Hesperian Health Guides
Mikakati ya kuzuia ueneaji wa vijidudu vya magonjwa na minyoo
HealthWiki > Mwongozo wa jamii juu ya afya ya mazingira > Sehemu ya tatu: Matatizo ya kiafya kutokana na maji yasiyo salama > Mikakati ya kuzuia ueneaji wa vijidudu vya magonjwa na minyoo
Yaliyomo
Katika sura hii:
Wakati vijidudu vya magonjwa na minyoo hupatikana kila mahali, kuna hatua rahisi ambazo kila mtu anaweza kuchukua katika kudhibiti magonjwa husika. Ili kuzuia kuenea kwa vijidudu vya magonjwa na minyoo:
- Linda vyanzo vya maji na tumia maji safi kwa ajili ya kunywa na kufanyia usafi-kuoga, kuosha vyombo na kufulia. Ni bora kutibu maji kabla ya kuyatumia – isipokuwa tu kama una uhakika kwamba ni salama.
- Daima nawa mikono baada ya kutumia choo, na kabla ya kushika chakula. Tumia maji safi na sabuni. Kama sabuni haipatikani, tumia mchanga safi au majivu. Kata na kutunza usafi wa kucha za mikono yako. Hili pia huchangia usafi wa mikono.
- Tumia choo. Matumizi sahihi ya choo husaidia kuweka vijidudu vya magonjwa na minyoo mbali na watu. Iwapo hakuna choo ni bora kujisaidia mbali na vyanzo vya maji, mahali ambapo vinyesi havitaguswa na watu au wanyama. Fukia vinyesi vyote kwa udongo au mchanga ili kuzuia nzi.away.
- Tumia njia safi na salama katika kuandaa na kutunza chakula. Osha matunda na mboga, au vipikwe vizuri kabla ya kuliwa. Mabaki ya vyakula yapewe wanyama, au yatumike kutengenezea mboji. Ondoa vyakula vilivyoharibika, tunza nyama na samaki tofauti na vyakula vingine na kuhakikisha nyama, mayai, na samaki vinapikwa na kuiva vizuri kabla ya kuliwa. Safisha vyombo, na vifaa vya kukatia kwa maji ya moto na sabuni baada ya kuvitumia, na vikaushwe vizuri juani kama inawezekana.
- Weka wanyama mbali na chakula cha familia na vyanzo vya maji ya jamii.
- Vaa viatu kuzuia minyoo kukuingia mwilini kupitia miguuni.
- Angamiza nzi na kufunika chakula kuzuia nzi wasieneze vijidudu vya magonjwa. Vyoo vyenye uwezo wa kudhibiti nzi au kuwazuia kuzaliana, na kupunguza mazalia ya nzi pia vinaweza kusaidia.
Jinsi ya kutengeneza mtego wa nzi kwa kutumia chupa ya plastiki

- Kata na kuondoa sehemu ya juu ya chupa ya plastiki.
- Funga waya au uzi kwenye chupa hiyo kwa ajili ya kuning’inizia..
- Weka chambo - vitu vitamu kama vile sukari, au matunda ndani ya chupa.
- Geuza sehemu ya juu ya chupa uliyokata na kuingiza kwenye sehemu ya chupa yenye chambo. Nzi wataingia ndani lakini hawataweza kutoka nje.
- Chupa itakapojaa, mwaga nzi chooni au kwenye sehemu ya kukusanya taka kwa ajili ya kutengenezea mboji. Hakikisha nzi wote wamekufa kabla ya kumwagwa kutoka kwenye mtego.
Ili kupunguza nzi, ning’iniza mtego huu karibu na choo na sehemu za maandalizi ya chakula.
Kunawa mikono

Njia kuu mojawapo ya kudhibiti matatizo ya kiafya kutokana na vijidudu vya magonjwa na minyoo ni kunawa mikono kwa maji safi na sabuni baada ya kujisaidia chooni, kumtawaza mtoto, kabla ya kuandaa au kugusa chakula, kumlisha mtoto, au kula.
Hakikisha kuna chanzo cha maji safi nyumbani ili kurahisisha unawaji mikono. Lakini kunawa mikono kwa maji pekee hakutoshi. Tumia sabuni kuondoa uchafu na vijidudu vya magonjwa. Iwapo hakuna sabuni, tumia mchanga au majivu.
Paka mikono yako sabuni na tumia mikono miwili kusuguana chini ya maji yanayotiririka kutoka bombani, koki au chombo chochote maalum kwa ajili ya kunawa mikono.

Paka sabuni ya povu, mchanga au majivu na kuruhusu kusuguana angalau kwa sekunde 30. Baada ya hapo, suuza na kukausha mikono yako kwa kitambaa kikavu, au acha ikauke kwa hewa ya kawaida.
Tippy tap: Kifaa rahisi kwa ajili ya kunawa mikono
Koki hii hukuwezesha kunawa mikono yako kwa kutumia maji kidogo sana. Pia humwezesha mtumiaji kusugua mikono yake chini ya maji yanayotiririka. Koki hii inaweza kutengenezwa kwa vifaa ambavyo hupatikana kwa urahisi. Kifaa hiki pia kinaweza kuwekwa mahali popote watu wanapohitaji kunawa mikono yao, kwa mfano, karibu na jiko, karibu na choo au sokoni.
Namna ya kutengeneza koki ya kunawia mikono kwa kutumia chupa ya plastiki
Ili kutengeneza koki hii utahitaji: chupa ya plastiki yenye kifuniko kinachoweza kushika vizuri. Pili utahitaji mrija au kitu kingine chochote chenye tundu ndani la kupitisha maji, mathalan mrija wa kalamu ya wino.


- Safisha chupa ya plastiki.
- Kwa kutumia waya wa moto, toboa tundu dogo katika sehemu ya chini ya chupa hiyo.
- Kama huna mrija wa kunywea, safisha mrija wa ndani wa kalamu ya kawaida ya wino. Kata mrija huo na kuuchomeka kwenye tundu ulilotoboa kwenye chupa hiyo. Mrija huo lazima ubane vizuri.
|
|