Hesperian Health Guides

Tunza maji kwa usalama

Katika sura hii:

Iwapo usafi na usalama wa maji havitazingatiwa kwa makini wakati wa uchotaji, usafirishaji na hifadhi, ni rahisi maji kuchafuliwa.

Yanapohifadhiwa katika tenki zenye nyufa au vyombo ambavyo havikutengenezwa vizuri au visivyo na mifuniko, maji yanaweza kuchafuliwa kupitia vinyesi vya wanyama na vijidudu vya magonjwa. Lazima awepo mtu au kikundi kazi chenye wajibu wa kufanya matengenezo ya bomba kila zinapoharibika.


Hadithi ya mpelelezi - Je ilikuwaje maji yakachafuliwa?

Zoezi hili linasaidia kuchunguza jinsi maji yanayochotwa kutoka kisimani, chemchemi au bomba yanavyoweza kuchafuliwa kabla ya kutumika. Zoezi hili linaweza kufanywa na watu wanne au zaidi.

Muda: Dak. 30

  1. Mwezeshaji - waeleze washiriki kwamba wao ni wapelelezi wa masuala ya afya halafu wapangie kazi. Kwa mfano, familia 10 huchota maji safi kutoka kwenye kisima kimoja. Baada ya siku chache, watoto wa familia mojawapo wanaanza kuugua ugonjwa unaotokana na kunywa maji yasiyo salama nyumbani. Familia zingine hazipatwi na tatizo hilo. Kazi ya mpelelezi ni kuchunguza jinsi gani maji yalivyochafuliwa baada ya kuchotwa kisimani.
  2. Omba mtu 1 hadi 3 kujitolea. Pembeni na kundi kubwa ili wasisikie, waambie kwamba jukumu lao ni kutoa kiashiria tu wakati kundi litakapokuwa likiuliza maswali kujua jinsi gani maji yalivyochafuliwa. Baadaye, waambie kuamua jinsi gani maji yalivyochafuliwa kabla ya kuungana tena na kundi kubwa.
  3. Kundi kubwa litaanza kuwauliza maswali wale waliojitolea jinsi gani maji yalivyochafuliwa, na wao watajibu kwa kutoa viashiria tu hadi hapo watu watakavyojitokeza kupendekeza kwa usahihi jinsi maji yalivyochafuliwa.
  4. Iwapo kundi ni kubwa, linaweza kugawanywa katika vikundi kadhaa vidogo. Punguza idadi ya maswali-mfano ruhusu kila kundi dogo au mtu kuuliza maswali 4. Kundi au mtu wa kwanza kujibu kwa usahihi ndiyo atakuwa ameshinda. Rudia zoezi hili mara kadhaa kwa kutumia njia mbalimbali. Baadaye, wezesha majadiliano ya pamoja kuchunguza njia zingine ambazo zinaweza kusababisha maji ya kunywa kuchafuliwa nyumbani. Pia jadili nini kifanyike kulinda usafi na usalama wa maji nyumbani na katika jamii nzima.

Usafi wa vyombo vya maji

Maji yaliyohifadhiwa yanaweza kuchafuliwa hasa pale yanapoguswa na watu wenye mikono michafu, kuwekwa kwenye vyombo vichafu, au vumbi na uchafu kuingia kwenye maji, au kutumia vikombe vichafu kuchotea. Ili kuzuia maji yasichafuliwe nyumbani:

EHB Ch6 Page 91-1.png
Vyombo vyenye midomo myembamba ni salama zaidi kuhifadhi maji.
  • Nawa mikono kabla ya kuchota na kubeba maji.
  • Safisha na kufunika vyombo vya kuhifadhia na kubebea maji.
  • Safisha mara kwa mara vyombo vinavyotumika kuhifadhia maji nyumbani.
  • Weka vyombo vya kuhifadhia maji mbali na wanyama, na visiwekwe chini sakafuni.
  • Unapomimina maji usiguse mdomo wa chombo hicho, au tumia kifaa kingine chenye mkono mrefu kuchotea maji.
  • Tunza usafi wa vikombe vyote vya kunywea maji.
  • Kamwe usiweke maji kwenye vyombo vilivyotumika kuhifadhia dawa za kuulia wadudu na kemikali nyingine zenye sumu.
  • Kama inawezekana usitibu maji mengi zaidi ya mahitaji yako ya muda mfupi. Kwa maji ya kunywa na kupikia, mahitaji ya kawaida ya kila mtu ni chini ya lita 5 kwa siku.

Funika tenki na vifaa vya kuhifadhia maji

An urn.

Tenki na vyombo vingine vilivyofunikwa ni salama zaidi kuhifadhia maji kuliko mabwawa au makaro yaliyowazi. Mbu na konokono hawawezi kuishi katika vyombo vilivyofunikwa. Kufunika tenki za kuhifadhia maji pia hupunguza upotevu wa maji kutokana na mvukizo.

Makaro na mabwawa ya kuhifadhi maji yanatakiwa kuwa na kina kirefu ili kupunguza upotevu wa maji kupitia mvukizo.

Zuia uvujaji

A leaking tap.

Maji mengi yanaweza kupotea kutokana na kuvuja, mvukizo na ufyonzaji wa ardhi. Ili kuzuia upotevu wa maji, hakikisha bomba au koki zinafungwa vizuri. Ziba au badilisha bomba au tenki ambazo zinavuja pale inapogundulika. Uvujaji pia ni dalili ya hatari ya maji kuchafuliwa kwa sababu vimelea vya magonjwa na uchafu vinaweza kuingia kwenye mabomba au tenki kupitia matundu hayo yanayosababisha uvujaji.



Ukurasa huu ulihuishwa: 04 Juni 2022