Hesperian Health Guides

Taka na sheria

Katika sura hii:

Serikali nyingi zina sera na miongozo ya kusimamia taka. Moja wapo ya malengo ya juhudi za jamii ni kuhakikisha kuwa sera hizo zinalinda afya za watu na mazingira. Lengo lingine ni kubadilisha sera hizo iwapo hazikidhi haja.

Wafilipino wapiga marufuku uchomaji taka na waimarisha sheria za taka

Kwa miaka mingi, taka nchini Ufilipino zilikuwa zikirundikana katika sehemu za wazi au kuchomwa moto. Lakini uchafuzi wa hewa ulipoongezeka, kutokana na taka zaidi na zaidi, jamii nyingi zilianza kuishinikiza serikali:

  • kupiga marufuku uchomaji taka,
  • kuanzisha programu za kurejeshea taka thamani, na
  • kuzuia utupaji taka maeneo ya wazi.


Kampeni ilianza mwaka 1985 na uelimishaji jamii. Wanaharakati walisafiri nchi nzima wakielimisha jamii kuhusu njia bora za kupunguza uzalishaji wa taka. Waliwaonyesha watu namna ya kupunguza taka na jinsi ya kutenganisha taka kwa ajili ya kutengeneza mboji, kurejeshea thamani au kutumiwa tena. Walialika watu kutoka nyanja zote za maisha wakiwemo wakulima, wanasiasa na viongozi wa dini, kufanya kazi pamoja ili kupunguza taka katika jamii zao.


Wakati huo huo, walielimisha jamii na viongozi wa serikali kuhusu uchafuzi kwa njia ya sumu kutokana na uchomaji taka. Wanakampeni walionyesha jinsi sumu kutokana na uchomaji taka inavyoishia kwenye mayai na vyakula vingine vya kawaida.

Shinikizo lao kwa serikali lilizaa matunda pale ambapo uchomaji taka ulipigwa marufuku mwaka 1999 kwa kupitishwa sheria mpya inayoitwa Sheria ya Usalama wa Hewa, 1999. Mwaka 2000 serikali ilianzisha programu ya urejesheaji taka thamani na pia kupitisha sheria ya kugeuza dampo zote za wazi kuwa mashimo salama ya kuhifadhi taka. Mwaka 2001 serikali ilipitisha Sheria ya Usimamizi Ekolojia wa Taka. Chini ya sheria hii, vituo vya usimamizi wa rasilimali taka vilianzishwa katika miji na majiji. Wanaharati wanaendelea kufanyakazi kuhakikisha kuwa sheria hizi zinawanufaisha wale wanaoathiriwa zaidi: wazoaji taka, wachambuaji taka na wanaofanya kazi ya urejesheaji taka thamani.


Sheria kama hizi ni muhimu katika kuweka kiwango cha jinsi taka zinafaa kushughulikiwa. Watu wanapochukua wajibu juu ya taka zao, na kuwashinikiza watunga sheria (wabunge, madiwani, na wajumbe wa serikali za vijiji na mitaa) kuweka sheria zinazokidhi na kuzisimamia kwa haki na ukamilifu, kila mtu hunufaika.

Smoke from burning waste covers a town and city.



Ukurasa huu ulihuishwa: 04 Juni 2022