Hesperian Health Guides

Kuboresha chanzo cha maji

Kabla ya kujaribu kuanzisha mradi mpya wa maji, labda itakuwa rahisi zaidi kukarabati mradi wenu uliopo sasa ili uweze kutoa maji ambayo ni safi na salama zaidi. Wakati wa kuandaa mpango wa kuboresha huduma ya maji ni muhimu kuanza kwa kuorodhesha rasilimali zote zilizopo mahali husika. Rasilimali ni pamoja na vyanzo vya maji, vifaa vya ujenzi, na muhimu zaidi, watu. Wajumuishe watu wenye ujuzi au utaalam wa kujenga visima, matenki, kutandaza mabomba na wengine ambao wanaweza kuongoza shughuli za vikundi. Pia orodhesha wazee katika eneo hilo ambao wanakumbuka namna huduma ya maji ilivyokuwa ikipatikana miaka iliyopita.

2 women stand on the lip of a well.
Maji yanaweza kuchafuliwa iwapo watu watasimama kwenye miaka iliyopita. kingo za kisima au kutumia ndoo zisizo safi kuchota maji.

Tafuta ufumbuzi

Hatua za kuboresha huduma ya maji ambazo jamii itachukua zinaweza kutegemea aidha matatizo ambayo yanahitaji ufumbuzi wa haraka, au matatizo ambayo ni rahisi kutatuliwa kwanza. Hata hivyo, ni muhimu kuandaa mpango ambao unalenga sababu za msingi za matatizo yaliyopo na unaozingatia mahitaji ya makundi yote katika jamii.

Iwapo tayari kuna mfumo wa huduma ya maji, jamii inaweza:


Iwapo kuna uwezekano kwamba maji yamechafuliwa na kemikali za sumu, tumia chanzo kingine hadi maji hayo yatakapopimwa kuthibitisha ubora wake. Iwapo kipimo kitaonyesha maji yamechafuliwa, endelea kutumia chanzo kingine cha maji na kushughulikia chanzo cha uchafuzi. Jaribu kuzuia uchafuzi wa maji yenu kwa kuvitaka viwanda kushughulikia taka zao kwa njia salama zisizoathiri mazingira kwa ujumla, na kutumia njia salama za uzalishaji zinazolinda mazingira. Pia ni muhimu kuwaomba wakulima kupunguza matumizi ya viuatilifu na mbolea za viwandani zenye madhara kwa binadamu.

Amua kila chanzo cha maji kitumike kwa ajili ya nini, hasa iwapo kuna maji kidogo au ni shida kuyapata. Ujenzi wa matenki ya kuvuna na kuhifadhi maji ya mvua, au mfumo wa usambazaji maji wa bomba vinaweza kusaidia kuleta maji karibu na jamii. Jamii nzima inapaswa kuchangia upatikanaji wa maji salama ya kutosha. Wanawake na wanaume kwa pamoja washiriki katika:

3 women post a sign on a wall reading "Community Water Meeting Today."

Wanawake washiriki katika kupanga huduma ya maji

Wanawake wanaweza kuwa na mahitaji tofauti ya maji kuliko wanaume. Vile vile, kawaida, wanawake ndiyo wachotaji, wabebaji na wahusika wakuu wa usafi wa maji katika kaya. Lakini mara nyingi wanaume ndiyo wasimamizi wa ujenzi na utunzaji wa mifumo ya maji. Kwa sababu ya tofauti hizi katika kazi za wanaume na wanawake, kawaida mahitaji ya wanawake na hata watoto husahaulika. Hivyo, ni muhimu kupanga kwa kuzingatia mahitaji maalumu ya wanawake, watoto, na hata makundi mengine yaliyo katika hatari zaidi.

Miduara miwili

Zoezi hili huwasaidia wanawake kutafakari juu ya mahitaji yao ya maji na vikwazo wanavyokabiliana navyo.

Muda: Dakika 45

Vifaa: Karatasi kubwa, kalamu za kuchorea

 1. Wezesha washiriki kujigawa katika vikundi vya watu wasiozidi 10. Gawa karatasi za kuchorea kwa kila kikundi.
 2. Kila kikundi kichore miduara 2 kwenye karatasi - mduara mkubwa na mduara mdogo ukiwa ndani yake.
 3. Ndani ya mduara mkubwa, kila mtu achore au aorodheshe matatizo yanayohusiana na maji, usafi na afya ambayo yanaathiri jamii nzima. Ndani ya mduara mdogo chora au orodhesha matatizo yanayowaathiri wanawake pekee.
 4. Yalete makundi tena pamoja na kujadili: Matatizo katika miduara 2 yanatofautiana namna gani? Matatizo katika miduara hiyo miwili yanafanana namna sani? Ni ufumbuzi gani unaweza kupatikana kwa ajili ya matatizo yote? Tunawezaje kuhakikisha kuwa matatizo ya wanawake yanashughulikiwa ipasavyo?
  A small group of women wearing saris sit on mats and talk.

  Zoezi hili pia linaweza kufanywa na wanaume na wanawake kwa pamoja. Iwapo wanaume watashiriki, hakikisha kundi moja linakuwa la wanaume pekee.

  • Wezesha kila kundi kuchora miduara miwili midogo ndani ya mduara mkubwa badala ya mmoja tu.
  • Ndani ya mduara mdogo mmoja waorodheshe matatizo yanayowasibu wanawake na mwingine ujumuishe matatizo yanayowasibu wanaume.
  • Baada ya hatua hii makundi yote yakae pamoja tena.
  • Waambie wanaume wafikirie namna ambayo wanaweza kusaidia kuboresha hali inayowaathiri wanawake.


  Njia za ufumbuzi zinaweza kujumuisha ujenzi wa vyoo karibu na kaya, wanaume pia kushiriki katika kutafuta na kubeba maji, kutumia muda zaidi kukaa na watoto, na njia nyingine.

  Ni jambo la faraja kwa wanawake kujadili matatizo yao katika faragha kabla ya wanaume kujadili matatizo ya kwao. Katika jamii nyingi, wanaume na wanawake wanatofauti kubwa za maoni juu ya mambo mbalimbali.

Vikwazo katika kuboresha upatikanaji wa maji

Zipo sababu nyingi kwa jamii kukosa huduma ya maji safi na salama. Matatizo yanaweza kuwa ni pamoja na ukosefu wa fedha, utaalam mdogo wa kujenga mifumo ya maji, kutokuwepo msaada wa serikali, wanajamii husika kutoshiriki ipasavyo, au hata rushwa na ubadhirifu katika usimamizi na utekelezaji wa miradi ya jamii. Ili kuwepo huduma endelevu ya maji safi na salama, vikwazo hivyo havina budi kubainishwa na kuondolewa, kimoja baada ya kingine. Jamii inaweza kushiriki zaidi katika kuboresha na kuendeleza miradi yao ya maji iwapo miradi hiyo itatoa matarajio ya:

 • Matokeo ya haraka kama vile ongezeko la maji, upatikanaji rahisi au magonjwa kupungua.
 • Gharama nafuu za maji.
 • Mabadiliko, japokuwa madogo, katika maisha ya kila siku.
 • Faida kwa mazingira kama vile kupunguza matope, kupunguza mbu, au ongezeko la maji kwa ajili ya bustani na mahitaji mengine ya kiuchumi.
A line of women and children with water containers, one in a wheelchair, wait for a turn at a village pump.
Mradi endelevu wa maji unapaswa kuondoa vikwazo vya kimiundombinu na kijamii, na kumsaidia kila mmoja katika jamii kwa usawa.


Ufumbuzi unaweza kupatikana ndani ya jamii husika

Kihistoria, kila jamii imeweza kubuni njia zake za kutafuta, kusafirisha na kulinda maji. Watu wameweza kutumia fimbo za kutabiri uwepo wa maji chini ya ardhi, wamegundua vifaa vya kuchotea maji na kuyasafirisha, wamejenga mifumo mbalimbali ya kuvuna maji ya mvua, na wamepanda miti ili kulinda vyanzo vya maji. Pia wamefanya mikataba au maelewano na jamii za jirani kushirikiana katika matumizi ya maji. Matumizi mazuri ya maji na uzuiaji migogoro kuhusiana na maji husaidia kuhifadhi rasilimali ya maji kwa ajili ya vizazi vijavyo, pamoja na kujifunza njia mpya za kuongeza upatikanaji wa maji na kulinda yasichafuliwe ili yaweze kuwa salama zaidi.

Jinsi wanakijiji wa kawaida walivyowafundisha wataalam wa maendeleo

Kundi la waelimishaji jamii lilifika katika kijiji kimoja sehemu ya milimani nchini Colombia kusaidia wanakijiji kupambana na ugonjwa wa kuhara, na kulinda vyanzo vyao vya maji. Walipotembelea chanzo kikuu cha maji cha kijiji, waligundua kwamba ng’ombe na mmomonyoko wa udongo vilikuwa vinaharibu chemchemi. Waelimishaji jamii hao walipendekeza njia mbili rahisi za ufumbuzi: Kuweka uzio wa seng’enge kulinda chanzo hicho, au kulisha mifugo sehemu nyingine.

flowering cactus plants.
Wanakijiji hawakupenda mawazo haya. Walitabiri kwamba waya wa seng’enge kwenye uzio huo ungeibiwa baada ya muda mfupi. Pia hawakuwa na ardhi wala fedha za kutosha kwa ajili ya kutengeneza malisho maalum. Badala yake, walifikia uamuzi wa kuandaa siku maalum kwa ajili ya kazi ya upandaji wa mimea yenye miba kuzunguka eneo la chemchemi kuu. Hatua hii iliwazuia mifugo na kuwalazimisha kunywa maji sehemu za chini mbali na chemchemi hizo. Hatimaye, tatizo hili kwa wanakijiji lilipata ufumbuzi.Ukurasa huu ulihuishwa: 04 Juni 2022