Hesperian Health Guides
Uharibifu wa misitu
HealthWiki > Mwongozo wa jamii juu ya afya ya mazingira > Sehemu ya nne: Misitu > Uharibifu wa misitu
Watu wasiotegemea misitu moja kwa moja bado wanatumia mazao mengi yanayotokana na misitu kama vile vitabu na magazeti, vifaa vya ujenzi, chakula kama nyama, soya, mafuta ya mawese, na madini yanayochimbwa chini ya misitu. Ni mara chache watu kufikiria kupanda upya misitu iliyoharibiwa kwa njia hizi.
Iwapo rasilimali za misitu hazitatumika na kusimamiwa kwa njia ambazo zinaruhusu misitu kuendelea kukua na kuzalisha, karibu misitu yetu yote itapotea. Sababu za uharibifu mkubwa wa misitu ni pamoja na:
- Ukataji wa miti yote katika eneo moja kwa ajili ya magogo au upasuaji mbao: Hali hii husababisha mgandamano na mmomonyoko wa ardhi, uharibifu wa maisha ya viumbehai vya porini na kujaza uchafu kwenye mito na njia zingine za maji .
- Kilimo cha mashamba makubwa: Ufugaji wa ng’ombe wengi na mashamba ya miti mara nyingi huhusisha ufyekaji wa misitu ili kupata ardhi inayohitajika kwa ajili ya mashamba hayo.
- Mashamba ya kamba maeneo ya pwani: Mashamba hayo huanzishwa kwanza kwa kusafisha maeneo oevu yenye mikoko na misitu mingine ya pwani. Hali hii husababisha jamii ndogo za wavuvi kukosa riziki, uchafuzi wa maji, ongezeko la magonjwa, umaskini na utapiamlo.
- Viwanda vya kutengeneza karatasi: Huzalisha taka zenye sumu ambazo huchafua ardhi, maji na hewa.
- Miradi ya ujenzi wa mabwawa makubwa: Husababisha maeneo makubwa ya misitu kufunikwa na maji. Watu hulazimika kuhama kutoka eneo la mafuriko na kukata miti ili kutengeneza makazi mapya na mashamba.
- Kampuni za uchimbaji madini, mafuta na Gesi: Hukata miti na kuzalisha taka zenye sumu ambazo huchafua maji, ardhi na hewa.