Hesperian Health Guides

Sehemu ya kwanza: Kubadili hatari ya kiafya kuwa fursa

HealthWiki > Mwongozo wa jamii juu ya afya ya mazingira > Sehemu ya kwanza: Kubadili hatari ya kiafya kuwa fursa

Katika sura hii:

People interact while using a resource recovery center.

Baada ya kusoma sehemu ya kwanza, utakuwa umejifunza:
  1. Madhara ya kukosa usimamizi bora wa taka ngumu.
  2. Jinsi ya kuanzisha mpango wa jamii wa usimamizi wa taka ngumu.
  3. Hatua na fursa muhimu katika usimamizi bora wa taka ngumu.


Taka ngumu kawaida huitwa majina mengi-takataka, uchafu, masalia, mabaki na majina mengine. Taka ngumu hazipaswi kusababisha matatizo ya kiafya. Zinaweza hata kuwa chanzo cha pato na rasilimali za kutengenezea bidhaa mpya. Lakini pale ambapo taka ngumu hazikusanywi ipasavyo, kutenganishwa, kutumika tena, kurejeshewa thamani au kuangamizwa kwa usalama, huweza kusababisha kichefuchefu, kutoa harufu mbaya, na kusababisha matatizo makubwa ya kiafya.

Watu wengi huwa tuna tabia ya kutupa taka hovyo kwa kudhani kwamba yupo mtu ambaye atashughulikia taka hizo. Mara nyingi ni watu maskini sana ambao hulazimika kuishi katika mazingira yenye uchafu unaozalishwa na watu wengine katika jamii, na wakati mwingine huutegemea uchafu huo kwa ajili ya riziki yao. Ni watu hao maskini ambao hufanya kazi ya kuzoa, kuchambua, kusafisha na kuzirejeshea thamani baadhi ya taka hizo ili ziweze kutumika tena. Ingawa kila mtu anakubali kuwa hii ni kazi muhimu ambayo inapaswa kufanyika ili kulinda afya zetu na mazingira, mara chache watu wanaofanya kazi hii hulipwa vizuri na hata kuheshimiwa.

Ili kusimamia taka kwa lengo la kulinda maisha ya watu na mazingira, tunatakiwa kupunguza kiasi cha taka tunazozalisha na kuzirejeshea thamani zile taka ambazo zinaweza kuwa rasilimali. Kila mtu, hasa viwanda na serikali, lazima wawajibike juu ya taka wanazozalisha, na awali kabisa wadhibiti uzalishaji taka.

Jinsi Jasiri alivyoboresha afya yake na kujipatia heshima

Kila siku Jasiri alikuwa akizunguka mjini akikusanya takataka. Kwa sababu siyo kila nyumba huzalisha taka ambazo aliona zinafaa, alitumia muda wake mwingi kutembea huku na kule akiwa amebeba viroba vizito.


Kila usiku Jasiri alichambua taka hizo ili aziuze asubuhi yake. Baadhi ya wateja walinunua glasi, wengine vyuma-chakavu na wengine karatasi. Lakini taka ambazo hazikuweza kununuliwa ziliendelea kurundikana nyumbani kwa Jasiri. Uwanja wake ukavurugika, na kugeuka kuwa dampo hatari la taka; lakini hakukuwa na sehemu yoyote ya Jasiri kuhamishia taka hizo. Mara nyingine alikuwa akipata maambukizo ya magonjwa ambayo yalichukua miezi kupona na kumfanya ashindwe kufanya kazi. Mara kwa mara, pia alikuwa akipata homa kali kutokana na malaria kwa sababu mbu walizaliana kwenye matairi yaliyokuwa uwanjani kwake. Vilevile, pamoja na juhudi zake, polisi mara nyingi walimsumbua pale walipomkuta akichambua taka ndani ya mapipa ya taka mbele ya maduka au mitaani.


A man sorts through trash.

Jasiri na waokotaji taka wengine waliamua kuanzisha kituo ili kuwasaidia kuuza kile walichokusanya; na kupata manufaa mengine kwa kubadilishana maarifa, vifaa na habari. Walitembelea taasisi moja ambayo inashughulikia masuala ya mazingira na haki za wafanyakazi, na pamoja wakapata wazo la kuanzisha mradi kamilifu wa urejesheaji taka thamani.


Watu kutoka taasisi moja ya mazingira waliomba Halmashauri ya mji kusaidia mradi huo wa urejesheaji thamani taka na kuwaagiza polisi na wenye maduka kuwathamini na kuwatendea vyema zaidi waokotaji taka. Halmashauri ilikubali na kituo kikaanzishwa mahali ambapo Jasiri na wenzake wangeweza kuchambua taka walizokusanya. Kila mwokotaji taka alipewa mkokoteni ili kumrahisishia kukusanya taka na kuzileta kwenye kituo kwa ajili ya uchambuzi, au kuwapelekea moja kwa moja wanunuzi wa vitu vilivyotumika.


Kituo cha urejesheaji thamani taka kilitoa mipira ya kuvaa mikononi na mabuti ili kujikinga dhidi ya vitu vyenye ncha kali na vingine ambavyo vilikuwa vimechafuliwa. Watu kutoka kwenye taasisi ya mazingira walipofahamu kuwa Jasiri alikuwa anaumwa malaria, walimsaidia kupata tiba kwenye kituo cha afya.


Jasiri bado anafanya kazi ya kukusanya taka kwa bidii lakini afya yake imekuwa bora zaidi na nyumba yake haionekani tena kama dampo. Polisi na wenye duka humpa yeye, pamoja na wazoa taka wengine, heshima wanayostahili kwa kutunza mazingira ya jamii . Na hata mji unajivunia kituo hicho cha urejesheaji thamani taka ambacho kinasaidia kuuweka mji katika hali ya usafi zaidi na kutoa ajira.


Ukurasa huu ulihuishwa: 05 Jan 2024