Hesperian Health Guides
Maji yaliyokwishatumika: Ni tatizo au rasilimali
HealthWiki > Mwongozo wa jamii juu ya afya ya mazingira > Sehemu ya pili: Utunzaji wa huduma ya maji ya jamii > Maji yaliyokwishatumika: Ni tatizo au rasilimali
Hata hivyo, maji yaliyokwisha kutumika lakini ambayo hayajachafuliwa na kemikali zenye sumu au vinyesi vya binadamu yanaweza kutumika tena baada ya kutibiwa. Njia ya kutibu maji hayo inayofaa zaidi kwa kaya au jamii yako hutegemea na:
- wingi wa maji yaliyotumika ambayo yanapaswa kutibiwa,
- aina ya uchafu kwenye maji,
- yatatumika kwa ajili ya nini, pamoja na
- rasilimali zilizopo - muda, nafasi na nguvu kazi kwa ajili ya kutibu maji hayo.
Maji ya kijivu- maji machafu mchanganyiko ya nyumbani
Maji ya kijivu ni maji ambayo yametumika kwa ajili ya kuoshea vyombo na vifaa vingine vya nyumbani lakini hayajachanganyika na vinyesi vya binadamu. Ili mradi sabuni na dawa zenye sumu hazikutumika kuoshea vyombo na vifaa vingine nyumbani, maji ya kijivu huhitaji tiba rahisi kabla ya kutumika tena kwa ajili ya bustani, au kutokuyatibu kabisa kabla hayajaingia ardhini.
Kuna aina nyingi tofauti za mifumo ya kushughulikia maji ya kijivu. Mfumo wowote kwa ajili ya maji ya kijivu hufanyakazi vizuri zaidi pale:
- Inapokuwa rahisi kuujenga na kuutunza.
- Mafuta mazito ya mitambo, dawa kali za kuoshea vyombo, na kemikali nyingine haviruhusiwi kuchanganyika na maji hayo.
Kutengeneza eneo oevu kuchuja maji ya kijivu
Njia mojawapo ya kusafisha maji haya ni kuiga njia ya asili ya kusafisha maji kwa kutengeneza eneo oevu. Eneo oevu linaweza kusafisha maji ya kijivu kwa kuchuja maji hayo kupitia matabaka ya mimea, udongo na miamba. Virutubisho katika maji hayo husaidia mimea kuota vizuri, na mimea huongeza hewa ya oksijeni kwenye maji na hivyo, kusaidia kuyasafisha. Maeneo oevu yaliyotengenezwa pia:
- Husaidia upatikanaji wa maji kwa ajili ya kumwagilia mazao.
- Huotesha mimea yenye manufaa kwa matumizi mbalimbali-mfano mianzi, mafunjo nk.
- Hubadili madimbwi kuwa bustani nzuri za maua.
Jinsi ya kutengeneza eneo oevu
Unapotaka kujenga eneo oevu, zingatia yafuatayo:
- Unahitaji eneo lenye ukubwa gani na lenye kina gani? Ukubwa na kina cha eneo oevu utategemea kiasi cha maji ya kijivu yanayotarajiwa kuingia. Vilevile uchujaji wa maji ya kijivu utategemea kina cha eneo oevu. Kama maji yataingia na kupita haraka matabaka ya mimea huenda yasifanye uchujaji vizuri.
- Je, chanzo cha maji kiko usawa wa juu kuliko eneo oevu? Maji lazima yatiririke kupita kwenye eneo oevu. Hivyo yanapaswa kutoka kwenye chanzo kilichopo usawa wa juu, la sivyo yatasukumwa kwa pampu.
- Je, maji yatakayosafishwa yataelekea wapi? Je, yanaweza kukusanywa kwenye tenki au kuelekezwa moja kwa moja kwenye bustani?
Maeneo oevu yanaweza kutengenezwa popote pale penye nafasi ya kutosha. Kama kuna nafasi ndogo, yanaweza kujengwa kwenye mabeseni, kwa mfano pipa lenye lita 200. Katika ardhi yenye maji ya kutosha, chimba shimo na kulipiga lipu ya saruji. Katika maeneo yenye, udongo wa mfinyanzi, lipu haihitajiki.
Eneo oevu lililojengwa linaweza kusafisha kiasi kikubwa cha maji ya kijivu
Kila eneo oevu lililojengwa lina mahitaji tofauti kutegemea na kiasi cha maji, aina ya udongo na mimea, na mahitaji mengine. Fanya majaribio kuangalia njia bora zaidi ya kufanikisha eneo oevu lako.
- Kama mimea inakauka au kufa - huenda maji yanayopita kwenye eneo hayatoshi. Vyanzo zaidi vya maji vinaweza kuongezwa, shimo na urefu wake kupunguzwa, au mimea mipya kuoteshwa.
- Kama maji hayatiririki ipasavyo - jaribu mawe makubwa na mchanga kidogo, au teremsha bomba la kutolea maji.