Hesperian Health Guides

Sehemu ya pili: Taka za kawaida zenye sumu

HealthWiki > Mwongozo wa jamii juu ya afya ya mazingira > Sehemu ya pili: Taka za kawaida zenye sumu

Katika sura hii:

Sw EHB Ch18 Page 409-2-a.png

Taka za kawaida zenye sumu ni taka ambazo zina kemikali zenye madhara makubwa kwa afya ya watu na mazingira. Kwa asili yake, taka hizi zinaweza kusababisha mlipuko, kubabua (mfano tindikali na dawa za uyeyushaji), kudhuru, kuachia sumu, kuwasha au kusababisha harara, kuwaka moto au kwa ujumla kuhatarisha mazingira.

Baada ya kusoma sehemu hii, utakuwa umejifunza:
  1. Maana ya taka za kawaida zenye sumu.
  2. Njia mbalimbali za kushughulikia taka za kawaida zenye sumu.


Taka za kawaida zenye sumu ni pamoja na rangi za nyumba na makopo yake; mafuta ya mitambo au gari yaliyotumika; betri za aina yoyote mfano za gari, redio na simu; dawa za kuua wadudu; taa (balbu) za umeme zilizotumika; mbolea za viwandani; mabaki ya viyoyozi na friji hasa zile ambazo zinatumia gesi chafu inayoharibu utando wa ozone; televisheni na kompyuta; baadhi ya taka za plastiki na taka za hospitali. Taka za sumu zingine ni sumu za kawaida, tindikali, na dawa za kufanyia usafi nyumbani.

Njia bora zaidi ya kuzuia madhara kutokana na taka zenye sumu ni kuzuia uzalishaji wake. Serikali zinapaswa kupiga marufuku bidhaa zenye sumu na uzalishaji wake, na kuhimiza uzalishaji wa bidhaa mbadala. Jamii zinaweza kuhimiza matumizi ya bidhaa za nyumbani mbadala kuliko kuendelea kutumia bidhaa zenye sumu. Vilevile vyama vya wafanyakazi vinaweza kuhimiza uzalishaji wa bidhaa mbadala viwandani kuliko kuendelea kuzalisha bidhaa zenye sumu. Kuanzisha vituo vya kukusanya taka zenye sumu mahali panapofikiwa kwa urahisi kunaweza kusaidia kuzuia uchafuzi wa ardhi na vyanzo vya maji.

A man and child drink from a barrel on which the word "Pesticide" is crossed out and "Drinking water" is written.
A man destroys the barrel with a pickaxe.
Destroy toxic materials containers so they cannot be used to store other things, especially food or water.

Njia za kushughulikia na kuondoa taka zenye sumu kwa usalama

Kwa sababu ni vigumu na ghali kuzishughulikia taka zenye sumu kwa usalama, ni bora zaidi serikali kuhakikisha utekelezaji wa miongozo kuhusu matumizi, hifadhi na uondoaji wa taka zenye sumu. Hii inapaswa kujumuisha utoaji elimu na mafunzo kwa wanajamii ili waweze kuzishughulikia taka zenye sumu kwa usalama. Yafuatayo ni maelekezo ya jumla katika ushughulikiaji wa taka zenye sumu:

  • Hifadhi bidhaa zenye sumu mbali na maji na chakula, na pia mahali ambapo watoto hawawezi kuzifikia.
  • Hifadhi bidhaa zenye sumu kwenye vyombo vyake vya awali na usibandue karatasi za maelezo zilizobandikwa. Hii itasaidia vyombo visitumike kwa ajili ya maji au kuhifadhia chakula.
  • Hifadhi taka zenye sumu mbali na taka nyingine za nyumbani.
  • Usichome moto taka zenye sumu. Uchomaji husambaza kemikali ya sumu kupitia majivu na moshi, na wakati mwingine huweza kutengeneza kemikali yenye sumu hatari zaidi.
  • Usitupe bidhaa zenye sumu kwenye vyoo vya shimo au vyoo vya maji, karo, njia na mifereji ya maji au hata juu ya ardhi.


Tafuta ushauri kwa maafisa afya na vituo vya usimamizi wa rasilimali taka kujua njia bora zaidi za kuondoa taka zenye sumu katika eneo lako.

Jinsi ya kuzishughulikia taka zenye sumu za kawaida

Bidhaa za kawaida za nyumbani hutengeneza taka zenye madhara iwapo hazitashughulikiwa kwa uangalifu na kuondolewa kwa usalama.

Rangi na makopo ya rangi

Hifadhi makopo ya rangi yaliyofunikwa sehemu yenye ubaridi. Mara rangi yote inapotumika, bonda makopo yote ya rangi, funga ndani ya gazeti, weka kwenye mifuko ya plastiki, halafu fukia kwenye shimo salama la kuhifadhi taka. Rangi zenye asili ya ulimbo (latex) zina madhara kidogo ukilinganisha na rangi zingine, lakini zinapaswa kushughulikiwa kwa utaratibu ule ule.

Dawa za uyeyushaji (mfano kwa ajili ya kusafisha grisi na rangi, pamoja na mafuta ya kuyeyushia na kuchanganya rangi)

Hifadhi dawa za uyeyushaji kwenye makopo yaliyofunikwa sehemu zenye ubaridi, ili isiweze kusababisha moto. Mara dawa yote inapotumika, toboa makopo yote ili yasiweze kutumika tena. Bonda makopo na kufunga ndani ya gazeti, halafu weka kwenye mfuko wa plastiki na hatimaye fukia au tupa kwenye shimo salama la kuhifadhi taka.

Mafuta ya gari yaliyotumika

Kamwe usimwage mafuta kwenye ardhi au kwenye njia za maji. Hifadhi kwenye vyombo vilivyofunikwa. Mafuta yaliyotumika mara nyingine huweza kurejeshewa thamani kwenye vituo au karakana za kukarabati mitambo. Mafuta ya gari yaliyotumika yanaweza pia kupakwa kwenye mbao au nguzo katika kazi za ujenzi kuzuia zisioze haraka au kuliwa na wadudu. Pia mafuta hayo yanaweza kutumika tena katika baadhi ya mitambo.

Betri

Baadhi ya betri zinaweza kurejeshewa thamani. Lakini urejesheaji betri thamani kwa mkono ni hatari na usifanywe bila mafunzo ya kutosha na vifaa vya kujikinga.

Dawa za kuulia wadudu

Toboa matundu au haribu kabisa vyombo vya kuwekea dawa za kuulia wadudu ili visiweze kutumika tena. Vifukiwe katika mashimo salama ya taka.

Taka kutokana na huduma za afya

Taka za huduma za afya zinajumuisha taka ambazo huzalishwa hospitali, zahanati, na vituo vya kutolea huduma za afya- maabara, benki za damu salama, kliniki za magonjwa ya meno, vituo vya kujifungulia, na hospitali za wanyama. Pia zinajumuisha taka zinazozalishwa na programu za chanjo, misafara maalum ya tiba kwa jamii, na huduma kwa wagonjwa nyumbani.Taka hizi ni pamoja na bendaji zenye damu damu, mipira ya kuvaa mikononi iliyotumika, sindano chafu, vifaa vingine vyenye ncha kali, na dawa zilizotupwa.

Usimamizi wa taka za huduma za afya, kimsingi, hutumia taratibu za kawaida za usimamizi wa taka. Hata hivyo, taka ambazo zimechafuliwa na majimaji ya mwilini na vijidudu vya magonjwa lazima zitibiwe kwanza na dawa maalum za kuua vijidudu, na kuondolewa kwa kuzingatia miongozo ya Wizara ya Afya, ili kulinda afya ya watu na mazingira.


Ukurasa huu ulihuishwa: 05 Jan 2024