Hesperian Health Guides

Kuongeza uelewa wa jamii

A group of women gather to talk near some makeshift dwellings.

Mwanamke anayebeba maji kutoka umbali mrefu kila siku hahitaji kuambiwa juu ya ada ya maji. Ila anaweza asihisi kama anao uwezo wa kubadilisha hali hiyo.

Pale watu wanapoona kwamba huduma ya maji salama na ya kuaminika ni tatizo lao wote, wanaweza kuanza kufanya kazi pamoja ili kuleta mabadiliko. Kuongeza uelewa wa jamii mara nyingi ndiyo hatua ya kwanza katika kuleta mabadiliko, na kawaida hujumuisha kundi la watu wakichukua hatua kadhaa kwa pamoja.

Zungumza na wasimamizi wa huduma ya maji

 • Je, katika eneo lako, yupo mtu, kundi, kampuni au mamlaka inayosimamia visima, mabomba au mifumo mingine ya usambazaji maji?
 • Je, yupo mtu au kundi linalohusika na usafi wa mazingira, hususan vyoo?
 • Ni watu gani au makundi ambayo mara nyingi hutafuta, hubeba, hutibu na kuyahifadhi maji?
 • Orodhesha watu wote wanaohusika na huduma ya maji, pamoja na vyanzo vyote vya maji katika eneo lako. Watu wanasema nini kuhusiana na ubora na kiwango cha upatikanaji wa maji?
 • Ni kiasi gani cha maji ambacho hutumika kila siku?
 • Je, vyanzo tofauti vinatumika kwa ajili ya maji ya kunywa, kupikia, kuoga, kunywesha mifugo, kumwagilia mazao, na matumizi mengine?
 • Je kuna maji ya kutosheleza mahitaji yote haya?
 • Je kuna chanzo cha maji au hifadhi ya maji kwa matumizi ya dharura?

Tembelea sehemu ambazo watu huchota maji

map of a village.

Vyanzo tofauti vya maji vinaweza kuwa na matatizo tofauti na hivyo kuhitaji ufumbuzi tofauti. Tembelea chemchemi, visima, vyanzo vya maji yaliyopo juu ya ardhi (mito, vijito, maziwa na madimbwi), na maeneo yanayokusanya maji ya mvua. Anzisha mjadala namna maji haya yanavyotumika na iwapo mtu yeyote anahisi kuwa yanaweza kuwa yamechafuliwa (sio salama).

Tengeneza ramani ya vyanzo vya maji katika eneo hilo na vyanzo vya uchafuzi

Ramani yako inaweza kuonyesha mahali vilipo vyanzo vya maji kutoka nyumba za watu na vyanzo vya uchafuzi. Tumia rangi mbalimbali kuonyesha vyanzo vya maji salama na vyanzo ambavyo vimechafuliwa.

Je, maji yenu ni salama?

Ni vigumu kujua iwapo maji ni salama au la. Baadhi ya vitu ambavyo husababisha matatizo ya kiafya ni rahisi kuvigundua kwa kuviangalia tu, kunusa, au kuyaonja maji. Vingine vinaweza kugundulika kwa kuyapima maji katika maabara. Ni muhimu kufahamu chanzo cha uchafuzi wa maji na kuchukua hatua za ulinzi dhidi ya uchafuzi ili kuzuia matatizo ya kiafya.

ZoeziMaji yanaweza kuonekana safi kwa macho lakini yasiwe salama

Zoezi hili linaonyesha jinsi maji yanavyoweza kuwa na uchafu hatari ndani yake ambao hauwezi kugundulika kwa macho, kunusa au kuonja.

Muda: Dakika 15 – 30

Vifaa: Chupa 4 ambazo zinaweza kuonyesha wazi kilichopo ndani, tope, chumvi, sukari na maji yaliyotibiwa

 1. Kabla ya zoezi, jaza chupa 4 maji yaliyochemshwa au kutibiwa kwa klorini au kwa njia nyingine inayofaa ili yawe salama. Katika chupa ya kwanza, ongeza kijiko kimoja cha tope. Katika chupa ya pili ongeza kijiko kimoja cha sukari. Katika chupa ya tatu, ongeza kijiko kimoja cha chumvi. Tikisa chupa hizo zote vizuri. Usiongeze chochote katika chupa ya nne. Chupa hizo nne ziletwe mbele ya kikundi.
 2. Wezesha wanakikundi kunusa maji katika kila chupa. Halafu wakaribishe kuonja maji kutoka chupa yoyote kati ya hizo. Kuna uwezekano mkubwa kuwa hakuna atakayeonja maji ya tope, lakini wengi wanaweza kuonja maji kwenye chupa zile nyingine.
 3. A woman holding a cup licks her fingers.
 4. Baada ya watu kadhaa kuonja maji hayo, waulize kwa nini hawakuonja maji ya chupa yenye tope. Halafu waulize maji waliyoonja yalikuwa na ladha gani, na walifikiri yalikuwa na nini? Je kuna mtu yeyote aliyeonja maji ya chupa ambayo haikutiwa kitu chochote? Waulize walijuaje kwamba hayakuwa na kitu chochote ambacho wangeweza kuona au kugundua kwa kunusa au kuonja.
 5. Wezesha mjadala juu ya vitu ambavyo vinaweza kuwa kwenye maji na kuyafanya yasiwe salama kwa ajili ya kunywa. Vitu hivyo vinaweza kujumuisha vijidudu vinavyosababisha kuhara, na viuatilifu au kemikali nyingine. Je, kuna sababu zozote za kuamini kwamba vitu hivi hatari vinaweza kuwa kwenye maji yenu? Je, mbali na kutazama na kunusa, kuna njia nyingine ambazo zinaweza kutusaidia kujua iwapo maji ni salama au la?

Kupima usalama wa maji

a water-testing kit.
Vipimo vya ubora wa maji huonyesha tu iwapo maji yalikuwa yamechafuliwa wakati na mahali ambapo sampuli ya maji hayo ilichukuliwa.

Ubora wa maji kawaida hupimwa kwa kuchunguza sampuli ya maji katika maabara. Vipimo hivi huonyesha aina na kiasi cha uchafuzi, na kawaida ni muhimu katika kuchunguza kiwango cha uchafuzi wa kemikali. Lakini vipimo hivi vinaweza kuwa ghali. Vipo vifaa vya kupima maji ambavyo vinaweza kutumika katika ngazi ya kaya kujua iwapo maji yana vijidudu ambavyo vinaweza kusababisha magonjwa au la. Vipimo hivi vya gharama nafuu hutoa matokeo ya haraka. Lakini vipimo vya aina hii wakati mwingine hushindwa kutofautisha vijidudu visivyo na madhara na vijidudu vyenye madhara. Vilevile, havionyeshi iwapo kuna kemikali au mayai ya vijidudu vya magonjwa kwenye maji. Hivyo, pamoja na kuwepo kwa vipimo vya maabara na vingine vyenye gharama nafuu, kuongeza uelewa wa jamii kuhusu masuala ya maji na utunzaji madhubuti wa vyanzo vyake ni muhimu zaidi.Ukurasa huu ulihuishwa: 04 Juni 2022