Hesperian Health Guides

Migogoro kuhusiana na misitu

Katika sura hii:

Kwa sababu kuna uhaba wa rasilimali za misitu, migogoro mara nyingi hutokea miongoni mwa watu ambao wanahitaji kutumia rasilimali hizo kwa njia mbalimbali. Migogoro pia hutokea kati ya jamii zinazotegemea misitu hiyo na viwanda nje ya jami ambavyo pia vinahitaji rasilimali hizo.

Igizo dhima

  1. Wezesha washiriki wajigawe katika vikundi vya watu watano na kukipa kila kikundi maelezo mafupi kuhusu hali ambayo inaweza kusababisha mgogoro juu ya rasilimali za misitu. Weka mazingira ya kusadikika miongoni mwa watu, lakini epuka hali ambayo inaweza kuleta aibu au chuki kwa watu watakaoshriki. Kutakuwa na uhalisia zaidi kwenye maigizo endapo washiriki watavaa mavazi kulingana na nafasi wanazoigiza.
  2. A group of people sit and discuss.
  3. Kila kikundi kitumie dakika 15-20 kuandaa igizo la dak. 5. Mhamasishe kila mtu aweze kushiriki. Kila kikundi kiwasilishe igizo lao. Baada ya kila igizo, ongoza majadiliano kuhusu migogoro ya kijamii na kutafuta suluhisho. Au unaweza kusubiri hadi vikundi vyote kuonyesha maigizo yao ndipo majadiliano yafanyike kwa pamoja.
  4. Umejisikiaje? Baada ya kila kikundi kuonyesha igizo na kabla ya majadiliano, uliza kila mshiriki jinsi alivyojisikia kuigiza nafasi yake. Waulize watu walioangalia igizo jinsi walivyojisikia wakati wa igizo na jinsi waigizaji walivyowafanya wajisikie kuhusu migogoro.
    A woman speaks.
    Mwezeshaji anatakiwa kuwa na uelewa juu migogoro iliyopo katika jamii na kuwa mwangalifu kuhusu mwitiko wa watu mbalimbali kuhusu majadiliano hayo. Wakati wa igizo, uwe makini katika kuweka mazingira salama na yenye uwazi ili watu wasiogope kuchangia.

    Chagua baadhi ya visa vifuatavyo kuandaa igizo kuhusu migogoro ya misitu. Au andaa maigizo mengine ambayo yataonyesha hali ya migogoro katika eneo lako.

    A woman speaks to a man who stands by a cow.

    Kisa 1: Wahusika: mwanaume akiwa na ng’ombe; waganga wa mitishamba, washiriki katika mkutano wa jamii.

    Baada ya miaka kadhaa akiwa mbali na jamii yake, mwanaume mmoja anarudi akiwa na ng’ombe 10 na kuanza kuwalishia kwenye ardhi na msitu wa jamii. Watu walipokwenda msituni kukusanya mitishamba na majani ya kuezekea wakakuta ng’ombe wamekula sehemu kubwa na kuacha kidogo tu. Wanaamua kuitisha kikao ili kujadili tatizo hilo. Bwana mwenye ng’ombe anasisitiza kwamba ni haki yake kulishia ng’ombe wake eneo hilo hata kama watakula kiasi gani. Wanajamii wengine wanakataa. Nini kitafuata baadaye?

    Kisa 2: Wahusika: vijana wa kiume wakatamiti, wafanyakazi wa serikali, wanawake wakusanyaji kuni.

    A woman yells and gestures to another woman and a man.

    Vijana kadhaa wa kiume wanakata miti kwenye eneo la kijiji bila kibali na kuuza mbao kwa wafanyakazi wa serikali ya mtaa ambao huchukua mbao hizo, kuzipakia kwenye gari na kuondoka nazo. Mwanamke anaenda mahali pake pa siku zote anapokusanya kuni na kukuta vijana wa kiume wanakata ovyo miti. Mmoja wa hao vijana ni mwanae. Anarudi kwenye jamii na kuwaeleza akina mama wa vijana wengine. Siku iliyofuata wanawake hao wanakwenda msituni kuwaambia vijana hao kuacha kukata miti. Mama wa kijana wa kwanza anasema anatarajia pesa itakayotokana na mauzo ya miti hiyo ili akanunue dawa kwa ajili ya mjukuu wake. Nini kitafuata?

    Kisa 3: Wahusika-wanajamii wakiwa na shoka, ng’ombe wa maksai, wafanya kazi wa serikali wakiwa na msumeno mkubwa wa mnyororo na gari la mizigo, na wajumbe wa baraza la kijiji.

    A big truck hauls lumber.
    Kwa miaka mingi, watu wanakata miti kwa kutumia shoka na kuibeba kwa kutumia ng’ombe wa maksai. Sasa watu kutoka serikali ya mtaa wamekuwa wakija na misumeno ya minyororo na kukata miti huku wakisema kuwa ni mali ya serikali. Siku moja watu wa serikali walikuja na tingatinga na zana nyingine nzito. Wanataka kujenga barabara katikati ya msitu ili waweze kukata miti mikubwa. Kundi la wanaume kutoka kwenye jamii hiyo wanakwenda kupambana nao. Nini kitafuata baadaye?

  5. Jadili kila igizo Waambie waigizaji kuondoa nguo walizovaa kuigiza nafasi zao, kuziweka pamoja chumbani na kurudi kwenye kundi. Baadae uliza maswali ambayo yatasaidia washiriki:
    • kueleza kile kilichojili kwenye igizo,
    • kutambua vitendo vilivyosababisha mgogoro,
    • kuainisha mahitaji mbalimbali ambayo ndiyo yalikuwa mzizi wa mgogoro,
    • kupendekeza njia za muda mrefu za kutatua mgogoro.

    Rudia hatua hii kwa kila igizo. Mwezeshaji anaweza kuandika mawazo muhimu kwenye karatasi kubwa, bango au ubao.

Maswali ya kuchochea mjadala ni kama vile

A group of people sit and discuss.
  1. Nini kilichosababisha mgogoro?
  2. Kwa nini mwanaume yule aliona ana haki ya kulishia ng’ombe wake msituni?
  3. Ni kwa kiasi gani uharibifu wa msitu uliathiri jamii?
  4. Kwa hiyo ni mambo gani yalihitajika ili kusiwepo na mgogoro?
  5. Je kuna njia yoyote ambayo mambo haya yote yanaweza kufikiwa ili kusiwepo na mgogoro?

Rudia hatua hii kwa kila igizo. Mwezeshaji anaweza kuandika mawazo muhimu kwenye karatasi kubwa, bango au ubao.

Kama majadiliano yatasababisha mgongano, ni muhimu kumaliza kwa njia ambayo itawaweka watu wote pamoja, mathalan kwa kuimba wimbo au kufanya jambo lolote kwa pamoja ili kuwasaidia kujisikia vizuri.



Ukurasa huu ulihuishwa: 04 Juni 2022