Hesperian Health Guides
Misitu na afya
Yaliyomo
Misitu na maji
Baadhi ya watu wanaamini kuwa miti huvutia mvua na huhifadhi maji kwenye udongo karibu na usawa wa ardhi. Wengine wanaamini kuwa miti hutumia maji mengi zaidi kuliko kiasi inachochangia, na kwamba hushindana na mazao kwa ajili ya maji hayo. Kutegemea na aina ya miti, mahali inapooteshwa na mazingira mengine, fikra zote hizi mbili zinaweza kuwa za kweli.
Udongo wenye rutuba kwenye misitu na mizizi mirefu ya miti husaidia kuchuja maji. Pale dawa za kuulia wadudu, vyuma na kemikali nyingine zenye sumu vinapochafua maji yaliyo juu na chini ya ardhi, misitu husaidia kuchuja na kuondoa sumu hizo. Maji yaliyochujwa huingia na kuimarisha uhai wa visima, mito na maziwa, na hifadhi zingine za maji, pamoja na afya za watu wanaoishi maeneo hayo.
Bila misitu kulinda vyanzo vyetu vya maji, kutakuwa na upungufu wa maji safi na salama kwa ajili ya kunywa na kuoga. Kutokana na sababu zote hizi, kawaida ni bora kuiacha miti iendelee kustawi kuliko kuikata, hasa kama kuna maji ya kutosha na salama.
Hata hivyo, baadhi ya miti, hasa miti ambayo hukua haraka na ni ngeni katika eneo husika, inaweza kunyonya maji yote yaliyopo. Kwa wakulima na wengine wanaotaka kulinda vyanzo vya maji, ni muhimu kutafiti jinsi miti tofauti inavyoathiri maji na kufanya uamuzi wa busara kuhusu aina gani ya miti inafaa kupandwa.
Misitu na hali ya hewa
Misitu ni muhimu sana kwa hali ya hewa na tabia nchi. Misitu huchangia kupoza hali ya joto kwa kuleta ubaridi na unyevunyevu, na pia kurekebisha hewa ya baridi kwa kuipa joto na ukavu. Miti hukinga nyumba na mazao shambani dhidi ya upepo mkali na jua kali, na pia kutoa kivuli wakati wa mvua nyingi. Kwa kiasi kikubwa, misitu hupambana na ongezeko la joto duniani kwa kunyonya uchafu wa sumu katika hewa. Hii husaidia kuleta unafuu katika tabia nchi ya dunia. Kadri tunavyozidi kupoteza sehemu kubwa ya misitu, hatari ya majanga ya asili kama vimbunga, ukame na joto-kali inaongezeka.
Misitu huzuia mmomonyoko wa ardhi na kupunguza mafuriko
Kwa kuongeza kiasi cha majani juu ya ardhi, kivuli kwa mimea ambayo inaota chini ya miti, na kuhifadhi udongo mahali pake kwa kutumia mizizi yake, miti huzuia mmomonyoko na kupunguza mafuriko. Pia hupunguza kasi ya maji ya mvua na kuyasambaza juu ya ardhi, ili yaweze kuingia ardhini kuliko kutiririka hovyo na kupotea.
Pale misitu inapofyekwa, udongo husafirishwa hadi kwenye mito na vijito. Mvua kubwa zinapoanza kunyesha, ardhi inakuwa haina uwezo tena wa kunyonya na kuhifadhi maji ya mvua. Badala yake, maji hutiririka haraka juu ya ardhi na kusababisha mafuriko. Kutunza miti na misitu husaidia kuelekeza maji kupita mkondo wake wa asili.
Anuwai ya misitu na afya
Katika msitu, ni rahisi kuuona utando wa maisha kwa sababu msitu unaostawi una kila aina ya mimea na wanyama. Utando huu wa maisha hulinda afya za watu kwa njia nyingi. Nyuki na wadudu wengine wanaoishi kwenye miti hurutubisha mazao ili yaweze kutoa maua na kuzaa matunda. Nyigu na wadudu wengine hula baadhi ya wadudu ambao huvamia mazao. Popo, ndege na mijusi hula mbu wanaoeneza malaria, homa ya manjano na magonjwa mengine. Wanyama wengine wa msituni hudhibiti panya, nzi, funza na kupe kwa kuwawinda, au kushindana nao, na hivyo kuwazuia kusambaza magonjwa.
Pale makazi ya watu yanapojengwa mahali au karibu na misitu iliyoharibika, idadi na aina za wanyama hupungua kwa sababu makazi na chakula chao vimepungua. Pia wanyama ambao wanabaki hulazimika kuishi karibu na watu. Hali hii husababisha uwezekano wa magonjwa ya wanyama kuwapata binadamu. Kwa kutunza misitu ya kutosha kwa ajili ya ustawi wa wanyama na mimea mbalimbali, tunalinda afya za binadamu.
Misitu, chakula, nishati na dawa
Misitu kawaida ina aina mbalimbali za matunda, mbegu, mizizi, wadudu, na wanyama ambao wanaweza kutumika kama chakula na dawa kwa watu. Misitu inapoharibiwa, mara nyingi husababisha njaa, utapiamlo na magonjwa. Watu wanaotegemea rasilimali hizi wanalazimika kutafuta mbadala ili waweze kuishi. Kadri chakula na dawa kutoka misituni vinapozidi kupotea, utaalamu wa kuvishughulikia pia unapotea, ambao ni sehemu muhimu ya sayansi ya jadi na utamaduni wa jamii.
Mahali penye uhaba wa rasilimali, watu mara kwa mara hulazimika ama kuacha misitu iendelee kustawi au kukata miti hiyo na kulima mazao ya chakula. Lakini hata kwa wakulima ambao wanakata miti ili kupata sehemu ya kupanda mazao ya chakula, ni muhimu kuacha baadhi ya miti. Hivyo, katika sehemu ambazo kilimo kinashindana na misitu, ni muhimu kuweka uwiano.
Mzigo kwa wanawake
Kubeba mizigo mikubwa ya kuni kwa mwendo mrefu kunaweza kusababisha maumivu ya kichwa, mgongo, na kwa watoto athari kwenye uti wa mgongo. |
Wanawake na watoto mara nyingi ndiyo hufanya kazi ya kukusanya na kubeba kuni kwa ajili ya kupikia. Uzito wa kazi hii kwa miaka mingi unaweza kuwaletea matatizo ya kiafya. Kadri misitu inavyoharibiwa, watu lazima watembee mwendo mrefu kutafuta kuni. Hali hii huwanyima muda wa kutosha wa kufanya shughuli nyingine muhimu, pamoja na kwenda shuleni.
Wanawake na watoto wanaweza pia kupigwa na hata kubakwa pale wanapokwenda kutafuta kuni. Kutokana na hili, wanawake na wasichana sehemu nyingi hutembea katika vikundi wanapokwenda kutafuta kuni wakati wa mchana. Kwa kupanda na kutunza miti vizuri kwa ajili ya kuni karibu na nyumbani, usalama na afya ya watu wanaolazimika kutafuta kuni utakuwa na uhakika zaidi.