilivyotunzwa kwa uangalifu sana. Lakini kwa ajili ya kuoga, kuosha vyombo na kufua nguo walitumia mito, mifereji na vyanzo vingine vya maji visivyotunzwa vema. Maji haya mara nyingi yalikuwa yamechafuliwa na vijidudu vya magonjwa, ambavyo vilisababisha kuhara, kipindupindu, hepatitis na matatizo mengine ya kiafya. Hivyo ilibidi serikali kufanya kazi pamoja na mashirika ya kimataifa kujenga visima nchini kote. Kampeni za afya kwa umaa pia zilifanyika kuhamasisha watu kutumia maji “salama” ya visima badala ya maji yaliyo wazi juu ya ardhi.


Lakini idadi kubwa ya matukio ya uchafuzi wa maji kwa njia ya sumu yaliripotiwa, kuanzia mwaka 1983. Watu wengi waliumwa sana magonjwa ya ngozi, kansa uharibifu wa neva, magonjwa ya moyo na kisukari. Watu wengi walifariki. Hakuna mtu aliyejua kilichokuwa kinasababisha magonjwa haya. Mwaka 1993, wanasayansi walikubaliana kwamba magonjwa hayo yalikuwa yanasababishwa na sumu kutokana na madini ya Aseniki kwenye maji. Hakuna mtu aliyekuwa amewahi kupima maji yanayotoka ndani ya ardhi kuhusiana na kemikali hiyo ya Aseniki. Hata hivyo, karibu nusu ya visima vyote walipochota maji vilikuwa na kiwango kikubwa cha Aseniki.


Je, sumu ya Aseniki hiyo iliingiaje kwenye maji? Kwa asili yake maji hayo chini ya ardhi yalikuwa na Aseniki ndani yake. Lakini kiwango cha sumu hiyo kiliongezeka na kusababisha waugue.


Teknolojia ileile iliyowezesha kuvuta maji “salama” kutoka ardhini maeneo ya vijijini pia iliwezesha umwagiliaji wa maeneo makubwa, na kuchangia ukuaji wa kilimo cha kibiashara. Utaratibu wa kuvuta maji mengi kutoka ardhini kwa ajili ya kumwagilia mashamba makubwa ulisababisha sumu ya Aseniki kukolea katika maji yaliyobaki chini ya ardhi kwa ajili ya kunywa. Pia matumizi ya mbolea za viwandani (ambazo mara nyingi hujumuisha kemikali ya Aseniki) yaliongezeka, pamoja na viuatilifu vilivyotumika mashambani. Hali ya uchafuzi wa maji kwa sumu nchini Bangladesh pia ilizidi kuwa mbaya zaidi kutokana na utupaji wa taka za sumu kutoka kwenye viwanda vya kusindika ngozi na viwanda vingine kwenye njia za maji ulivyoongezeka.


Karibu watu 40,000 nchini Bangladesh, wanaumwa kutokana na uchafuzi unaosababishwa na Aseniki, wengi wao wakiwa wanawake, watu maskini na wafanyakazi wa ndani. Matatizo ya kiafya yanayohusiana na Aseniki huchukua miaka mingi kuanza kujitokeza. Hivyo watu wengi zaidi wataugua.

Janga hili baya liliendelea kwa muda mrefu, na kubaki bila kufanyiwa utafiti wala ufumbuzi, kwa sababu waliokuwa wakiathirika ni miongoni mwa watu maskini sana duniani. Ingekuwa maji katika mji mkuu wa Dhaka ndiyo yalikuwa yamechafuliwa, au ugonjwa huu kutokea katika nchi tajiri, hatua zingechukuliwa haraka zaidi.


Hali ya sumu katika maji nchini Bangladesh inaonesha hatari za uchafuzi wa maji - maji yaliyo juu ya ardhi na maji yaliyo chini ya ardhi. Pia inadhihirisha umuhimu wa kupima vyanzo vya maji na kuchukua hatua haraka iwapo kuna mashaka yoyote kuhusu usalama wa maji hayo.

Kuondoa sumu ya Aseniki kwenye maji ya kunywa

Chujio rahisi limegunduliwa nchini Bangladesh ambalo hutumia misumari kuondoa sumu ya Aseniki kwenye maji. Njia hii inaweza kusaidia kupunguza matukio ya madhara, lakini siyo ufumbuzi kamili kwa tatizo la maji ambayo yamechafuliwa na sumu hiyo.Ukurasa huu ulihuishwa: 04 Juni 2022