Hesperian Health Guides
Mpango wa jamii wa usimamizi wa taka ngumu
HealthWiki > Mwongozo wa jamii juu ya afya ya mazingira > Sehemu ya kwanza: Kubadili hatari ya kiafya kuwa fursa > Mpango wa jamii wa usimamizi wa taka ngumu
Mara jamii inapokuwa na ufahamu wa pamoja kuhusu matatizo yanayosababishwa na taka, inaweza kuchukua hatua kutatua matatizo hayo; ikianza na miradi ambayo inakidhi vizuri zaidi mahitaji na uwezo wa jamii husika.
Mpango kamilifu wa jamii wa taka ngumu ungetarajiwa kujumuisha hatua zote zifuatazo:
- Upunguzaji wa taka zinazozalishwa, hasa taka za sumu na taka ambazo haziwezi kurejeshewa thamani.
- Utenganishaji taka mahali zinapozalishwa ili kufanya kazi ya kuzishughulikia iwe rahisi na salama zaidi.
- Utengenezaji mboji kwa kutumia mabaki ya vyakula na taka zingine zenye asili ya kuoza.
- Kutumia tena vitu na vifaa kadri inapowezekana.
- Urejesheaji thamani wa vitu mbalimbali na ushawishi kwa serikali na wamiliki wa viwanda kuanzisha mipango ya jamii ya urejesheaji thamani taka.
- Ukusanyaji, usafirishaji na utunzaji wa taka kwa usalama. Heshimu watu wanaofanya kazi hii na kuwalipa ujira unaostahili.
- Uangamizaji salama wa taka zote ambazo haziwezi kutumika tena au kurejeshewa thamani.
Yaliyomo
- 1 Punguza taka unazozalisha
- 2 Tenganisha taka kwenye chanzo
- 3 Tengeneza mboji: Badilisha taka ngumu zenye asili ya kuoza kuwa mbolea
- 4 Tumia tena kile unachoweza
- 5 Urejesheaji taka thamani hubadili taka kuwa rasilimali
- 6 Ukusanyaji taka, usafirishaji na hifadhi
- 7 Kuanzisha kituo cha jamii cha usimamizi wa rasilimali taka
Punguza taka unazozalisha
Taka zinazoishia kwenye mitaa, nyumba na maeneo yetu huanzia katika shughuli za viwanda za utengenezaji bidhaa ambazo haziwezi kutumika mara kadhaa au kurejeshewa thamani. Lengo moja wapo la mpango wa jamii wa taka ngumu ni kupunguza taka kwa muda mrefu kwa kusaidia watu kupunguza matumizi ya vitu vinavyogeuka kuwa taka. Baadhi ya njia za kupunguza taka ni:
- Kutonunua vitu vilivyofungwa katika vifungashio vingi.
- Kuchagua vitu vyenye asili ya kioo au glasi na mbao kuliko plastiki na chuma.
- Kutumia mfuko au kikapu chako binafsi kubebea vitu unapokwenda kununua vitu dukani au sokoni, na kukataa mifuko ya plastiki inayotolewa na wafanyabiashara.
- Kununua chakula kwa wingi ili kupunguza kiasi cha vifungashio unavyoleta nyumbani.
Jamii zinaweza kufanya kazi na wenye maduka na serikali za mitaa ili kuzuia bidhaa ambazo zinaweza kusababisha matatizo ya kiafya kuingia katika jamii. Jamii iliyojipanga vizuri inaweza kuishinikiza serikali kutunga sheria za kuwalazimisha wenye biashara kuwajibika kwa taka wanazozalisha.
Tenganisha taka kwenye chanzo
Kuzuia mabaki ya vyakula kuchanganyika na taka za karatasi, vioo au glasi na taka zingine hurahisisha:
- matumizi ya taka hizo tena,
- kuzirejeshea thamani,
- kuziangamiza kwa usalama, na
- kupunguza matatizo ya kiafya yanayosababishwa na taka mchanganyiko.
Utenganishaji taka ndiyo hatua ya kwanza katika usimamizi bora zaidi wa taka. Hata hivyo, lazima iwepo njia nzuri ya kushughulikia taka hizo baada ya kutenganishwa. Utenganishaji taka ni sehemu ya mchakato wa usimamizi wa taka ngumu ambao unajumuisha utumiaji tena wa baadhi ya taka hizo, utengenezaji mboji, ukusanyaji mara kwa mara, urejeshaji thamani na uangamizaji salama wa taka zinazobaki.
Njia za kutenganisha taka
Sehemu kubwa ya taka zinazozalishwa maeneo ya mijini na vijijini ni taka zinazooza au takarojo au zenye unyevu (mabaki ya vyakula na taka za mazao ya bustani kama vile mimea na majani). Taka zenye uwezo wa kuoza huvunjwavunjwa na mwanga wa jua na maji, au kuliwa na viumbe hai (minyoo, wadudu na bakteria) na kubadilishwa kuwa mboji.
Kawaida, kuna kiasi kikubwa cha karatasi, vioo au glasi, na vyuma katika taka. Sehemu kubwa ya taka hizi hutokana na vifungashio vya bidhaa. Taka za nyumbani pia zinaweza kujumuisha vitu vyenye sumu kama vile rangi za kupaka nyumba au mitambo, betri, nepi za plastiki, mafuta ya magari, dawa za kuulia wadudu ambazo muda wake umekwisha, na makopo au chupa za dawa za kufanyia usafi nyumbani.
Taka rojo (zenye asili ya kuoza) au zenye unyevu -hubadilika kuwa mboji | Taka kavuhuchambuliwa na kutumika tena, kurejeshewa thamani, au kupelekwa kwenye dampo maalum ya taka. |
Taka rojo au zenye unyevu hugeuka kuwa mboji | Taka kavu, zenye uwezo wa kutumika tena na kurejeshewa thamani, hutenganishwa na kushughulikiwa ipasavyo au kupelekwa kwenye dampo maalum. | Taka zenye sumu huhitaji kushughulikiwa na kuangamizwa kwa utaratibu maalum |
Nani mwenye wajibu wa kutenganisha taka?
Taka zinaweza kutenganishwa na kaya au biashara zinazozalisha taka hizo, au na watu wanaozikusanya. Katika mfumo wowote ambao jamii yako inatumia kutenganisha na kukusanya taka kwa ajili ya kutumia tena, urejeshaji thamani, au kuangamizwa kwa usalama, ni muhimu kwa wale wanaofanya kazi hiyo kupewa heshima na ujira unaostahili juhudi zao.
Wakusanyaji taka wanaweza kujipatia fedha kwa kutenganisha na kuuza vile vitu vyenye thamani zaidi, na kupeleka taka zingine zilizotenganishwa kwenye kituo cha urejeshaji thamani taka. Baadhi ya wakusanyaji huwalipa wenye nyumba kiasi kidogo cha fedha kwa ajili ya taka zilizotenganishwa, au hutoza ada ndogo kwa kuondoa taka ambazo hazijatenganishwa.
Pale utenganishaji taka unapofanyika nyumbani, taka kavu zinaweza kuhifadhiwa kwenye vyombo vinavyofaa hadi zitakapochukuliwa. Vyombo kwa ajili ya taka rojo vinaweza kuwekwa nje ya nyumba, na kutumika katika kutengeneza mboji nyumbani au, vinaweza kukusanywa na mradi wa pamoja wa majirani wa kutengeneza mboji.
Mboji bora ambayo imeiva vizuri ina harufu nzuri na ni laini na nyeusi kama udongo mzito wa msituni. |
Tengeneza mboji: Badilisha taka ngumu zenye asili ya kuoza kuwa mbolea
Kwa sababu vitu vinavyooza ndiyo sehemu kubwa ya taka, kutenganisha mabaki ya vyakula na utengenezaji mboji husaidia kupunguza taka kwa kiwango kikubwa. Kuongeza mboji kwenye udongo ni njia ya kuiongezea na kuirudishia ardhi virutubisho vinavyotokana na mazao.
Njia bora zaidi ya kutengeneza mboji hutegemea ukubwa wa sehemu iliyopo. Kiasi kidogo cha mboji kinaweza kutengenezwa kwenye vyombo katika kila kaya au biashara. Miradi mikubwa zaidi ya utengenezaji mboji inaweza kuanzishwa katika miji na majiji, na kwenye mashamba yenye nafasi kubwa kwa ajili ya marundo makubwa ya taka.
Jinsi ya kutengeneza mboji kwa kutumia minyoo ya ardhini
Boksi kwa ajili ya minyoo linaweza kuwa la kawaida... |
...au linaweza kuwa na sehemu kadhaa maalum |
Minyoo ya ardhini ni miongoni mwa watengenezaji asili wakuu wa mboji. Sanduku dogo lenye minyoo wa ardhini wenye afya watakula mabaki ya chakula cha nyumbani na kugeuza taka kuwa udongo wenye rutuba sana kwa ajili ya bustani yako. Sanduku la minyoo ya ardhini hutoa fursa ya kutengeneza mboji kutokana na mabaki ya chakula pale ambapo hakuna eneo la kutosha kwa ajili ya kuhifadhi rundo kubwa la taka.
- Tengeneza matobo katika kitako cha sanduku la mbao au plastiki ili kuruhusu hewa kuingia, na maji na udongo kutoka.
- Weka sanduku la pili au sinia chini ya sanduku lenye matobo. Hili litakusanya udongo wote vizuri unaotengenezwa na minyoo.
- Jaza sanduku la juu vipande vya karatasi na majani makavu ambavyo vimechanwachanwa, na mabaki ya vyakula. Chukua koleo moja lililojaa minyoo wa ardhini kutoka mahali wanapozalishwa au kwa mkulima na kuwaweka katika sanduku hili.
Ongeza mabaki ya vyakula mara kwa mara na kuhakikisha sanduku linabaki na unyevunyevu lakini lisilowe. Funika sanduku la juu ili kuwakinga minyoo dhidi ya mwanga wa jua.
Kadri minyoo watavyokuwa wanakula vile unavyoweka kwenye sanduku hilo, watakuwa wanarutubisha udongo, na pia kuzaliana. Baadhi ya minyoo wanaweza kuangukia kwenye sanduku au sinia lililoko chini. Warudishe tu kwenye sanduku la juu, au wapeleke kwenye bustani yako na udongo mpya uliorutubishwa.
Jinsi ya kutengeneza mboji kwa utaratibu ambao unachukua muda mrefu
Njia hii ya kutengeneza mboji huhitaji nafasi na kazi kidogo, na mboji hupatikana baada ya takriban miezi 6.
- Chimba shimo ardhini lenye usawa wa sentimita 60 kwa 60, na kina cha mita 1.
- Tia kwenye shimo mchanganyiko wa taka zenye asili ya kuoza, zilizo kavu na zenye unyevu.
- Funika kila kina cha sentimita 20 za taka kwa sentimeta 3 za udongo na kuumwagia maji ili uzidi kuwa na unyevunyevu (ubaki na unyevu siyo kuloweshwa kabisa).
- Funika shimo ili kuzuia mvua kuingia. Baada ya wiki moja mboji inapaswa kuanza kutengenezwa. Rundo hilo la taka litapata joto na kupungua kadri litakavyozidi kuoza.
Jinsi ya kutengeneza mboji kwa utaratibu wa haraka
Hii ni njia ya kutengeneza mboji nyingi katika muda wa mwezi 1 hadi 4, kama unalo eneo kubwa la wazi.
- Chagua eneo tambarare lenye upana wa mita 1.5 na urefu wa mita 4. Simika nguzo kuonyesha eneo hilo. Lainisha udongo kwa kuutibua tibua hadi kina cha sentimita 30. Hii itasaidia rundo la mboji kutoa mvujo, na pia minyoo kuingia kwenye rundo na kula taka. Iwapo udongo umekauka sana, umwagie maji.
- Tafuta nguzo mbili zenye urefu angalau wa mita mbili na nusu.Simika nguzo hizo wima ardhini mahali udongo ulipolainishwa. Usizisimike chini sana ardhini kwa sababu baadae utazitoa.
- Weka alama ya mistari kwenye nguzo katika urefu wa sentimita 20 kutoka ardhini, halafu sentimita 5 juu yake, na sentimita 2 juu ya mstari huo. Rudia kuweka alama hizi za mstari mara 7 au 8 hadi nguzo nzima itakapokuwa imewekewa alama.
- Weka rundo la mabaki ya chakula na mimea (mchanganyiko wa mabaki makavu na yenye unyevu ndio mzuri zaidi) hadi kwenye alama ya mstari wa sentimita 20. Rundo linapaswa kufunika eneo lote lililoandaliwa na kulingana kwa usawa. Iwapo limekauka sana mwagia maji ili kupata unyevu lakini si kulowesha kabisa.
- Weka tabaka la mbolea ya wanyama hadi alama ya mstari wa sentimita 5 inayofuata. Mbolea ambayo haijakauka ni nzuri zaidi kwa sababu ina joto na husaidia mboji kuoza haraka. Juu ya mbolea ya wanyama, ongeza tabaka la udongo hadi alama inayofuata ya sentimita 2. Endelea kuongeza tabaka mbalimbali kwa kufuata utaratibu huu kadri taka zaidi zitakapokuwa zikipatikana. Mwagia kila tabaka maji kidogo ili rundo zima liwe na unyevunyevu. Baada ya muda unaweza kujenga rundo lenye kimo cha mita 2 au zaidi. Halafu funika rundo zima kwa tabaka la udongo, na limwagie maji zaidi.
- Baada ya siku mbili, ondoa zile nguzo. Hii itaacha mashimo mawili kwa ajili ya kuruhusu hewa kuingia kwenye rundo ili kusaidia uozaji. Baada ya wiki tatu, geuza na kuchanganya rundo zima kwa kutumia koleo. Fanya hivyo kila wiki au zaidi. Kadri utakavyoligeuza zaidi, ndivyo litakavyooza haraka. Rundo litapata joto na kunywea wakati uozaji ukiendelea. Baada ya mwezi 1 hadi 4, rundo linapaswa kutoa harufu nzuri, kugeuka na kuwa na rangi nyeusi, na udongo wenye rutuba.
Kujua ukamilifu wa mboji yako
Bila kuzingatia mbinu gani unatumia, zipo njia za kujua iwapo taka zako zinabadilika kuwa mboji nzuri na sio tu rundo kubwa la uchafu unaonuka.
- Ili kubadilika, mboji inahitaji taka nyevu kama vile mabaki ya vyakula na taka kavu kama nyasi kavu, majani makavu, maganda, au vipande vya karatasi vilivyo chanwachanwa. Iwapo rundo litabaki kuwa rundo la vyakula vinavyooza badala ya kupata joto na kubadilika kuwa udongo, linaweza kuhitaji vitu vikavu na mabaki ya mimea zaidi.
Rundo la mboji likizidi kupata joto wakati wa mchakato wa kubadilika kuwa mbolea. |
- Iwapo rundo linatoa harufu mbaya au halijanywea, linahitaji hewa zaidi. Geuza rundo hilo kwa kutumia koleo au tengeneza mashimo kwa kusimika nguzo katika rundo hilo.
- Iwapo rundo halipati joto, tatizo linaweza kuwa maji mengi au maji kidogo. Geuza rundo kwa kutumia koleo. Iwapo rundo hilo ni kavu sana, ongeza maji zaidi. Iwapo rundo hilo limelowa sana, ongeza maji kidogo sana. Kufunika rundo kwa kutumia karatasi kubwa ya nailoni pia kutasaidia rundo kubaki na joto.
- Iwapo rundo lina mchwa au siafu, ongeza maji zaidi.
- Iwapo rundo hilo linavutia nzi, linahitaji kufunikwa vizuri zaidi kwa kutumia udongo.
Baada ya muda mboji inapaswa kubadilika kuwa na harufu nzuri, na udongo mweusi wenye rutuba.
Vitu gani ambavyo havitakiwi kuingizwa katika utengenezaji mboji?
Usiingize vitu hivi katika taka kwa ajili ya kutengeneza mboji. |
Watu wana mawazo tofauti kuhusu kile kinachofanya mboji kuwa nzuri au la. Kwa mfano, baadhi ya watu huondoa mabaki ya nyama au karatasi. Wengine wengi wanakubali kwamba kinyesi cha ng’ombe, punda au farasi kinafaa kwa ajili ya kutengeneza mboji, lakini kinyesi cha mbwa, paka au nguruwe hakifai.
Matawi makubwa ya miti au majani mazito yataoza taratibu sana. Iwapo karatasi za kawaida au zile zinazotumika kutengeneza maboksi zitaingizwa, ni vizuri kuchanwachanwa na kulowanishwa kwa maji ili ziweze kuoza kwa urahisi zaidi. Nyama, mifupa na mabaki ya jikoni yenye mafuta huvutia wadudu na huoza taratibu sana.
Baadhi ya vitu kamwe havifai kabisa kwa ajili ya kutengeneza mboji. Plastiki, chuma, glasi na chochote kile ambacho hakijatoka ardhini moja kwa moja hakitaoza na kutengeneza mboji.
Mimea yenye sumu ambayo huathiri binadamu na mimea mingine kama vile mbegu za mbalika na mikaratusi, haiwezi kutengeneza mboji nzuri.
Tumia tena kile unachoweza
Taka kwa mtu mmoja inaweza kuwa riziki kwa mtu mwingine. Duniani kote, watu huokoa fedha na kulinda mazingira kwa kugundua mbinu mpya za kutumia tena kwa usalama vitu vilivyotupwa. Kwa mfano, kutokana na:
- matairi: hutengeneza malapa, ndoo na vyombo vya kuoteshea mimea, kuzuia mmomonyoko wa ardhi nk.
- makopo: hutengeneza taa za chemli, vibatari, vyombo vya kuoteshea mimea, stendi za mishumaa nk.
- mifuko ya chakula iliyotengenezwa kutokana na kemikali ya salfeti: hutengeneza mifuko ya kuhifadhia vitu na vikapu vya kubebea bidhaa kutoka dukani au sokoni.
- vifuu vya nazi: hutengeneza vikombe, uma, vijiko, mifuniko, urembo n.k.
- majani makavu ya migomba: hutengeneza kamba, vifaa vya sanaa, vifungashio, vifaa vya kuezekea mabanda n.k.
- mabaki ya chuma: hutengeneza stovu, taa na vitu vya sanaa.
- karatasi: hutengeneza mifuko na vifungashio, na huwashia moto, hasa majiko ya mkaa.
- vumbi la mbao, hususan kwenye karakana: hutengeneza mboji, nishati ya kupikia katika majiko maalum, au hugandamizwa kama tofali na kutumika kwa ajili ya kupikia kama nishati.
Urejesheaji taka thamani hubadili taka kuwa rasilimali
Mchakato wa kurejeshea thamani mfuko mmoja wa taka za makopo ya alumini huokoa nishati ya kuweza kuwasha Televisheni moja kwa saa kumi na nane! |
Urejeshaji thamani huchukua vitu ambavyo havifai tena na kuvigeuza kuwa rasilimali kwa ajili ya kutengenezea vitu vipya ambavyo vinafaa. Urejeshaji thamani wa baadhi ya vitu (kama vile vyuma na mipira) lazima ufanyike viwandani. Vitu vingine kama vile karatasi na glasi au vioo vinahitaji mashine na nafasi ndogo tu na vinaweza kushughulikiwa katika karakana ndogo au hata kwenye nyumba za watu.
Urejeshaji thamani taka ni njia muhimu ya kupunguza taka. Lakini urejesheaji taka thamani huhitaji msaada kutoka serikalini na kwa wenye viwanda, pamoja na msimamo thabiti wa jamii na watu binafsi. Kama hakuna soko kwa ajili ya bidhaa kutokana na taka zilizorejeshewa thamani, au hata kama urejeshaji thamani haujafanyika kwa usalama, njia hii haiwezi kuwa suluhisho hata kidogo.
Urejesheaji taka thamani hupunguza taka kwa kuzibadili kuwa bidhaa mpya na pia kuokoa nishati inayotumika viwandani katika utengenezaji bidhaa mpya. Kwa mfano, kutengeneza karatasi kwa njia ya urejeshaji thamani hupunguza nishati inayohitajika kutengeneza karatasi mpya kabisa kwa theluthi mbili (⅔), au kutengeneza chuma cha pua kutoka vyuma chakavu ukilinganisha na nishati inayohitajika kutengeneza bidhaa hiyo kutokana na mawe ya madini ghafi ya chuma. Kutengeneza alumini kutoka kwenye taka chakavu za alumini hutumia kiasi kidogo tu cha nishati ambayo ingehitajika kutengeneza rasilimali hiyo kutoka kwenye mawe ya madini ghafi ya boksiti-madini ambayo hutengeneza alumini.
Ni dhahiri kuwa urejesheaji taka thamani:
- Hupunguza kiwango cha taka ngumu ambazo zinachafua mazingira yetu.
- Hupunguza kiwango cha taka ngumu zinazotakiwa kuzolewa, hivyo kuokoa fedha na nafasi (ardhi).
- Hupunguza matumizi ya rasilimali kwa kutumia rasilimali zaidi ya mara moja.
- Husaidia kukuza uchumi wa eneo husika na uchumi wa kitaifa kwa kupunguza kiasi cha malighafi ambazo zinatakiwa kuagizwa kutoka nje.
- Hutoa fursa za ajira.
Ni vifaa gani ambavyo vinaweza kurejeshewa thamani?
Vifaa ambavyo vinaweza kurejeshewa thamani hutegemea viwanda vya urejeshaji thamani vilivyopo katika eneo husika.
Kioo au glasi: Glasi hutengenezwa kutokana na mchanga, madini ya magadi (soda ash) na chokaa. Kioo kinapotupwa kama taka huweza kulika lakini hakiozi na kurudia asili yake ya madini ya awali. Hivyo urejeshaji thamani wa glasi au kioo kawaida huhitaji taka za asili ya glasi kutenganishwa kwa rangi, kuyeyushwa na kuwa maji maji, na kutengenezwa katika maumbo mbalimbali ya vyombo vipya. Baadhi ya taka glasi hurejeshewa thamani na kutumika kwa ajili ya barabara au majengo.
Alumini: Alumini inatokana na mawe ya madini chuma aina ya boksiti ambayo huchimbwa kutoka ardhini. Taka za bidhaa za alumini haziozi na hivyo haziwezi kurudi katika asili yake ya madini ya awali lakini humomonyoka tu kama glasi. Alumini hurejeshewa thamani kwa kuyeyushwa na kutengenezwa kuwa bidhaa mpya kama makopo na vinginevyo.
Makopo ya chuma au bati: Makopo ya kuhifadhi vyakula vilivyosindikwa mfano matunda na nyanya hurejeshewa thamani kwa kutenganisha bati na chuma. Chuma na bati baadaye husafishwa na kuuzwa kama malighafi ya kutengeneza makopo zaidi au vitu vingine.
Mpira: Hutengenezwa kutokana na utomvu wa miti na petroli. Mpira wakati mwingine hurejeshewa thamani kwa kuyeyushwa au kukatwakatwa na kutengenezwa katika maumbo ya bidhaa nyingine.
Karatasi: Hutengenezwa kutokana na miti, pamba na mazao mengine yenye nyuzi ngumu. Karatasi ni moja ya bidhaa chache ambayo inaweza kurejeshewa thamani na kurudia hali yake ile ile. Karatasi kwa ajili ya matumizi ya kibiashara mara nyingi hurejeshewa thamani viwandani. Lakini karatasi inaweza kurejeshewa thamani pia kwa kutumia mikono na kutoa bidhaa nzuri za karatasi kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na biashara.
Bidhaa zenye kemikali ya sumu: Bidhaa hizo, vikiwemo kompyuta, betri, vifaa vya elektroniki, rangi, viuatilifu na vyombo vinavyohifadhi bidhaa hizo vinahitaji uangalifu katika kuvishughulikia ili wale wanaofanya kazi ya kuvirejeshea thamani wasidhurike. Baadhi ya bidhaa hizo haziwezi kurejeshewa thamani kabisa. Hivyo kimsingi, kwa bidhaa kama hizo, ni bora kutengeneza chache sana.
Tatizo katika urejesheaji thamani taka za plastiki
Taka za plastiki zinaporejeshewa thamani, ubora wake hupungua. Chupa ya plastiki hairejeshewi thamani na kuwa chupa nyingine ya plastiki, lakini hutengeneza kitu kingine chenye ubora wa chini. Kwa sababu hii, plastiki inaweza kurejeshewa thamani mara chache tu na baada ya hapo haitafaa tena.
Urejesheaji thamani wa baadhi ya taka za plastiki huachia gesi ya sumu yenye madhara kwa wafanyakazi viwandani na jamii. Na taka nyingi za plastiki ambazo zinatakiwa kurejeshewa thamani huishia kwenye madampo ya taka. Hivyo, ni bora kupunguza matumizi ya plastiki kadri iwezekanavyo.
Ukusanyaji taka, usafirishaji na hifadhi
Kama jamii yako haina huduma ya ukusanyaji taka ya kuaminika, unaweza kuanzisha huduma hiyo kwa msaada wa serikali ya mtaa na asasi za kibiashara. Wakati unapanga, kumbuka taka gani zitakazokusanywa na iwapo ni kwa ajili ya mauzo kwa biashara na viwanda vikubwa vya urejesheaji taka thamani au kwa miradi ya jamii ya urejesheaji taka thamani.
Ni bora zaidi taka kusafirishwa umbali mdogo. Lakini jamii nyingi hazina uwezo wa kurejeshea taka thamani katika maeneo yao. Hivyo, njia nyingine za ufumbuzi hazina budi kutafutwa.
Namna ya kuandaa taka kwa ajili ya ukusanyaji, usafirishaji na hifadhi
Jinsi taka zinavyoandaliwa kwa ajili ya kukusanywa, kusafirishwa na kuhifadhiwa hutegemea ukubwa wa eneo lililopo, nani atanunua taka zinazobaki, na zitatumika kwa ajili ya nini. Ili kuzuia harufu mbaya na kuenea kwa vijidudu vya magonjwa, bidhaa zinatakiwa kusafishwa, kukaushwa, kubondwabondwa na kuwa kama bati au kupangwa vizuri pamoja ili kutumia nafasi kidogo kadri inavyowezekana na kuzuia uwezekano wa ajali.
Kompyuta, redio na televisheni zinakuwa na vifaa vingi ambavyo vinaweza kuuzwa na kurejeshewa thamani. Lakini ndani ya vifaa hivyo, kuna kemikali zenye uwezo wa kudhuru. Vitu hivi huwa vinatenganishwa baada ya kupata mafunzo kuhusu kila bidhaa husika, na kwa kutumia vifaa vya kujikinga katika mazingira yenye hewa ya kutosha. Vyombo vyote vinavyohifadhi kemikali za sumu au vitu vyenye uwezo wa kudhuru afya na mazingira vinahitaji kushughulikiwa kwa uangalifu chini ya utaratibu maalum.
Afya na usalama kwa wazoaji taka
Wazoaji taka wako hatarini kutokana na matatizo yote ya kiafya yanayohusiana na taka. Ili kuzuia madhara, wazoaji taka wanahitaji mafunzo ya kuzuia matatizo ya kiafya, na wapi wanapostahili kwenda kupata msaada pale matatizo yanapotokea.
Wazoaji taka wanaweza kujipanga na kuunda ushirika na biashara zao ndogo ndogo ili kurahisisha ukusanyaji rasilimali au mitaji, utoaji mafunzo na upatikanaji wa misaada kutoka serikalini au jamii kwa ajili ya kununua vifaa vya usalama na kujikinga, na hivyo kuifanya kazi hiyo kuwa salama zaidi.
Kuanzisha kituo cha jamii cha usimamizi wa rasilimali taka
Kituo cha jamii cha usimamizi wa rasilimali taka ni sehemu ambapo vitu ambavyo vinaweza kutumika tena au kurejeshewa thamani hukusanywa kwa ajili ya kuuzwa au kutumiwa tena. Kituo pia kinaweza kuwa mahali pa kuanzisha mradi wa jamii wa urejesheaji taka thamani na bustani ya mbogamboga kwa ajili ya wateja wa karibu, utengenezaji wa bidhaa mpya kutokana na vifaa vya zamani na ubadilishanaji wa vitu kama vile nguo, pazia, vyombo vya nyumbani, samani, chupa, vifaa vya ujenzi n.k.
Watu wakishirikiana na kufanya kazi pamoja wanaweza kuifanya jamii kuwa sehemu nzuri kuishi. |
Vituo vya jamii vya usimamizi wa rasilimali taka
Jamii kadhaa nchini Ufilipino wana vituo vya usimamizi wa rasilimali taka ambavyo vimeanzishwa na serikali za mitaa kwa kushirikiana na asasi moja ya mazingira iitwayo Mother Earth Foundation. Vituo hivi vya usimamizi wa rasilimali taka vimekuwa mfano kwa programu za jamii za usimamizi wa taka ngumu nchi nzima, na vimesaidia kubadili mfumo mzima wa usimamizi wa taka.
Kaya huhamasishwa kutenganisha taka zao na kusafisha vifaa ambavyo vinaweza kutumika tena au kurejeshewa thamani. Baadhi ya jamii zimepitisha sheria ya kupunguza harufu mbaya inayozuia watu kulundika taka nje.
Watu hutunza taka zao zenye asili ya kuoza kwenye vyombo vilivyofunikwa katika nyumba zao au hutakiwa kuzipeleka kwenye mapipa ya taka kwa ajili ya mboji yaliyowekwa kila sehemu katika jamii. Kila siku, wafanyakazi kutoka kwenye vituo vya usimamizi wa rasilimali taka hupitia jamii mbalimbali, wakitumia magari ya mkokoteni yenye magurudumu matatu, kukusanya taka zenye asili ya kuoza, taka zenye uwezo wa kurejeshewa thamani, na taka ambazo zinafaa kutupwa kabisa. Mara nyingine watu hulipwa kwa ajili ya taka zao zenye sifa ya kurejeshewa thamani. Kila kitu hupelekwa kwenye kituo cha usimamizi wa raslimali taka ambacho kina sehemu kuu mbili:
- Bustani ekolojia (bustani inayoendeshwa kwa msingi unaolinda uwiano kati ya mazingira na viumbe hai) mahali ambapo mboji hutengenezewa na kutumika kwa ajili ya kilimo cha mboga mboga ambazo huuzwa kwa jamii.
- Banda ekolojia au stoo ni mahali ambapo vifaa safi vyenye uwezo wa kurejeshewa thamani huhifadhiwa kabla ya kuuzwa kwa maduka ya vitu chakavu, na makampuni au viwanda vya kurejeshea thamani taka.
Baadhi ya vituo hutoa nafasi ya kufanyia kazi ambapo watu hutengeneza bidhaa mpya kutokana na vile vilivyotumika. Katoni za juisi hubondwa na kushonwa pamoja ili kutengeneza mifuko ya kubebea vitu. Chupa za glasi hubadilishwa na kuwa glasi za kunywea maji. Magazeti ya zamani hukatwa vipande vipande na kushonwa pamoja ili kutengeneza vikapu na mifuko, ambavyo huunganishwa na gundi na kuvifanya kuwa vigumu na imara zaidi. Vitu hivi huuzwa ili kuwapatia pato wanaovitengeneza na wakati kiasi kingine huchangia gharama za uendeshaji wa vituo.
Vituo hivi vimesaidia sana, kwa kiwango ambacho hakikutarajiwa, kupunguza kiasi cha taka katika jamii hizo. Badala ya kuendelea kuishi na marundo ya taka yanayotoa harufu mbaya, watu hivi sasa wana pato zaidi kutokana na vifaa vinavyotumika tena na vilivyorejeshewa thamani, na huzalisha mboga mboga kwa kutumia mboji itokanayo na mabaki ya vyakula.