Hesperian Health Guides
Sehemu ya nne: Misitu
HealthWiki > Mwongozo wa jamii juu ya afya ya mazingira > Sehemu ya nne: Misitu
Baada ya kusoma sehemu ya nne, utakuwa umejifunza: |
|
Misitu hutoa rasilimali muhimu kwa binadamu kama vile chakula, kuni, vifaa vya kujengea, magogo, dawa na vitu vingine vingi. Miti na misitu pia ina nafasi muhimu sana katika kuhifadhi na kuendeleza afya ya mazingira. Inatunza hewa, maji safi, kuzuia mmomonyoko na mafuriko, kurutubisha ardhi na mimea, kutengeneza makazi kwa ajili ya ndege na wanyama, kutoa kivuli na kuyafanya mazingira yetu kupendeza.
Ili misitu iendelee kutoa rasilimali na kutengeneza mazingira yenye afya, inatakiwa kutunzwa na kutumiwa kwa busara. Lakini kwa sababu misitu inaharibiwa na viwanda vya magogo pamoja na jamii, na ardhi yenye misitu sehemu mbalimbali inahitajika kwa ajili ya matumizi mengine, misitu ulimwenguni kote inakatwa kwa haraka kuliko inavyooteshwa. Wakati mwingine kampuni za magogo au viwanda hutumia misitu kuwapatia watu vyanzo vya pato ambalo kwa kweli wanahitaji sana.
Hata hivyo ni lazima kutafuta urari kati ya mahitaji ya sasa ya ardhi na rasilimali za misitu, na wajibu wa kulinda raslimali hizi kwa ajili ya vizazi vijavyo. Raslimali inapotumika kupita kiasi, husababisha madhara makubwa ya muda mrefu. Jamii nyingi ambazo zimeishi kwa kutegemea misitu zinaelewa fika kuwa zitaathirika sana iwapo sehemu kubwa ya misitu itatumika au kufyekwa kabisa.
Vuguvugu la Ukanda wa Kijani
Wangari Maathari, mwanamke kutoka Afrika Mashariki nchini Kenya anasema, mlima Kenya ulikuwa mlima wenye aibu- daima ukiwa umejificha kwenye mawingu. Mlima huu ni mtakatifu kwa watu wake kwa sababu mito mingi hutiririka kutoka kwenye misitu ambayo hapo awali ilifunika vilele vya mlima huu. Hivi sasa mlima Kenya hauna aibu tena-upo uchi. Mawingu ambayo yalikuwa yakiufunika yametoweka na vivyo hivyo misitu. Na pamoja na upotevu wa misitu na mawingu, mito pia imeanza kukauka.
Wakati akikua, Wangari alishuhudia jinsi gani ufyekaji misitu ulivyokuwa ukisababisha mmomonyoko wa ardhi, upotevu wa vyanzo vya maji na uhaba wa kuni. Alianza kuelewa kuwa ufyekaji misitu ulikuwa ukisababisha umasikini na ukame.
Hivyo Wangari akaanza kupanda miti. Wangari aliunda kikundi cha kina mama cha kupanda miti kuzunguka nyumba zao na mashamba. Kwa sababu walipanda miti kwa mstari au ‘ukanda’, walikuja kujulikana kama Jumuiya au shirika la ‘Ukanda wa Kijani”. Akina mama hawa kutoka Ukanda wa Kijani walianza kuwafundisha watu wengine jinsi maisha yao yalivyokuwa yanathiriwa na ufyekaji misitu, na kuwahimiza nao kupanda miti. Waliwapelekea wakulima miti ya matunda na kuipanda kwenye miteremko ya vilima ili kuzuia mmomonyoko. Kwa kupanda miti mijini na vijijini ili kutengeneza bustani za kijani, kutoa vivuli, na kupata kuni, walionyesha jinsi upandaji miti unavyoweza kutatua matatizo mengi. Shirika wa Ukanda wa Kijani pia ulipanda bustani za mboga-mboga, kutengeneza mabwawa madogo ambayo yalivuna maji ya mvua na kuendesha warsha ili kusaidia watu kuweza kuelewa mahitaji ya misitu bora.
Katika kubeba wajibu wa kulinda mazingira yao, shirika lilitambua kuwa wanahitaji msaada wa serikali yao ili kutunza mazingira kwa faida ya Wakenya wote. Upandaji miti uligeuka kuwa ishara ya vuguvugu la amani na demokrasia nchini Kenya. Migogoro ilipotokea baina ya jamii mbalimbali, shirika lilituma ‘miti ya amani’ kuwasuluhisha.
Akiwa mwanamke aliyepanda miti, Wangari akawa shujaa katika nchi yake. Lakini alikumbana pia na matatizo magumu mengi. Baada ya kushindwa kuishi na mke jasiri, mume wake alimwacha. Kwa sababu alifanya kazi miongoni mwa watu maskini, alikamatwa na serikali. Lakini kwa sababu ya ujasiri wake na juhudi za maelfu ya Wakenya, shirika la Ukanda wa Kijani lilifanikiwa kupanda miti kwa mamilioni.
Mwaka 2004, Wangari Maathai alishinda tuzo yenye heshima kubwa duniani ya Nobel. Alipewa tuzo hiyo kutokana na kupigania na kukuza amani kupitia mpango endelevu uliohusisha demokrasia, haki za binadamu na usawa kwa wanawake. Na hayo yote yalianza kwa kupanda miti.