Hesperian Health Guides
Misitu na riziki
Misitu ni chanzo muhimu cha riziki. Baadhi ya serikali, mashirika na kampuni za kimataifa hudai kuwa uharibifu mkubwa zaidi wa misitu husababishwa na watu masikini ambao hukata miti kwa ajili ya kilimo au kupata riziki kwa namna yoyote ile. Lakini pale watu wanapokuwa hawana chakula cha kutosha, pato au mahitaji mengine ya msingi, uhai wao unakuwa muhimu zaidi kuliko kuhifadhi misitu. Wakati mwingine watu hawana njia mbadala isipokuwa kukata miti, iwe katika kusafisha shamba, kuvuna kuni au kwa ajili ya mbao au kuchoma mkaa. Ni nadra sana viwanda au kampuni kubwa kulaumiwa kwa uharibifu wa misitu, pamoja na kwamba hupokea kiwango kikubwa cha mbao, na kukata miti na misitu kwa ajili ya shughuli za uchimbaji madini, kutafuta mafuta au kuanzisha mashamba makubwa.
Watu wanapofanikisha mahitaji yao ya kila siku, wanakuwa katika hali nzuri zaidi kufikiria maisha ya baadae likiwemo suala la kutunza mazingira. Watu waishio ndani ya misitu na kuitunza wanajua kwamba, zipo njia nyingi za kujipatia riziki kutokana na misitu bila kusababisha madhara makubwa. Mara nyingi, ufyekaji wa misitu husababishwa na mahitaji ya viwanda na shinikizo la umaskini.
Uharibifu misitu husababisha umasikini, na umasikini husababisha uharibifu misitu zaidi. |
Yaliyomo
Shughuli za kilimo ndani ya msitu
Wakulima katika sehemu nyingi husafisha maeneo yaliyo wazi ndani ya misitu na kupanda mazao bila kuathiri msitu unaozunguka. Hulima eneo hilo hadi magugu yanapoanza kuzidi mazao yao. Baadaye husafisha eneo lingine la wazi, huku eneo la zamani likirudia kuota tena, kuwa msitu na kurudishia ardhi rutuba yake.
Aina hii ya kilimo imekuwa ikifanyika kwa miaka mingi, lakini kadri idadi ya watu inavyozidi kuongezeka na makazi mapya kuanzishwa, misitu iliyopo kwa ajili ya kilimo cha aina hii imepungua. Hakuna ardhi ya kutosha kuruhusu mashamba yaliyolimwa mwanzoni kuota na kuwa sehemu ya msitu. Kilimo cha aina hii siyo endelevu tena kwa mkulima na msitu. Jamii zinazoendesha kilimo katika maeneo ya msitu wanaweza kupata matokeo mazuri zaidi na kubaki kwenye ardhi yao kwa muda mrefu iwapo tu watatumia mbinu endelevu za kilimo.
Kulinda misitu na riziki
Katika misitu ya Andra Pradsh nchini India, wanavijiji hufyeka sehemu za msitu ili kupanda mazao. Lakini katika miezi yenye uhaba wa chakula, riziki ya wengi wao hutegemea vitu vinayvoota ndani ya msitu. Baadhi ya wanavijiji hukusanya na kuuza kuni, wakati wengine hutumia miti kutengeneza vifaa mbalimabali vya kuuza. Matumizi ya rasilimali za misitu na wanakijiji hudhibitiwa na “Kamati za Jamii za Msitu”.
Baada ya Kamati za Misitu kuona kuwa baadhi ya maeneo yalikuwa yakiharibiwa kutokana na matumizi makubwa mno, walitengeneza sheria mpya kupunguza kiasi cha mbao ambacho kilikuwa kinavunwa. Sheria zilikuwa kali mno na riziki ya watu ilikuwa hatarini. Watu waliokuwa wanaishi kwa kuuza mbao, kuni na kutengeneza vifaa mbalimbali walipoteza chanzo hiki cha pato. Katika miezi yenye uhaba wa chakula, familia hizi ziliteseka.
Wajumbe wa kamati za misitu walitoka kwenye jamii hii, na hivyo walitaka kupata ufumbuzi ambao ungehakikisha kuwa hakuna atakayeathiriwa na njaa, lakini kwa wakati huo huo misitu ikiwa salama. Baada ya mikutano mingi, uamuzi ulifikiwa. Badala ya kubadili sheria mpya za misitu, kamati za misitu ziliamua kusaidia kuboresha eneo la mashamba kwa kujenga matuta ya kupunguza kasi ya maji na kuzuia mmomonyoko wa ardhi. Hii ingesaidia kurutubisha ardhi, upatikanaji wa maji kwa ajili ya mazao, mashamba kuzalisha zaidi, na kuwepo chakula kwa kila mtu bila kuathiri misitu.
Utalii ekolojia
Utalii ekoljia ni njia ya kupata fedha kutoka kwa wageni wanaokuja kuangalia uzuri wa asili wa eneo husika, au kujifunza kuhusu mimea na wanyama wanaoishi katika eneo hilo. Baadhi ya miradi ya utalii ekolojia huvutia watu kuburudika tu na uzuri wa asili. Wengine huwaalika kuja kuishi na watu katika jamii hiyo ili kujifunza jinsi ya kutunza mazingira. Lakini miradi mingine hualika watalii kuja kufanya kazi katika miradi ya kulinda mazingira.
Utalii ekolojia ni chanzo muhimu cha pato kwa jamii zinazopakana na misitu. Lakini kuanzisha na kuendesha mradi wa utalii ekolojia kunaweza kuwa na gharama kubwa, na kawaida huhitaji kuandaliwa kwa uangalifu. Watalii wanahitaji huduma nzuri, mathalan chakula, utulivu, malazi, waongozaji wenye utalaam na subira katika kushughulikia tofauti za kiutamaduni. Wanaweza kupatwa na ajali au kuhitaji huduma za afya za kawaida. Kupata watalii kuja kuwatembelea kunahitaji matangazo katika magazeti au tovuti, kuchapisha brocha na kupitia njia nyingine za utangazaji.
Miradi ya utalii ekolojia inapaswa kusimamiwa vizuri ili fedha wanazoleta watalii ziinufaishe jamii, na siyo wakala wa nje, biashara au familia chache. Miradi ya utalii ekolojia yenye mafanikio kawaida hudhibiti idadi ya watalii wanaotembelea eneo husika ili kupunguza shinikizo kwa jamii na athari kwa mazingira.
Mazao mengine ya misitu pembeni na mbao
Mazao mengine ya misitu pembeni na mbao ni chochote pembeni na mbao ambacho kinaweza kuchukuliwa kutoka msituni na kwenda kuuzwa bila kuathiri msitu. Bidhaa hizo ni pamoja na matunda, dawa ya mitishamba na kamba. Jamii ambazo zimefanikiwa kuuza mazao mengine ya misitu wameona umuhimu kuzingatia taratibu zifuatazo:
- Kuweka sheria wazi kuhusu nani anaweza kuvuna na kuuza zao, na njia za uvunaji endelevu. Mara zao husika linapoonyesha mafanikio, kuna hatari ya kuvunwa kupita kiasi. Vuna tu kiasi ambacho kitaruhusu zao hilo kuendelea kukua na kuzaliana.
- Tafuta au kuza soko kwa ajili ya zao husika. Hakuna maana kuvuna zao kama haliuziki au kutumiwa.
Kuvuna dawa kutoka msituni
Karibu na Bengali nchini India, watu wengi huenda kwa waganga wa jadi pale wanapougua. Waganga hawa hutengeneza dawa kutokana na mitishamba iliyokusanywa kutoka msituni. Siku moja, watu kutoka shirika lisilo la kiserikali walifika kijijini hapo kusaidia kuwafundisha wanajamii jinsi ya kujipatia fedha kutokana na kukusanya dawa za mitishamba na kuziuza mijini. Kwa kutumia taasisi hii kuuza dawa hizo, waliisaidia jamii kupata fedha kutoka msituni bila kukata miti.
Wanakijiji walifurahi kupata njia mpya ya kujipatia pesa na watu wengi wakaanza kukusanya na kuuza dawa za mitishamba. Lakini hawakuwauliza waganga wa jadi jinsi gani ya kukusanya mitishamba bila kuiharibu, na hawakuwa maakini kuhusu kiasi gani wanafaa kukusanya.
Katika vuguvugu ya kujipata pesa zaidi, baadhi ya wanavijiji waliharibu miti iliyokuwa chanzo cha dawa hizo. Badala ya kuchimba kuzunguka mti ili kuchukua mizizi michache, baadhi ya watu walikata kabisa mti na kuuangusha chini. Kwa muda mfupi, mimea ya dawa ilikaribia kutoweka msituni. Hali hii iliwaacha waganga wa jadi bila mimea kwa ajili ya kutengeneza dawa. Hivyo walipoumwa, wanavijiji walijikuta wakitumia fedha nyingi kununua dawa kutoka kwenye maduka ya dawa. Mwisho wake, afya za watu wa msituni ziliathirika kutokana na kuvuna mitishamba kwa njia zisizoendelevu.