Hesperian Health Guides
Taka mchanganyiko ambazo hazisimamiwi vizuriu
HealthWiki > Mwongozo wa jamii juu ya afya ya mazingira > Sehemu ya kwanza: Kubadili hatari ya kiafya kuwa fursa > Taka mchanganyiko ambazo hazisimamiwi vizuri
Pale taka zinaporundikana au kutapakaa katika jamii zetu, husababisha kinyaa, harufu mbaya, kero na hatari kubwa kwa afya. Taka zisipotenganishwa, kiasi cha taka na matatizo yanayosababishwa na taka hizo huwa kubwa kuliko inavyostahili. Pale taka zenye madhara, kama vile betri zilizotumika na taka za hospitali au kutoka vituo vya afya zinapochanganywa na taka za kawaida kama vile karatasi na mabaki ya vyakula, mchanganyiko huo huwa mgumu na wa hatari kushughulikia.
Zisipoondolewa kwa usalama, taka hizo zinaweza kusababisha matatizo ya kiafya:
- Marundo ya taka huzalisha panya, nzi, mbu, mende na wadudu wengine ambao hueneza vijidudu vya magonjwa kama vile malaria, dengue fever, homa ya uti wa mgongo, typhus na mengine.
- Dampo na marundo ya taka huzalisha vijidudu vya maradhi. Vijidudu hivi vinaweza kuambukiza watoto wanaochezea maeneo hayo na watu wanaopekua taka hizo kutafuta vitu mbalimbali vya kutumia au kuuza. Vijidudu kwenye taka hizo vinaweza kusababisha matatizo ya kiafya kama vile kuhara na kipindupindu, magonjwa ya ngozi, pepopunda, fangasi, na maambukizi mengine ya ngozi na macho.
- Taka huziba njia za maji na mitaro na kusababisha maji kutuama. Hali hii husababisha madimbwi ya maji ambayo huruhusu wadudu kuzaliana, na pia mafuriko kutokea pale mvua zinaponyesha. Mitaro ya maji iliyofurika hubeba vinyesi vya binadamu na wanyama, na pia kuchafua vyanzo vya maji ya kunywa, na udongo.
- Marundo makubwa ya taka yakiporomoka na taka hizo kusambaa, yanaweza kuwadhuru watu wanaoshughulikia taka hizo au wanaoishi karibu.
- Kemikali zenye sumu zilizomo ndani ya baadhi ya taka zinaweza kuvuja na kuingia kwenye vyanzo vya maji na udongoni, na kuathiri watu kwa miaka mingi. Wakati mwingine marundo ya taka zenye sumu hulipuka au kushika moto.
- Taka za plastiki na taka zingine zenye sumu zinapochomwa katika eneo la wazi au katika tanuri maalumu za uteketezaji, kemikali zenye sumu huingia hewani, na majivu ya sumu huathiri udongo na maji. Katika muda mfupi, kemikali hizi zenye sumu zinaweza kusababisha maambukizi kifuani, kikohozi, kichefuchefu, kutapika, na maambukizi ya macho. Madhara ya muda mrefu yanayosababishwa na kemikali hizi zenye sumu ni pamoja na magonjwa yasiyopona kama vile saratani, na kuzaa watoto wenye ulemavu.
Kuvaa mipira ya mikononi, vifunika pua na mdomo, na viatu maalumu vinavyofunika miguu kunaweza kuzuia matatizo mengi ya kiafya yanayosababishwa na kushughulika na taka ngumu.