Hesperian Health Guides
Hifadhi chemchemi yenu
HealthWiki > Mwongozo wa jamii juu ya afya ya mazingira > Sehemu ya pili: Utunzaji wa huduma ya maji ya jamii > Hifadhi chemchemi yenu
- Je, hiki ni chanzo halisi, au kuna kijito au maji mengine kutoka juu ya ardhi ambayo yanaingia ndani ya ardhi na kupita juu ya chemchemi? Kama ni hivyo, kile kinachoonekana kuwa ni chemchemi kinaweza kuwa maji ya juu ya ardhi ambayo yanatiririka umbali mfupi yakiwa chini ya ardhi. Katika hali kama hii, maji hayo yanaweza kuwa yamechafuliwa, au kupatikana msimu wa mvua tu.
- Je, ipo mianya mikubwa katika mwamba juu ya chemchemi? Kama ndivyo ilivyo, chunguza maji yaliyopo kwenye chemchemi baada ya mvua kubwa kunyesha. Iwapo yataonekana kuwa na vumbi au matope, ni rahisi kuchafuliwa na maji yanayotiririka juu ya ardhi.
- Je, kuna uwezekano wa uchafuzi karibu au juu ya chanzo cha chemchemi? Chanzo cha uchafuzi kinaweza kuwa malisho ya mifugo, vyoo vya shimo, karo za maji machafu, matumizi ya viuatilifu na mbolea za viwandani, au shughuli nyingine za binadamu.
- Je, udongo ni mwepesi au wa kichanga ndani ya mita 15 kutoka chemchemi? Hali hii inaweza kuruhusu maji machafu kutoka juu ya ardhi kuchanganyika na maji safi yaliyoko chini ya ardhi.
Yaliyomo
Linda eneo linalozunguka chemchemi
Gharama ya kulinda chemchemi ni rahisi kuliko kuchimba kisima. Mara baada ya chemchemi kuhifadhiwa, inakuwa rahisi kutandaza bomba kutoka kwenye chemchemi na kusogeza huduma ya maji karibu na watu. Katika kuhifadhi eneo linalozunguka chemchemi, unaweza kuzungusha uzio na kuchimba mfereji kwa ajili ya kuondoa maji yanayotiririka na uchafu. Uzio pia huzuia mifugo kufika kwenye chemchemi.
Panda miti ya asili karibu na chemchemi kwa ulinzi zaidi. Miti itazuia mmomonyoko wa ardhi, na kulifanya eneo hilo kuwa mahali panapopendeza kuchota maji.
Boresha chemchemi kwa kuijengea
Chemchemi inaweza kujengewa ‘chumba’ kidogo na mafundi waashi, kwa kutumia matofali au zege. Chumba hicho husaidia kukusanya maji ya chemchemi na kuyalinda yasichafuliwe. Chumba hiki pia hurahisisha uchotaji maji kutoka chemchemi, au kuelekeza maji hayo kwenye bomba au tenki la kuhifadhia maji ya jumuiya. Ujenzi wa kuboresha chemchemi bora hutegemea hali halisi ya ardhi eneo hilo na vifaa vya ujenzi vilivyopo.
Sehemu za chumba cha chemchemi
Mabomba na chumba cha chemchemi vinahitaji usafi wa mara kwa mara
Chumba cha chemchemi kinahitaji uangalizi wa karibu ili kuhakikisha chemchemi inaendelea kutoa maji salama. Tope, majani, mizoga ya wanyama na vitu vingine vinaweza kujikusanya katika mabomba na ndani ya chumba, kuziba mabomba au kuchafua maji.
Funga chujio la wavu wa chuma kwenye mdomo wa bomba linaloingia katika chumba cha chemchemi ili kuzuia vitu visivyo salama kuingia. Kusafisha chujio mara kwa mara kutahakikisha maji kutoka vizuri.