Hesperian Health Guides

Matumizi endelevu ya misitu

Usimamizi endelevu wa msitu humaanisha kusimamia na kutunza misitu kwa njia ambazo zinakidhi mahitaji ya kila siku ya sasa, pamoja na kulinda misitu hiyo kwa ajili ya mahitaji ya baadaye. Njia endelevu hazilingani kila mahali. Kila jamii inahitaji kujua njia zipi hasa zinafaa kwao na misitu yao.

Maandalizi ya mpango endelevu wa usimamizi wa misitu husaidia jamii kuamua njia bora ya kutumia misitu yao. Unaweza pia kusaidia katika kupinga vitisho mbalimbali kwa msitu kutoka viwandani au hata serikalini. Mara nyingine, unaweza kupata bei nzuri ya mazao ya misitu iwapo utaweza kuthibitisha kuwa bidhaa hizo zilizalishwa kwa njia endelevu. Lakini kikubwa zaidi kuhusu mpango wa usimamizi endelevu wa msitu, ni kwamba husaidia jamii kufanya kazi pamoja katika kuutumia na kuulinda msitu.

Njia za kutumia na kulinda msitu kwa wakati mmoja ni pamoja na:

 • Kupunguza msongamano wa mimea na miti: Huruhusu mwanga wa jua zaidi kuingia msituni na kuwezesha mimea inayotakiwa kukua.
A group of closely spaced trees with narrow trunks next to a group of widely spaced trees with thick trunks.
Kupunguza miti maana yake ni kukata baadhi ya miti ili ile inayobaki iweze kukua na kustawi zaidi.
 • Kujazia uotoupya: Maana yake ni kupanda miti mipya au mimea chini ya miti ya zamani, au kwenye maeneo yaliyo wazi iwapo miti haiwezi kuota yenyewe.
 • Kupanda miti baada ya kuvuna mti: Hii huhakikisha kuwepo kwa miti na mbegu mpya baada ya miti mikubwa kuvunwa.
 • Usafishaji kwa moto: Uchomaji moto kwa uangalifu husaidia kupunguza mabaki ya mavunomti chini ya msitu. Njia hii husaidia kuachia virutubisho kuingia kwenye udongo, na pia kuua wadudu ambao wanaweza kuharibu miti. Moto kwa ajili ya usafishaji unapaswa kudhibitiwa kwa uangalifu ili usienene na kusababisha uharibifu.
 • Uvunaji wa mpangilio: Hujumuisha kuvuna baadhi ya miti iliyokomaa, huku ukibakisha miti ambayo haijakomaa na mingine iliyokomaa ili kulinda ardhi na kutoa mbegu kwa ajili ya mahitaji ya baadaye.


Illustration of the above: A landscape of tree stumps next to a landscape with some stumps and some mature trees.
Uvunaji wa mpangilio hulinda baadhi ya miti kwa ajili ya mahitaji ya baadaye, wakati huohuo misitu ikiendelea kukua
 • Kuvuna na kuuza mazao mengine ya msitu tofauti na mbao: Njia hii huwezesha kuendelea kuutunza msitu wakati huohuo ukipata riziki.
 • Kuwalipa wafugaji ili wasiingize mifugo yao kwenye misitu, au wakulima ili wasikate miti iliyopo kwenye mashamba yao: Utaratibu huu unaweza kuchangia ustawi wa misitu na kuzuia migogoro.
 • Kuhifadhi njia na maeneo ya wanyamapori kupita au kushi: Hii huruhusu wanyamapori kuishi na kupita katika eneo husika.
 • Kupanda miti maeneo ya wazi: Kupanda miti katika sehemu zilizo wazi ambapo miti mingi imekatwa, au mahali ambapo msitu umetoweka kabisa ni njia ya kuboresha ardhi, maji na hewa- iwe ni kwenye jiji lenye watu wengi au mji mdogo.
 • Kusaidia misitu kuota upya: Hii inawezekana kwa kupunguza matumizi ya maeneo ambayo yamepoteza miti mingi ili misitu ipate fursa ya kuota upya.
 • Kutumia wanyamakazi: Matumizi ya wanyamakazi katika kukokota magogo husababisha madhara kidogo ikilinganishwa na tingatinga na zana nyingine nzito.
Illustration of the above: Oxen pull a log through a forest, next to a tractor pulling a log through the same forest.
Wanyamakazi hawagandamizi sana ardhi kama zana nzito.
 • Kupogoa magome na matawi kutoka kwenye miti iliyoangushwa kabla ya kutolewa nje ya msitu hupunguza madhara kwa mimea mingine pale miti inapovutwa. Magome na matawi huoza na kurutubisha ardhi.
 • Kuendeleza utalii-ekolojia: Huzalisha pato zaidi kwa kuwaonyesha watalii uzuri asilia wa msitu bila kukata miti au kuharibu mazingira.
In a forest, people hunt, log, and gather plants and firewood.
Tumia maarifa ya kila mtu, zingatia mahitaji ya kila mtu

A man chops a tree with an axe.

Lengo la zoezi hili ni kusaidia jamii kutafakari jinsi ya kutumia na kutunza rasimali zao za misitu kwa njia ambazo zitamwezesha kila mtu kunufaika. Zoezi linaweza kujumwisha watu 25 waliogawanywa katika makundi madogo 3. Ni muhimu kumshirikisha kila mtu ambaye ataathirika kutokana na maamuzi kuhusu matumizi ya msitu.

Muda: Saa 3-6 (au zaidi ya kipindi kimoja ili mradi uwe umezihifadhi ramani)

Vifaa: Kalamu, penseli, daftari, karatasi kubwa 3 zenye ramani ya eneo lako, na gundi. Ramani zinaweza kuchorwa kiurahisi ili mradi tu watu waweze kutambua kile kinachoonyeshwa.

A child gathers sticks.
 1. Gawa ramani moja kwa kila kikundi. Mwaambie kila mtu achore kile anachofanya anapokuwa msituni (mfano kukata kuni, kulisha mifugo, kutafuta matunda na mimea, kuwinda nk.) kwenye daftari zao.
 2. Katika kila kikundi, kila mtu azungumzie kile walichochora na maana yake kwao. Mtu moja au wawili baadaye wachore picha kwenye ramani kubwa kuonyesha wapi na namna gani kila mtu anavyotumia msitu.
 3. A woman gathers fruit in a basket.
 4. Vikundi viunganishwe pamoja kwa ajili ya majadiliano kuhusu yale yaliyomo kwenye ramani zao kubwa:
  • Je kuna sehemu za msitu ambazo zinatumiwa zaidi kuliko nyingine?
  • Je wanaume, wanawake, watoto na wazee wana matumizi tofauti ya msitu?
  • Je kulikuwa na jambo la kushangaza au lisilo la kawaida kuhusu matumizi ya misitu?
 5. Wezesha majadiliano kuhusu afya ya msitu kwa kuuliza maswali yafuatayo:
  • Je msitu bado unatoa rasilimali kama ilivyokuwa siku za nyuma?
  • Je kuna ndege, wanyama na mimea michache kuliko siku za nyuma?
  • Je kuna sehemu ambazo miti yote imekatwa?
  • Nini kinafanyika sasa katika maeneo hayo?
 6. Trash discarded in a forest.

 7. Mtu mmoja au wawili waweke alama kwenye ramani zao, kwa kutumia rangi mbalimbali, kuonyesha wapi misitu inastawi, wapi imeharibiwa au imetoweka kabisa.
 8. Fikiria kuhusu maeneo mengine ya misitu na kujadili mabadiliko gani ambayo watu wangehitaji kuyaona. Orodhesha mabadiliko haya kwenye ramani, au kwenye ubao au bango kitita. Baadhi ya maswali ambayo unaweza kutumia yameelezewa chini ya kipengele kinachofuata. A goat eating a plant.


Andaa mpango wa usimamizi wa msitu

Baada ya kufanya zoezi lililopita, fikiria maswali yafuatao:

 • Misitu hutupatia faida na rasilimali zipi?
 • Je ni miti, mimea na wanyama gani ambao hutumika? Ni kiasi gani hutumika kila msimu? Je kuna maeneo ambapo rasilimali hizi zimekuwa zikipunguwa au zimetoweka kabisa?
 • Tunausaidiaje msitu? Je jamii huwa inapanda miti, kulinda baadhi ya maeneo au inatekeleza njia nyingine za kuhakikisha msitu unaendelea kustawi?
 • Je, baadhi ya sehemu za msitu zizuiwe kutumika kabisa? Je hii itaathiri vipi watu ambao wanatumia sehemu hiyo ya msitu?
 • Je, ni vema mbinu endelevu zitumike katika baadhi ya sehemu? Je jamii inayo elimu inayostahili kuhusu matunzo ya msitu ambayo inaweza kusaidia kuleta mabadiliko?
 • Ni mbinu gani ambazo tunahitaji ili kufanikisha usimamizi endelevu wa misitu?
  • Kama hatuna mbinu hizo, tunaweza kujifunza?
  • Je tutahitaji kutegemea taasisi nyingine?
  • Tunawezaje kuanzisha ushirikiano na asasi zenye moyo na uwezo wa kutusaidia kupata mbinu na maarifa hayo?
 • Jamii yetu ifanye nini kubaki na mamlaka juu ya miradi yetu ya msitu? Jamii zilizojipanga vizuri na ambazo zinatoa ujumbe thabiti na unaoeleweka, kwa watu wa nje ya jamii hiyo, kuhusu kile hasa wanachotaka kawaida hupata manufaa mengi kutokana na miradi endelevu ya msitu.
 • Tutayafikishaje mazao yetu sokoni? Mara nyingi ni ghali kupeleka mazao kwenye masoko ya kitaifa na ya kigeni kuliko kuuza bidhaa hizo katika masoko ya kawaida katika maeneo husika. Hata hivyo, bei katika masoko ya kawaida ni duni ingawaje gharama za uuzaji ziko chini.
 • Je mazao yetu ya misitu yatakuwa na thamani gani? Kama huna uhakika kwamba unapata bei nzuri kwa ajili ya mazao ya misitu, huenda ukahitaji kuwasiliana na asasi za biashara zinazotoa taarifa juu ya bei za bidhaa.
 • Mpango mpya wa usimamizi wa msitu utaleta mabadiliko gani? Je, mpango huu mpya wa usimamizi wa msitu utapunguza uwezo wa watu kutumia msitu? Jamii itawasaidiaje katika hali hiyo?
2 people speak while looking at a chart.
Tukivuna kiasi kikubwa cha miti mwaka huu, tunaweza kukosa miti ya dawa ya kutosha mwakani.
Pia tunahitajika kutunza miti ya kuni ya kutosha msimu mzima wa masika.

Ubia kwa ajili ya ulinzi wa msitu

Kujenga ubia na idadi kubwa ya vikundi ambavyo vinanufaika kutokana na msitu, husaidia kuhakikisha kwamba msitu unatumika kwa njia ambazo zinakidhi mahitaji ya kila mtu. Ubia na watu wa nje ya eneo lako pia husaidia katika kulinda haki zako.

Kufanya kazi pamoja kulinda msitu wa Amazoni

Wakazi wa Amazanga hawakuwa wakiishi mahali walipo sasa kwa miaka yote. Ajali ya mafuta yaliyomwagika na kuathiri eneo la kabila lao la Kichua iliwalazimisha kuhama eneo lao la asili karibu na misitu ya Amazoni. Pale makazi yao mapya yalipoanza kutishiwa na uharibifu wa misitu na kilimo cha mashamba makubwa ya kibiashara, wanakijiji waliamua kwamba kusimamia ardhi yao kwa mujibu wa mila na utamaduni wao-uwindaji, uvuvi, na ukusanyaji wa mimea ya chakula na dawa, ndiyo ilikuwa njia bora ya kulinda maeneo yao.


Lakini hii ilihitaji ardhi zaidi kuliko waliokuwa nayo.Kijiji cha Amazanga kiliitaka serikali kukipatia eneo mahali babu zao waliishi. “Hatuwezi kuishi kama manamba”, walisema. “Tunataka kuishi katika eneo letu, tukiwa na haki na uhakika wa kutumia msitu wetu”. Serikali ilivyopuuza madai yao,waliomba mashirika ya mazingira ya kimataifa msaada wa kurudisha maeneo yao ya asili kwa kuyanunua tena.


Wanakijiji waliwaalika wabia wao wa kimataifa kuja kupiga picha na kuchukua mikanda ya video inayoonyesha njia za asili za kutumia msitu, na kuwaonyesha watu katika nchi zao. Baada ya miaka kadhaa, kijiji cha Amazanga kilifanikiwa kuchangisha fedha za kutosha kununua kiasi cha hkta 2000 za msitu.


Lakini ununuzi wa ardhi yenye ukubwa huu ilisababisha wasiwasi miongoni mwa kabila jirani la Shuara. Watu wa Shuara nao walipodai kuwa eneo hilo ni lao, watu wa Amazanga waligundua walikuwa wamekosea. Walikuwa wamejenga ubia na mashirika ya kimataifa, lakini wakasahau kuweka mikataba ya maelewano na jirani zao!. Watu wa kabila la Shuara walikuwa na hasira na kutishia kuanzisha vurugu. Baada ya mikutano mingi, hatimaye jamii za Amazanga na Shuara walikubaliana kuumiliki msitu huo kwa pamoja chini ya kanuni walizojiwekea.Kwa kuwa makabila hayo yote mawili yana asili ya matumizi mazuri ya misitu, waliweza kuanzisha ushirikiano.


Waliligeuza eneo hilo kuwa hifadhi ya msitu na kukubaliana juu ya mpango wa usimamizi ambao ulizuia ukataji miti holela na kupitisha miundo mbinu. Eneo hilo liliamuliwa kuwa chini ya “uangalizi wa makabila yote ya asili ya Amazoni”, na kuhifadhiwa kwa ajili ya vizazi vijavyo. Kwa kushirikiana na watu wa mbali na karibu, watu wa Amazanga watalinda msitu wao, kutunza utamaduni wao, na kuwasaidia wengine kulinda urithi wao ikiwemo misitu.

Ukurasa huu ulihuishwa: 04 Juni 2022