Hesperian Health Guides

Usafirishaji salama wa maji

Katika sura hii:

Ni muhimu kuhakikisha kuwa maji yanabaki safi na salama wakati wa kuyasafirisha kutoka kwenye chanzo chake hadi eneo walipo watu ambao wanayahitaji. Ubebaji maji ni miongoni mwa kazi ngumu ya kila siku katika jamii yoyote ile, na mara nyingi hufanywa na wanawake na wasichana. Ubebaji mizigo mikubwa ya maji kichwani, mgongoni au kwa kamba iliyofungwa kichwani unaweza kusababisha maumivu ya mara kwa mara ya kichwa, mgongo, athari kwa uti wa mgongo na hata kusababisha mwanamke kupoteza ujauzito kutokana na msongo.

Miradi ya uboreshaji wa huduma ya maji inaweza kupunguza mzigo huu. Mabadiliko kidogo, wakati mwingine, yanaweza kurahisisha usafirishaji wa maji. Mifumo ya maji inaweza kujengwa kwa njia ambazo zitaondoa haja ya kubeba maji kutoka mbali. Afya ya jamii itakuwa bora zaidi iwapo wanaume wataelewa umuhimu wa kazi hii katika maisha ya familia na kushiriki ipasavyo katika jukumu la kuchota na kubeba maji.

Sw EHB Ch6 Page 87-3.PNG

Maji ya bomba

Mfumo wa usambazaji maji kwa njia ya bomba una faida nyingi. Maji ya bomba hupunguza hatari ya maji kuchafuliwa na ni nadra konokono na mbu kuishi ndani ya bomba. Hata hivyo, mfumo wa maji ya bomba ambao umejengwa vibaya, na usiotumika kwa usalama, unaweza kuruhusu uchafuzi mkubwa wa maji hata kuliko maji yanayotiririka wazi bila mfumo wa bomba. Mfumo wa huduma ya maji ya bomba lazima upangwe kwa uangalifu, kwa kuzingatia kiasi cha maji ambayo yanahitajika na yaliyopo hivi sasa, na kiasi gani kitahitajika kwa siku zijazo kadri jamii yako inavyokua.

A woman points to water spouting from the ground by a man holding a pickaxe.
Lazima awepo mtu au kikundi kazi chenye wajibu wa kufanya matengenezo ya bomba kila zinapoharibika.

Maji ya bomba yanaweza kusukumwa kawaida kutoka kwenye vyanzo vyote vya maji. Hata hivyo, vyanzo vikuu ni chemchemi na hifadhi kama mabwawa. Chanzo rahisi na chenye gharama nafuu zaidi ni kile kilichopo kilimani juu ya makazi ya jamii ambacho huruhusu maji kutiririka kutoka kwenye chanzo kwa msukumo wa kawaida wa asili. Mifumo mingi ya maji ya bomba hupeleka maji kwenye tenki kuu la hifadhi. Tenki kuu la hifadhi linaweza kutibiwa kwa kutumia klorini, au kuunganishwa na chujio maalum la kutibu maji. Baada ya hapo maji husafirishwa kutoka kwenye tenki kuu la kuhifadhia na kusambazwa kwenye mabomba kuelekea nyumba za watu au koki za umma katika jamii.

Mfumo wa maji ya bomba unahitaji matunzo ya mara kwa mara. Ni muhimu kuwa na kumbukumbu za mtandao mzima wa bomba ili kuzuia ajali, na pia kurahisisha ukaguzi na matengenezo ya kawaida. Mabomba makubwa yanayovuja yanaweza kupoteza maji mengi, kuruhusu maji kutoka vyooni kuingia pamoja na uchafu mwingine, na kusababisha mazalia ya mbu na konokono. Kama mabomba yamefungwa kwa katani, pamba na kamba za ngozi, sehemu hizo zinaweza kuvutia vijidudu vya magonjwa kuota juu yake na kuchafua maji yaliyoko ndani ya bomba.



Ukurasa huu ulihuishwa: 04 Juni 2022