Hesperian Health Guides
Hifadhi za misitu
Baadhi ya jamii huendelea kutumia rasilimali katika misitu iliyohifadhiwa kwa makubaliano maalum na serikali na jamii nyingine katika eneo hilo, ili kuweza kusimamia rasilimali hizo kwa pamoja. Huu ni ‘mpango wa usimamizi wa pamoja’.
Mipango ya usimamizi wa pamoja huruhusu watu kuendelea na matumizi yao ya jadi na endelevu ya misitu na mazao yake. Jamii zinazosimamia hifadhi za msitu zinaweza pia kuelimisha jamii nyingine kuhusu umuhimu wa kulinda msitu.
Utunzaji misitu ambao huimarisha ustawi wa watu na miti
Katika msitu mkubwa wa Amazoni nchini Brazili, migogoro kawaida huibuka kati ya makampuni ya uvunaji magogo, wafugaji wa ng’ombe,na wengine ambao hushi kwa kukata miti, kulima msituni, kuvuna zao la utomvu wa mpira, na kutengeneza vifaa mbalimbali kutoka msituni. Baada ya sehemu kubwa ya msitu kufyekwa, wafanyakazi na wakazi wa asili wa eneo hilo hatimaye walishawishi serikali kuanzisha hifadhi zinazoruhusu uvunajimaeneo makubwa ya msitu yanayolindwa ili yasiangamizwe, lakini yakiwa wazi kwa matumizi kiasi yanayoruhusiwa.
Kwa bahati mbaya,hata watu walioshi katika maeneo ya msitu huo kwa miaka mingi walinyimwa haki ya kutumia hifadhi hizo zinazoruhusu uvunaji. Msitu ambao waliupigania sana kuulinda usingeweza kuwasaidia tena katika maisha yao.
Watu katika jamii hizo kawaida wameishi maisha yao yote wakitegemea kilimo, uwindaji, na matumizi ya rasilimali za misitu kutengeneza bidhaa mbalimbali vikiwemo vikapu na mitumbwi. Lakini wanahitaji pia dawa, vitendea kazi, nishati, umeme na vitu vingine ambavyo huwalazimu kuwa na vyanzo vya pato. Kwa msaada wa kifedha, waliweza kuanzisha karakana. Kwa kutumia miti iliyokatwa kutoka maeneo yao ya kilimo, waliweza ktengeneza samani na kuiuza kwa wanajamii katika eneo hilo na kote nchini Brazili.
Pato hili liliwafanya kufikiria bidhaa nyingine kutokana na mbao ambazo zingewawezesha kupata fedha zaidi. Lakini hawakuruhusiwa kukata mti wowote uliosimama bila kuwepo “hesabu ya miti kwenye msitu” na “mpango endelevu wa usimamizi” uliyoidhinishwa na Wizara ya Mazingira.
Kutimiza matakwa ya serikali, walipaswa kukusanya taarifa kuhusu idadi ya miti iliyopo kwenye msitu na kiasi gani cha miti huota kila mwaka. Serikali haikuamini kuwa wanakijiji, wengi wao wakiwa hawajui kusoma wala kuandika, wangeweza kufanya kazi hiyo. Kumbe wanakijiji walikuwa watalaam hasa wa misitu. Kwa miaka mingi walikuwa wakiwaoongoza wanasayansi ya mazingira, wakiwafundisha juu ya wanyama na mimea katika msitu huo. Wanasayansi nao walikuwa wamewafundisha kutumia zana rahisi kupima ukuaji wa mti, na kukokotoa kiasi cha miti ambayo iliota kila mwaka. Wanakijiji waliandaa mpango wa kuzalisha bidhaa ndogo lakini zenye bei ya juu, na hivyo kuwianisha matumizi yao ya miti na idadi ya miti mipya ambayo inaota kila mwaka.
Wizara ya Mazingira ilikubali mpango huu, na hivi sasa karakana hiyo huwawezesha wanakikiji kupata fedha bila kuuharibu msitu.
Wanakijiji kwenye eneo hilo la msitu wa Amazoni wameweza kufanya kile ambacho wanasayansi, wachumi na wafanyakazi wa maendeleo ya jamii wamekuwa wakihangaika kufanikisha kwa muda mrefu-kuanzisha mpango wa usimamizi wa misitu ambao ni endelevu kwa jamii na misitu wao.