Hesperian Health Guides

Matembezi ya kiutafiti katika jamii kujua hali ya taka

Katika sura hii:

Matembezi ya kiutafiti kijijini au mtaani kujua hali ya taka katika jamii ni fursa kwa watu kuona na kujadili matatizo yanayohusiana na taka. Watu wanaweza kutoa maoni yao kuhusu hali ya taka na matarajio yao ya kuwa na jamii iliyo safi na afya bora zaidi. Wakati na baada ya matembezi, kundi hilo linaweza kujadili hatua ambazo zinaweza kuchukuliwa kuimarisha usafi ndani ya jamii, na kutumia vizuri taka kwa kuzirejeshea thamani.


Kuandaa matembezi ya kiutafiti kujua hali ya taka katika jamii

  1. Alika watu kushiriki katika matembezi ya kiutafiti kuona hali halisi ya taka.

    Ili matembezi hayo yaweze kufanikiwa, shirikisha majirani, watu wanaoshughulika na taka, na wale wenye madaraka ya kubadili namna taka zinavyokusanywa, kusafirishwa na kusimamiwa. Shirikisha:

    • Wafanyakazi katika viwanda vidogo vidogo.
    • Wanaoshughulika na vifaa vilivyotumika na wasafirishaji wa taka.
    • Wanunuzi wa vitu vilivyotumika kutoka kwenye nyumba za watu na sehemu za biashara.
    • Wakusanyaji taka wanaopata riziki kutokana na vitu wanavyokusanya kutoka mitaani au kwenye dampo.
    • Maofisa wa serikali ambao wanaweza kusaidia juhudi za usafi katika jamii.
  2. Andaa mkutano kabla ya matembezi

    Ni muhimu kufanya mkutano ili kuzungumzia sababu za kufanya matembezi hayo, nini cha kuangalia wakati wa matembezi hayo, na nini kila mtu anatarajia kufanikisha kwa kushiriki katika matembezi hayo ya kiutafiti. Pia ni muhimu kufahamu nini kinachomtia moyo kila mmoja wao kushiriki. Baadhi ya watu wanaweza kuwa wanapata riziki kwa kukusanya rasilimali ambazo wengine hutupa. Wengine wanaweza kuwa wanataka kuboresha afya na mandhari ya jamii yao.

  3. People talk as they gather outside a small store.
    Miaka thelathini iliyopita tulikuwa tukilima chakula chetu chote. Hivi sasa, tunanunua sehemu kubwa sokoni na dukani.
    Kila tunachonunua hufungashwa katika mifuko ya plastiki ambayo hutupwa mitaani.
    Hivi sasa taka za plastiki zimetapakaa. mitaani.
  4. Panga matembezi yenu

    Amua wapi matembezi yatafanyika na kwa pamoja andaa orodha ya vitu ambavyo vinapaswa kuangaliwa, kama vile:

    • Mahali ambapo taka zimeziba mitaro na njia zingine za maji, mitaa au barabara.
    • Vinyesi vya binadamu na wanyama mitaani na kwenye njia za maji.
    • Taka zenye sumu.
    • Wanyama wanaokula kwenye marundo ya taka.


    Waombe wazee kwenye jamii hiyo kueleza hali ilivyokuwa miaka 20 au 30 iliyopita. Je, kulikuwa na aina tofauti za taka kama ilivyo sasa? Watu walishughulikiaje taka zao kipindi hicho? Fikiria jambo hili wakati wa matembezi.

  5. Sasa anza matembezi!

    Jigawe katika makundi yatakayotembelea sehemu mbalimbali za jamii. Kwa sababu makundi tofauti yatagundua matatizo tofauti, unaweza kuunda kikundi cha wanaume pekee au wanawake peke, au kikundi cha vijana kutembea peke yao bila kuwa na watu wazima. Au vikundi vyote vinaweza kuwa mchanganyiko.

    Angalia mahali taka zinakusanywa na njia za kawaida za uondoaji taka hizo. Je, yapo mapipa ya taka kwa ajili ya umma? Je, watu huchoma taka au hutupa kwenye maeneo ya wazi? Huzipeleka kwenye eneo maalum lililoandaliwa au katika tanuri maalum la kuteketeza taka? Je baadhi ya taka hukusanywa na kutumika tena au kurejeshewa thamani, kama vile chupa za glasi au magazeti? Vipi kuhusu taka kutokana na biashara?

    Kila kikundi kiwe na mtu wa kuorodhesha au kuchora matatizo waliyoyaona wakati wa matembezi, pamoja na aina za taka ambazo zitaonekana.
  6. Health workers talk with 2 women on their doorstep, beside their buckets of trash.


  7. Angalia taka katika kaya za watu. Ni kiasi gani na aina zipi?

    Kama sehemu ya matembezi, nenda kwenye kaya za baadhi ya watu waliojitolea kushiriki katika matembezi kuona kuna aina gani za taka na rasilimali gani. Chukua chombo cha taka kilichojaa na kumwaga taka zote chini. Tenganisha taka hizo katika marundo 5:

    • Mabaki ya vyakula na taka zingine zinazooza mbichimbichi.
    • Plastiki.
    • Karatasi.
    • Vyuma, na
    • Taka zingine.


    Ni rundo gani lililo kubwa zaidi na ni lipi dogo zaidi? Huwa taka katika kila rundo zinashughulikiwaje? Nini kinaweza kufanyika badala ya kuzitupa kama uchafu? Chukua baadhi ya taka kutoka katika kaya kadhaa kwenye majadiliano ya kikundi ambayo yanafuata.

    Kumbuka kurudisha taka zilizobaki katika pipa la taka.


  8. Rudi katika kundi kubwa kujadili watu walichokiona

    Baadaye siku hiyo, au siku inayofuata, wezesha makundi yote kukaa pamoja kujadili walichojifunza.

    Omba kila mmoja kuwashirikisha wenzake alichokiona wakati wa matembezi. Kila mmoja aonyeshe kipande cha taka ya nyumbani na kueleza iwapo ameona aina hiyo ya taka mahali pengine katika jamii ikizagaa, ikitumika tena au kurejeshewa thamani. Je washiriki wameona uwezekano wa matatizo au matatizo halisi ya kiafya yanayosababishwa na uondoaji taka kwa njia zisizo salama? Ni mawazo gani yaliyo bora zaidi kuhusu uondoaji taka ambao baadhi ya familia zilikuwa zikitumia?
  9. Orodhesha sababu za matatizo na athari zake

    Women talk as they look at a chalkboard labelled "Trash Walk. Causes: no composting. Burning trash. Lots of bottles and cans. Problems: bad smells and smoke. Trash piles. Health effects: coughing. Children sicker with asthma. Polluted water.
    Siku hizi, wafanyabiashara wakubwa na wadogo, maduka ya kawaida na maduka makubwa hufunga kila bidhaa wanazouza kwenye mifuko ya plastiki. Nao waorodheshwe kama mojawapo ya ‘sababu’ za matatizo ya taka ngumu.
    Mwezeshaji anaweza kuandika ubaoni au kwenye karatasi kubwa matatizo yaliyoibuliwa na jamii. Omba kila mmoja kufikiria sababu za matatizo ya taka ngumu katika jamii na orodhesha kwenye jedwali ambayo inaonyesha matatizo na sababu zake. Halafu uliza namna kila tatizo linavyoathiri afya ya jamii. Andika au chora safu nyingine kwenye jedwali ambayo inaonyesha athari za kiafya za kila tatizo.

  10. Panga hatua zinazofuata

    Wezesha kundi kupitia matatizo yaliyoorodheshwa na kufikiria njia za ufumbuzi. Hatua zinazofuata zinaweza kuanza na njia za kupunguza athari za kiafya kutokana na tatizo husika, au kujaribu kuliondoa tatizo kabisa. Uliza maswali kama vile:

    • Kila nyumba inawezaje kupunguza kiasi cha taka inazozalisha?
    • Tunawezaje kuendeleza utaratibu wa utengenezaji mboji kutokana na taka na utenganishaji wa taka?
    • Je kinaweza kuanzishwa kikundi cha jamii au biashara kwa ajili ya kukusanya na kutumia tena taka?
    • Je linaweza kupatikana eneo kwa ajili ya kujenga mtambo wa kutengeneza mboji, au kujenga kituo cha kuchambua na kuainisha taka kwa ajili ya urejeshaji thamani?
    • Mtambo wa karibu zaidi wa urejesheaji taka thamani uko wapi?
    • Je serikali za mitaa, vijiji au halmashauri, viongozi wa jamii, viwanda na biashara wanaweza kuwajibika, kila mmoja, namna gani katika kutatua matatizo yanayosababishwa na taka?

Jamii yajipatia riziki kutokana na biashara ya taka

Vitongoji vyeye nyumba nyingi za mabanda katika jiji la Curitiba, nchini Brazili vilikuwa na mashimo mengi ya wazi ya kutupa taka. Mashimo hayo yalikuwa mazalia ya wanyama wadogo na wadudu wanaobeba magonjwa. Ili kukabili tatizo hili, Halmashauri ya jiji la Curitiba ilianzisha mpango ulioitwa, ‘Usitupe Taka Zako – Tutazinunua’, kwa kifupi UTAZATU. Halmashauri ya jiji la Curitiba ilitafakari gharama ya kusafisha madampo yote ya taka. Halafu, badala ya kuajiri mkandarasi, walitafakari gharama ya ukusanyaji wa gunia moja la taka, na hatimaye kuamua kutoa kiasi hicho kwa wakazi wa mji huo kuifanya kazi hiyo.

People bring their trash to a municipal collection truck.

Mbali na kujipatia fedha kutokana na taka walizokusanya, kila mtu alipewa tiketi ya kusafiri bila malipo kwenye vyombo vya umma kwa kila gunia la taka alilopeleka kwenye gari la manispaa la ukusanyaji taka. Kwa sababu makazi yao yako mbali na kitovu cha jiji, tiketi hizi za usafiri bila malipo zilithaminiwa sana. Jiji pia lilitoa fedha ya hamasa, kwa kila mfuko wa taka uliokusanywa, ili kuboresha bustani kwenye maeneo ya umma na miradi mingine ya kijamii. Maeneo ambayo wakati fulani yalikuwa yamejaa taka yalibadilika na kuwa bustani za mjini au viwanja vya umma vikiwa na miti. Afya ya jamii iliimarika.


Wahamiaji jijini wasio na ajira, watu wenye ulemavu au wengine waliohitaji ajira walipatiwa kazi katika kituo cha kuchambua na kutenganisha taka. Mabaki ya vyakula na taka za shambani yalitumika kutengeneza mboji kwa ajili ya matumizi katika viwanja na bustani za jiji, na mashamba na bustani za wakazi. Mabaki ya plastiki na vyuma yaliuzwa kwenye viwanda vya karibu. Sponji za plastiki zilicharangwa na kutumika kama ujazo katika utengenezaji wa blangeti za kujifunikia.


Miaka michache baada ya mpango huo kuanza, jiji liliuimarisha zaidi. Walianza kununua vyakula moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji karibu na jiji kwa bei nafuu, na kuwapatia watu mfuko wa chakula kizuri kutoka shambani kwa kila gunia la uchafu walilokusanya. Mkakati huu ulisaidia wakulima katika vitongoji vya jiji kuuza mazao yao, lishe ya familia katika vitongoji pembezoni kuboreka, na usafishaji wa jiji.



Ukurasa huu ulihuishwa: 04 Juni 2022