Hesperian Health Guides

Maji na afya ya jamii

Katika sura hii:

Maji ni zawadi na urithi wetu kutoka kwa Mungu. Na usalama wa maji – uhakika wa kupata maji ya kutosha na ambayo ni safi, ni sehemu muhimu ya afya ya jamii. Iwapo watu watafanya maamuzi ya pamoja kuhusu namna ya kupata, kuhifadhi na kutumia rasilimali zao za maji, wanaweza kuhakikisha usalama wa maji ya jamii.

Watu wengi wako tayari kufanya kazi au kulipa gharama inayostahili ili kupata huduma ya maji salama na ya kutosha. Lakini katika sehemu nyingi, maji ambayo watu wanapata kwa ajili ya kunywa yamechafuliwa na vijidudu, minyoo au kemikali za sumu. Vilevile, kiasi kikubwa cha maji huchukuliwa na viwanda au mashamba makubwa, au huuzwa kwa gharama ambayo watu wa kawaida hawawezi kumudu. Katika maamuzi yote kuhusu huduma ya maji - bei, ulinzi, hifadhi, usambazaji na matumizi, mahitaji ya binadamu ya maji kwa ajili ya maisha na afya zao yanapaswa kupewa kipaumbele kabla ya matumizi mengine.

A man kneels to wash a shirt in a bucket.
Kila mtu anahitaji maji
Kiwanda chachukua maji ya jamii

Coca-Cola bottle

Plachimada ni kijiji kidogo kusini mwa India mahali ambapo wakulima hulima mpunga na minazi. Zamani, wakulima walikuwa wakiishi maisha mazuri kwa sababu kulikuwa na mvua za kutosha na ardhi nzuri. Lakini miaka michache iliyopita, hali ilianza kubadilika baada ya kampuni moja ya kimataifa kujenga kiwanda cha vinywaji baridi pembeni mwa kijiji hicho.


Kampuni ilichimba visima virefu ili kupata maji kutoka ardhini kwa ajili ya kutengenezea vinywaji hivyo. Kila siku kiwanda kilitumia lita milioni moja na nusu za maji. Miaka 2 baada ya kiwanda kufunguliwa, mazao ya wanakijiji yalianza kukauka pamoja na visima vyao. Walipotumia maji hayo kupikia wali, ulibadilika kuwa na rangi ya kahawia na wenye ladha mbaya. Walipokunywa au kuoga maji haya, waliota upele kwenye ngozi, nywele kung’oka, kusikia maumivu katika viungo, udhaifu wa mifupa na matatizo ya neva. Waligundua kwamba kampuni ilikuwa imechafua maji yao yaliyo chini ya ardhi kwa kemikali za sumu. Ili kulinda afya yao, wanakijiji walianza kuchota maji kutoka mbali na kaya zao.


Mwaka mmoja, mvua hazikunyesha kabisa. Lakini kampuni hiyo iliendelea kuchukua maji wakati wa ukame. Wanakijiji walitazama tu malori yalipokuwa yakitoka kiwandani kila siku kuchukua rasilimali hii muhimu, ambayo wakati fulani iliwahakikishia uhai wao na mazao yao. Hata vyanzo vya maji vilivyopo mbali na kijiji chao vilikauka. Baada ya kuona watu wengi wakizidi kuugua, walikutana pamoja kuzungumzia namna wanavyoweza kuzuia kampuni hiyo ya kimataifa kuchukua maji yao.


Baada ya mkutano, zaidi ya watu 2000 walifanya maandamano ya amani hadi kwenye kiwanda cha kampuni hiyo na kuitaka kampuni kuondoka na kuwalipa wanakijiji fidia kwa ajili ya maji yao. Kampuni iliitika kwa kutoa lori lenye tenki kupeleka maji kwa wanakijiji kila siku. Lakini tenki moja la maji halikutosheleza mahitaji ya wanakijiji. Baada ya siku 50 za maandamano, polisi walikamata watu 130. Miezi kadhaa baadaye, watu 1000 waliandamana tena hadi kwenye kiwanda na polisi wakawakamata wengi wao.


Mapambano haya yalisababisha ugumu wa maisha kwa watu wa Plachimada, lakini pia yaliwaunganisha ili kudai haki yao ya kupata maji salama. Baada ya miaka kadhaa, serikali ya mtaa ilianza kuwaunga mkono wananchi hao na kuamuru kampuni kuacha kutumia maji ya aridhini nyakati za ukame. Lakini serikali kuu ilisisitiza kuwa kampuni iruhusiwe kuendelea kutumia maji ya aridhini. Mgogoro huo ulipelekwa mahakamani na hatimaye watu wa Plachimada walishinda na kiwanda cha vinywaji baridi kufungwa.


Watu wa Plachimada walipokuwa wakipigania haki yao ya kupata maji, kampeni yao ilivuta hisia za watu kote nchini India na hata duniani. Mapambano yao yaliwatia moyo wengine wengi. Katika dunia ambamo mamilioni ya watu hawana maji salama ya kutosha kwa ajili ya kunywa, hakuna mantiki ya kutumia rasilimali hii muhimu yenye ukomo kuzalisha vinywaji baridi vya anasa. Zaidi ya hapo matumizi ya maji na kiwanda hicho yalikuwa yakisababisha watu kuugua.



Ukurasa huu ulihuishwa: 04 Juni 2022