Hesperian Health Guides
Kuifanya jamii na maliasili zetu kuwa endelevu
HealthWiki > Mwongozo wa jamii juu ya afya ya mazingira > Sehemu ya kwanza: Tuhifadhi maliasili kwa manufaa ya wote > Kuifanya jamii na maliasili zetu kuwa endelevu
Uendelevu pia humaanisha kuweza kumudu mahitaji ya watu ya kila siku ya sasa wakati tukiendelea kupanga kwa ajili ya mahitaji ya vizazi vijavyo. Moja ya changamoto kubwa zinazoikumba dunia leo ni kujaribu kukidhi mahitaji ya watu wote bila kuathiri mazingira ambayo hutulisha, hutupatia malazi, mavazi, maji, nishati, dawa na hasa msingi wa uhai wetu.
Kila upande, tumezungukwa na dalili za maendeleo yasiyo endelevu. Kuna uhaba mkubwa wa chakula bora, hewa safi, maji safi na shughuli salama za kujikimu. Pia kuna ongezeko la uchafuzi, ukataji hovyo miti na misitu na magonjwa. Kadri jamii zinapoendelea kukua katika hali ambayo siyo endelevu, zinazidi kujisababishia matatizo makubwa na hata kwa vizazi vijavyo.
Katika moduli hii nzima, tunatoa mifano ya misingi ya uendelevu. Misingi hiyo muhimu ya uendelevu ni pamoja na: kuheshimu Bioanuai, mfungamano wa viumbe hai, kufanya kazi kwa kuheshimu asili ya dunia, kuzuia madhara kutokana na uchafuzi, na daima kuchukua tahadhari kwanza.
Yaliyomo
Kuheshimu mfungamano wa viumbe hai: Bioanuai
Dunia inajumuisha viumbe hai vya aina nyingi. Bioanuai ni neno la kisayansi linalomaanisha mjumuiko wa idadi kubwa ya viumbe hai tofauti duniani ambavyo hutegemeana kwa namna moja au nyingine. Viumbe hai hivyo ni pamoja na watu, mimea, wanyama na wadudu. Zamani kabla wanasayansi hawajaibua msamiati huu wa bioanuai, watu wengi walikuwa wakiwafundisha watoto wao jinsi viumbe hai vinavyotegemeana. Kwa mfano, watu hukusanya na kula matunda yenye virutubisho muhimu kwa afya zao kutoka kwenye miti au mimea. Matunda haya huota kwenye miti au mimea baada ya maua yake kurutubishwa na wadudu.
Bila maua kurutubishwa, matunda hayawezi kuota. Ndege hula wadudu na ndege huwindwa na wanyama wengine mfano mbweha. Uwiano katika mfumo wa viumbe hai huhakikisha kuwepo kwa maua ya kutosha, wadudu, ndege na mbweha, na viumbe hai vyote kuishi katika eneo moja. Kama mbweha wengi watauawa, eti kwa sababu wanakula kuku wa wanakijiji, huenda pengine idadi ya ndege ikaongezeka na kula wadudu na hata vifaranga vya kuku kupita kiasi. Kwa njia hii, kuua mbweha wengi kunaweza kusababisha upatikanaji kidogo wa matunda.
Kwa bahati mbaya, dunia inakabiliwa na upotevu mkubwa wa bioanuai huku aina nyingi za wanyama na mimea zikiendelea kutoweka kila mwaka. Kama jinsi utando wa buibui unavyokuwa imara kutokana na wingi wa nyuzi zinazouunganisha, bioanuai pia hutegemea mfungamano unaounganisha viumbe hai vyote.
Uharibifu wa bioanuai husababisha magonjwa mapya kuibuka
Upotevu wa bioanuai husababisha aina za mimea na wanyama kupungua, na uwiano wa asili miongoni mwa mimea, wanyama na watu kutoweka. Hii inaweza kusababisha magonjwa mapya. Kuna mifano 2 ambayo inaonyesha jinsi upotevu wa bioanuai kutokana na kukata ovyo miti umesababisha magonjwa mapya:
- Barani Afrika, sehemu ambapo misitu ya asili imefyekwa kwa ajili ya kilimo na makazi, kumetokea milipuko ya magonjwa kadhaa yakiwemo homa ya manjano na ugonjwa wa malale. Haya ni magonjwa ambayo huenezwa na wadudu ambao hushamiri sana kwenye maji yaliyotuamamaji ambayo yangeweza kunyonywa na ardhi yenye msitu.
- Miti mikubwa mingi ilipokatwa kule Marekani ya Kaskazini, panya waliongezeka sana kwa sababu chakula chao pia kiliongezeka na idadi ya wanyama wanaowawinda ilipungua. Panya hawa walieneza magonjwa kwa watu.
Dawa hutegemea bioanuai
Dawa nyingi hutokana na mimea. Misitu inapokatwa na mito na maeneo oevu kukauka, mimea ya aina nyingi hupotea. Pia, maarifa ya jadi juu ya matumizi ya dawa za mitishamba yatazidi kupotea.
Mlo unaofaa kiafya hutegemea bioanuai
Afya njema hutegemea kula vyakula mbalimbali kama vile matunda, mboga mboga, nafaka na vyakula vya porini vikiwemo samaki na nyama. Tukipoteza bioanuai, tutapoteza pia vyakula vingi ambavyo tunahitaji kwa ajili ya lishe bora. Hatimaye, jamii zinaweza kukabiliwa na matatizo ya kiafya kutokana na lishe duni.
Bioanuai huongeza uzalishaji wa mazao
Mazao yote ya vyakula yakiwemo mpunga, mahindi na ngano kwa miaka mingi yalilimwa kutokana na mimea pori. Mazao haya bado hutegemea kurutubishwa na wadudu, na viumbe hai wengine ili kustawi vizuri zaidi. Kilimo cha mashamba makubwa, ambacho huhusisha matumizi ya mashine kubwa, mbolea na dawa zenye kemikali, hutoa matarajio ya upatikanaji wa mazao mengi. Lakini kemikali hizo huua wadudu na mimea yenye faida, na kuharibu ardhi. Hata kama uzalishaji ukiongezeka, kawaida ni wa aina moja tu ya zao na tena kwa kipindi kifupi. Baada ya miaka kadhaa, kunakuwa na upungufu wa chakula na aina za vyakula halisi ambavyo vinafaa kiafya.
Kwa kutumia njia za kilimo endelevu, mashamba yanaweza kutoa mazao zaidi na athari za wadudu waharibifu kupunguzwa. Njia za kilimo endelevu hulinda wadudu na wanyama wenye faida, hurutubisha ardhi kwa mbolea ya asili, na hulinda ardhi iliyo na miti na mimea mingine. Uzalishaji wa aina nyingi ya mazao husaidia kuboresha lishe na afya bora kwa wote.
Bioanuai hulinda vyanzo vya maji
Uharibifu wa misitu na kilimo cha mashamba makubwa kwa pamoja huchangia kupoteza unyevunyevu kwenye udongo, na kukausha mito wakati wa kiangazi. Mbolea za viwandani na dawa za kuulia wadudu kutoka kwenye mashamba hayo huchafua mito na maziwa.
Bioanuai hulinda jamii
Maisha ya viumbe mbalimbali hutegemea kuwepo maliasili za kutosha. Pale maliasili hizo zinapotoweka, umasikini huongezeka. Katika maeneo ya mashamba, kilimo cha mashamba makubwa huongeza madeni kwa baadhi ya watu na wengine hupoteza ardhi.
Kuhifadhi bioanuai
Katika bioanuai kifo cha kiumbe hai mmoja huathiri viumbe hai vingine wakiwemo watu. Kwa mfano, kutoweka kwa msitu kunaweza kusababisha jamii inayouzunguka kupoteza vyanzo vya chakula, nishati, dawa na pato. Hivyo, kuupanda upya msitu kunaweza kusaidia kuirudishia ardhi uhai wake pamoja na viumbe hai vingine vinavyoitegemea vikiwemo mimea na wanyama, vyenye umuhimu kwa jamii.
Wakulima wanaozingatia kanuni za kilimo endelevu hutumia mfumo wa urutubishaji udongo wa asili kuhakikisha ardhi inabaki yenye rutuba.
Kufanya kazi kwa kuheshimu asili ya dunia
Katika asili ya dunia, kila kitu kina matumizi na kusudi lake. Njia moja wapo ambapo rasilimali inaweza kutumika bila kuacha mabaki yasiyo na faida ni kuzingatia miduara asilia ya uendelevu.
Kwa bahati mbaya miduara asilia ya uendelevu imevurugwa na watu pamoja na viwanda, na hii imesababisha madhara makubwa kwa afya ya mazingira. Mfano mmoja wa madhara hayo ni kuongezeka kwa joto duniani.
Wahamasishaji wa afya ya mazingira nchini Ufilipino wana usemi:
Kwa kuelewa umuhimu wa usemi huu, tunaweza kujifunza kutokana na asili ya dunia na kulinda maliasili na afya zetu. Mifumo ya uendelevu tunayojenga katika nyumba zetu, jamii zetu na hata viwandani ni mifano michache ya hatua ambazo tunaweza kuchukua kuboresha afya ya mazingira. Kwa mfano, kutengeneza mboji na kurejeshea thamani chupa na makopo yaliyokwisha kutumika ni baadhi ya njia za kutii miduara asilia ya uendelevu badala ya kutegemea dampo la taka.
Wahamasishaji wa afya ya mazingira nchini Ufilipino wana usemi mwingine:
Viwanda husababisha kiwango kikubwa sana cha uchafuzi wa mazingira kupitia hewa yenye sumu au mabaki ya kemikali zinazoathiri afya. Hivyo viwanda pia vinaweza kujifunza kutokana na miduara asilia ya uendelevu inayolinda mazingira kwa kutumia tena nishati, vifaa na mabaki mengine na kuzingatia mchakato wa uzalishaji usiochafua mazingira.
Hatua ya kwanza ni wenye viwanda kuchukua taka zote wanazozalisha. Iwapo taka, mfano taka za kemikali zenye sumu haziwezi kurudishwa viwandani na kutumika tena, viwanda vinapaswa kuziondoa kwenye mazingira kwa usalama, kupunguza matumizi yake, na hatimaye kuacha kuzitumia kabisa. Kama kiwanda kina dhamira ya kufanya biashara endelevu, hakina budi kuchukua tahadhari na kuzuia uchafuzi wa mazingira. Pia kiwanda hakina budi kuzingatia haki ya afya kwa wote, na siyo kupata faida tu pasipo kujali hatari, kutupa taka hovyo, na kuchangia kueneza magonjwa.
Kwa kutumia rasilimali chache na kurejeshea thamani vifaa vilivyokwisha kutumika, viwanda vinaweza kupunguza madhara yake kwa afya ya mazingira yetu. |
Kuzuia madhara kutokana na uchafuzi
Madhara ya uchafuzi wa mazingira kwa binadamu hutokana na kukithiri kwa sumu au bidhaa zenye sumu kutokana na shughuli za watu, hasa taka kutoka viwandani, usafirishaji na kilimo. Uchafuzi kwa njia ya sumu au kemikali huenea katika mazingira yetu kupitia hewa, maji na ardhi.
Uchafuzi mkubwa zaidi hutokana na vitu vya kawaida ambavyo tunatumia na vilivyopo karibu nasi katika maisha yetu ya kila siku. Njia kuu za hatari ya uchafuzi kwa watu zinazohusisha sumu ni pamoja na:
- Moshi kutokana na moto: huwa tunavuta moshi wenye sumu hususan wakati wa uchomaji wa vitu vya plastiki. Vile vile majivu yenye sumu huchafua vyanzo vyetu vya maji ya kunywa na mashambani tunapolima mazao.
- Moshi kutoka viwandani: huchafua hewa, maji na ardhi.
- Kemikali: hasa zinazotumika viwandani, kwenye migodi na wakati wa uchimbaji na usafishaji wa mafuta. Mara nyingi kemikali hizi hutupwa kwenye vyanzo vya maji, na pia kuchafua hewa na ardhi.
- Viuatilifu: kawaida hutumika na kuhifadhiwa karibu na vyakula, vyanzo vya maji na nyumbani. Vinapopulizwa, husafiri mbali kupitia hewa na kusababisha madhara makubwa.
- Kemikali: mfano zilizomo ndani ya betri, rangi za nyumba, rangi za viwandani kwa ajili ya kutengeneza nguo na bidhaa zingine, na pia kemikali ambazo hutumika katika utengenezaji wa vifaa vya elektroniki. Kemikali hizo husababisha madhara ya kiafya kwa watu wanaovitengeneza na wanaovitumia.
- Moshi wa magari: moshi wa magari huchafua hewa, maji na ardhi.
Uchafuzi unaoeneza sumu katika mazingira, husababisha madhara ya kiafya kwa watu, mimea na wanyama, siyo tu pale uchafuzi unapofanyika lakini pia mbali na chanzo chenyewe. Kujilinda dhidi ya madhara ya uchafuzi na vitu vyenye sumu ni sehemu muhimu ya uendelevu wa maisha na mazingira yetu.
Soma “Pigania mabadiliko” na “Taka za kawaida zenye”.
Chukua tahadhari daima
Katika harakati zao za kutafiti bidhaa mpya na faida zaidi, kampuni kubwa zimetengeneza maelfu ya kemikali mpya ambazo hazikuwahi kuwepo duniani. Usalama wa idadi kubwa ya kemikali hizi haujathibitishwa. Lakini zimeendelea kutumika kutengenezea bidhaa ambazo tunauziwa kila siku. Hata pale watu wanapohofu baadhi ya bidhaa hizi kwa afya zao, pasipo uthibitisho wa kitaalam, bidhaa husika huendelea kuuzwa na kutumika.
Baadhi ya viongozi wa jamii na wanasayansi husisitiza kanuni ya kuchukua tahadhari katika kufanya maamuzi. Kanuni hii inaeleza kuwa: “kama kuna sababu ya kuamini kuwa kitu fulani kinaweza kusababisha madhara, hata kama hatujui kwa uhakika, basi bora kuepuka kitu au bidhaa hiyo kuliko kubahatisha”.
Hata hivyo, nchi nyingi zinafanya kinyume na ujumbe huu. Msimamo wa nchi nyingi ni kwamba lazima madhara yathibitishwe kwanza kabla kitu au bidhaa haijapigwa marufuku. Mtazamo huu ni sawa na dhana ya ‘Watu Wafe Kwanza’.Principle.
Kuongezeka kwa joto duniani
Dunia nzima, mfumo wa viumbe hai au bioanuai inaharibiwa. Ufyekaji misitu, ongezeko la uchafuzi wa maji na hewa yetu, upotevu wa wanyama pori na urithi mwingine ni mifano ambayo inaonekana wazi. Kisichoonekana wazi ni ongezeko la joto duniani linalosababishwa na uchafuzi wa mazingira.
Tatizo la kuongezeka kwa joto duniani linabadili tabia ya nchi katika sehemu nyingi duniani. Kile kinachoonekana kama ongezeko dogo la hali ya joto kinasababisha mabadiliko makubwa. Baadhi ya maeneo yanakumbwa na vimbunga na mafuriko mabaya, wakati sehemu zingine zinapata mvua kidogo na hata vipindi virefu vya ukame. Mabadiliko ya tabia nchi kutokana na ongezeko la joto duniani yanasababisha maafa makubwa dunia nzima, mwaka hadi mwaka, na kuchochea matatizo makubwa ya kiafya kwa watu.
Miongoni mwa athari hizo:
- Mafuriko, vimbunga na ukame vinasababisha uzalishaji mazao kushuka, njaa, uharibifu wa makazi, watu kuhama, majeraha na hata vifo kwa mifugo na watu.
- Magonjwa yanaongezeka au kusambaa kwa sababu mabadiliko ya hali ya hewa yanachochea ongezeko la wadudu na wanyama wasambazao magonjwa na kuwafanya kuenea katika maeneo mapya.
- Kuongezeka kwa kiwango cha nyuzi joto ambacho wakati mwingine pia husababisha magonjwa na vifo kuongezeka.
Sababu za msingi za kuongezeka kwa joto duniani
Mazingira ya dunia yana uwezo wa asili wa kuhimili uchafuzi. Lakini uchafuzi ukizidi sana mazingira ya dunia hayawezi kuhimili. Zaidi ya miaka 100 iliyopita, wakati watu walipoanza kuchimba na kutumia kiwango kikubwa cha nishati yenye asili ya mafuta ya kawaida na mkaa wa mawe, kiwango cha uchafuzi wa mazingira kutokana na moshi wa ukaa kimeongezeka mara dufu. Hiki ni chanzo cha msingi kimojawapo cha kuongezeka kwa joto duniani. Pia baadhi ya kemikali zilizogunduliwa kwa ajili ya matumizi viwandani, huchafua hewa na haziwezi kufyonzwa na mazingira. Kemikali hizo pia huchangia ongezeko la joto duniani.
Sababu nyingine ya msingi ya kuongezeka kwa joto duniani ni matumizi ya rasilimali yasiyozingatia haki, usawa na uendelevu. Nchi tajiri kama Marekani, katika jitihada za kupata faida kubwa na maisha bora zaidi, zilianza kuongeza joto duniani kwa kutumia rasilimali nyingi kupita kiasi na kusababisha uchafuzi mkubwa wa mazingira.
Iwapo nchi zinazoendelea nazo zitafuata njia zisizoendelevu katika jitihada za kujipatia maendeleo, uchafuzi wa mazingira utakithiri na kuielemea kabisa dunia. Ili kuzuia maafa yanayosababishwa na ongezeko la joto duniani, kama yalivyoelezwa hapo juu na mengine mabaya zaidi ambayo yataendelea kutokea, nchi zinazoendelea na zile zilizoendelea kwa pamoja hazina budi kuzingatia matumizi endelevu ya rasilimali. Tunahitaji hasa kuacha kutegemea nishati zinazotoa hewa chafu ya ukaa na kuanza kutumia nishati safi na salama zaidi. Nishati hizo ni pamoja na nishati zinazotokana na jua, upepo, maji na taka zinazoweza kuvundishwa na bakteria (biogas)