Hesperian Health Guides

Haki ya kupata maji salama ya kutosha

Katika sura hii:

Ulimwenguni kote, watu wanajitahidi kulinda haki yao ya afya bora, ikiwemo haki ya kuwa na chanzo cha maji salama na yakutosha. Makampuni ya ugavi wa maji ya binafsi yameanza kutoa huduma ya maji kibiashara katika sehemu mbalimbali. Lakini pale kampuni binafsi zinapochukua mamlaka yote ya huduma za maji (ubinafsishaji wa maji), bei mara nyingi hupanda, na kuwalazimisha watu kutumia maji kidogo sana kuliko mahitaji yao ya msingi na kwa ajili ya afya njema. Watu wengi, katika hali hiyo, wanakuwa hawana njia mbadala isipokuwa kuchota maji kutoka popote pale wanapoweza kuyapata bure, hata kama maji hayo yana vijidudu vya magonjwa, minyoo au kemikali zenye sumu. Hali hii husababisha matatizo makubwa ya kiafya.

Serikali na jamii hawana budi kufanya kazi pamoja kuboresha na kupanua huduma ya maji safi na salama, hasa kwa wale wanaoyahitaji zaidi.

Ubia huboresha huduma ya maji

A woman with a baby on her back shakes hands with a man near a village pump as other people look on.

Nchini Ghana, Afrika Magharibi, vikundi vya kijamii vimechukua usimamizi wa huduma ya maji katika maeneo yao. Katika mji wa Savelugu, kampuni ya maji inayomilikiwa na serikali husambaza maji kwa njia ya bomba, na wanajamii huwajibika kupanga bei, kusambaza maji na kuifanyia ukarabati miundombinu ya maji. Mfumo huu wa usimamizi wa huduma ya maji ni mfano wa “ubia kati ya jamii na serikali.”


Kwa sababu jamii inawajibika kusimamia huduma ya maji, kuna uhakika zaidi wa maji salama na ya kutosha kwa sababu haya ndiyo matakwa ya wengi. Iwapo baadhi ya watu hawawezi kumudu gharama ya maji, jamii hulipia hadi pale watakapokuwa na uwezo wa kulipia wao wenyewe. Watu hupatiwa mahitaji yao siyo tu kwa sababu wanazo fedha za kulipia, lakini kwa kuwa wao ni sehemu ya jamii. Kampuni ya maji ya Ghana hunufaika na utaratibu huu kwa sababu jamii daima hulipia huduma ya maji wanayopata.


Usimamizi shirikishi wa huduma ya maji wa Savelugu, ni mfano bora wa usimamizi wa huduma ya maji nchini Ghana. Kwa kusimamia mfumo wao wa maji, watu wa Savelugu wameonyesha kwamba ubinafsishaji sio njia pekee ya kutoa huduma ya maji. Tangu ubia kati ya jamii na serikali kuanzishwa, magonjwa yamepungua sana, na kila mmoja anayo maji ya kutosha. Mafanikio yao yanaonyesha kuwa jamii ikipewa nafasi ya kufanya maamuzi na kuwajibika kwa ajili ya masuala yote ya huduma ya maji katika maeneo yao, uhakika wa maji kwa wote huongezeka.

Kutengeneza na kuuza maji

Imani inayozidi kujengeka ni kwamba maji ya bomba siyo safi wala salama. Hivyo, wenye uwezo wananunua maji ya chupa. Iwapo kuna vijidudu vya magonjwa katika maji ya bomba, kunywa maji salama ya chupa kunaweza kuepusha magonjwa. Lakini maji kuuzwa kwenye chupa hakumaanishi kwamba ni salama. Mara nyingi, maji ya chupa ni maji ya kawaida ya bomba, ambayo hata hivyo huuzwa kwa bei ya juu zaidi. Njia bora zaidi ya kusaidia kuinua afya ya watu na mazingira ni kuongeza ubora na uhakika wa ugavi wa maji kwa umma.

Ukifikiria matatizo ya kiafya yanayosababishwa na utengenezaji wa chupa za plastiki ambazo hutumika kuuzia maji, jinsi zinavyojazwa maji, kusafirishwa na kutupwa baada ya kutumika, gharama ya maji ya chupa ni kubwa kuliko kutoa maji salama kwa kila mtu.

A man wearing a tie covered with dollar signs fills a bottle labelled "Mountain Springs Superior Water" from a tap labelled "Municipal Tap Water."

Makampuni huuza maji ya chupa kwa sababu ni biashara yenye faida kubwa. Mara nyingi hutangaza bidhaa zao kwa njia ambazo huwafanya watu kudhani kwamba maji ya bomba sio mazuri kiafya au sio “salama kiasi cha kutosha”. Makampuni makubwa ya kimataifa ambayo huuza maji, na vinywaji vingine vya asili ya Cola, mara nyingi pia huathiri uchumi wa nchi husika kwa kudhoofisha biashara ya vinywaji baridi vya kawaida. Wakati mwingine hutumia maji mengi sana na kuathiri maisha ya watu katika maeneo hayo kwa kusababisha uhaba wa maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, umwagiliaji mazao na matumizi mengine.

Huduma ya usambazaji maji ya bomba - maji safi, salama na ambayo yanakidhi mahitaji ya msingi ya jamii ndiyo njia muhimu zaidi ya kuboresha afya ya kila mtu. Katika bara la Ulaya na Amerika ya Kaskazini, huduma ya maji salama kwa jamii ndiyo msingi mkuu wa afya ya jamii. Katika nchi maskini, watu wanakosa maji salama na kutakiwa kununua maji ya chupa yenye gharama kubwa.

Kuwa na maji safi, salama na ya kutosha kwa ajili ya afya bora ni haki ya kibinadamu. Ni rahisi kulinda na kutimiza haki hii kwa kuboresha mifumo ya ugavi wa maji ambayo inamilikiwa na umma au na jamii husika. Wanajamii wanapaswa kushiriki katika usimamizi wa miradi ya maji. Hii itasaidia kuhakikisha kuwa afya yao inapewa kipaumbele.



Ukurasa huu ulihuishwa: 04 Juni 2022