Hesperian Health Guides

Vuna maji ya mvua

Katika sura hii:

Uvunaji wa maji ya mvua ni njia rahisi mojawapo ya kujihakikishia upatikanaji wa maji salama. Maji ya mvua ni salama kwa ajili ya kunywa isipokuwa katika maeneo yenye kiwango kikubwa cha uchafuzi wa hewa. Uvunaji wa maji ya mvua ni suluhisho bora kwa matatizo yote mawili ya uhaba wa maji, na usalama wa maji.

Tenki zinaweza kujengwa juu ya ardhi karibu na nyumba. Paa la nyumba hukusanya maji ya mvua na kuyaelekeza kwenye tenki hizo. Paa ambazo zimetengenezwa kutokana na debe au bati ndiyo bora zaidi kwa ajili ya uvunaji. Paa za nyasi kawaida hukusanya uchafu mwingi ambao unaweza kuathiri usalama wa maji. Paa ambazo zimetengenezwa kutokana na chuma chenye risasi, vigae na lami huwa na kemikali zenye sumu ambazo zitafanya maji yasiwe salama kwa ajili ya kunywa. Ni muhimu pia kuhakikisha kuwa pipa, ndoo na vyombo vingine kwa ajili kuvuna na kuhifadhi maji ya mvua ni salama na havikuwahi kutumika kuhifadhi kemikali zenye sumu, kama vile mafuta ya mitambo au viuatilifu.

Gutters hanging from the edge of a roof funnel rainwater into barrels with taps.
Kutumia paa la bati kuvuna maji ya mvua'


Hifadhi zingine za maji juu ya ardhi, kama mabwawa, zinaweza kutumika pia kuvuna maji yanayotiririka juu ya ardhi pamoja na maji ya mvua. Ili kutengeneza hifadhi rahisi kwa ajili ya kukusanya maji ya mvua, chimba shimo ardhini na kushindilia udongo, au malizia kwa kutumia udongo wa mfinyanzi, vigae, zege au tandiko la plastiki. Hifadhi hizi za maji ya mvua zinaweza kutumika kunywesha wanyama au vyanzo vya maji ya kuoga na matumizi mengine. Iwapo hifadhi hiyo itatumika kwa ajili ya maji ya kunywa, inapaswa kuzungushiwa uzio ili kuzuia wanyama. Maji kutoka hifadhi za maji juu ya ardhi, yakiwemo mabwawa, yanapaswa kutibiwa kabla ya kutumika kwa ajili ya kunywa.

Maji yanayovunwa kutoka kwenye paa za nyumba au kwenye mabwawa yanaweza pia kuelekezwa na kuhifadhiwa kwenye tenki zilizojengwa chini ya ardhi. Hii ni njia nzuri ya kuhifadhi maji katika hali ya ubaridi na yakiwa yamefunikwa. Inaweza pia kuwa na gharama nafuu, kuliko kujenga au kununua tenki zinazokaa juu ya ardhi.

Jinsi ya kuboresha usafi wa maji ya mvua ili yaweze kufaa kwa ajili ya kunywa

Maji ya mvua yanapaswa kulindwa dhidi ya uchafuzi ili yaweze kuwa salama kwa ajili ya kunywa. Hatua za msingi za kuhakikisha usalama wa maji ya mvua ni pamoja na:

  • Kabla msimu wa mvua kuanza, kusafisha tenki, bomba linaloingiza maji kwenye tenki, paa na bati za kutega mvua.
  • Kamwe usitumie vyombo ambavyo vilitumika kuhifadhi mafuta, viuatilifu na kemikali nyingine zenye sumu kwa ajili ya maji.
  • Mvua ya kwanza ya msimu itumike tu kusafisha paa, bati za kutegea maji ya mvua, na tenki.
  • Funika mdomo wa tenki na kuweka chujio ili kuzuia wadudu na uchafu mwingine kuingia. Hii pia husaidia kuzuia mbu kuingia na kuzaliana.
  • Kinga maji kwa njia ya koki kama inawezekana. Kama maji yatachotwa kwa kutumia ndoo au vichoteo vingine, hakikisha vifaa hivyo ni safi na salama.
  • Kwa usalama zaidi, weka klorini kusafisha maji, au kichujio maalum cha maji kiunganishwe na tenki.
  • Usikoroge au kutikisa maji kwenye tenki ili yabaki yametulia. Kwa kufanya hivyo uchafu au wadudu wowote waliomo watatuama na kubaki chini kwenye tenki.
  • Kusafisha paa mara kwa mara kutasaidia pia kuongeza usafi wa maji ya mvua yanayovunwa.
Uvunaji wa maji ya mvua jangwani – Thar, rajastathan, India

Njia mojawapo ya uvunaji maji ya mvua katika jangwa ya Thar, Rajasthan huko India ni kwa kutumia mabwawa ya vijiji yaitwayo Naadi. Kila mwanakjiji na hata wapita njia wanaruhusiwa kutumia maji hayo.


Near a naadi, a man leads a camel pulling a water carrier on wheels.

Kila mwanakijiji huchangia kazi ya kutunza bwawa hilo-Naadi. Sheria ambazo zimekuwepo enzi na enzi huzuia watu kukata miti karibu na kingo za Naadi au kwenye vyanzo vya maji yanayoingia kwenye Naadi. Mifugo na wanyama wengine hawaruhusiwi kusogelea bwawa hilo, wala watu kuchafua mazingira yake kwa kujisaidia haja ndogo au kubwa karibu na bwawa hilo. Mara moja kwa mwezi wanakijiji hukusanyika kusafisha bwawa kwa kutoa mchanga na uchafu mwingine ambao unaweza kuwa umelundikana ndani ya bwawa. Usafishaji huongeza kina cha bwawa hilo na kuondoa vijidudu ambavyo vinaweza kuwa chini ya bwawa. Baada ya usafishaji, wanakijiji huruhusu maji ya mvua kuingia, kutulia na kuwa safi tena. Kwa njia hizi, jamii hufanya kazi pamoja kulinda maji yao.


Ukurasa huu ulihuishwa: 04 Juni 2022