Hesperian Health Guides

Baadhi ya taka hudumu muda mrefu

Katika sura hii:

Taka ni changamoto karibu kila mahali kwa sababu tunaendelea kuzalisha taka nyingi sana. Na kama tunavyoona kwenye maeneo yanayotuzunguka, taka kutokana na plastiki, glasi na chuma haziozi.

Vyakula na bidhaa nyingine zamani vilikuwa vikifungwa kwenye vifungashio vya asili na ambavyo vinaweza kutumika tena, kama vile majani ya migomba, vikapu au magazeti. Vyombo vya kuhifadhia au kubebea na vifaa vingine vilikuwa vikitengenezwa kutokana na udongo wa mfinyanzi, miti au malighafi nyingine kutoka ardhini. Pale vilipotupwa, vitu hivi havikubaki kama taka kwa muda mrefu kwa sababu vilioza haraka na kuwa udongo.

Hivi sasa, viwanda vikiwa vinatumia vifaa kama plastiki, vyuma na kemikali, bidhaa nyingi kutoka viwandani hugeuka kuwa taka baada ya kuvitumia. Vifaa vingi kama vile chupa, ndoo, mifuko, hata magari na kompyuta vimetengenezwa kutokana na malighafi ngumu na nyepesi, lakini huchukuwa muda mrefu kuoza. Kufungasha bidhaa kwenye makopo, chupa, na mifuko ya plastiki hurahisisha usafirishaji na uuzaji wa bidhaa hizo, lakini husababisha taka nyingi zaidi.

Mduara wa maisha ya mfuko wa plastiki


 Arrows lead from an oil tanker and drilling platform, to a refinery, to a woman carrying a plastic bag, to a dog at a trash heap.
Awali, watu walikuwa wakitumia vikapu na mifuko ya nguo kubebea vitu. Hivi sasa tunatumia mifuko ya plastiki na milioni ya mifuko hiyo hutengenezwa na kutupwa kila mwaka.
Mafuta huchimbwa chini ya ardhi au chini ya bahari.
Mafuta ghafi husafishwa na kuchanganywa na kemikali ili kutengeneza plastiki. Mali ghafi ya plastiki baadaye hutumika kutengeneza bidhaa mbalimbali pamoja na mifuko ya plastiki au nailoni
Kwa sababu bei ya mafuta haikua ghali sana na plastiki inafaa sana kwa njia mbalimbali, mifuko ya plastiki au nailoni hutumika duniani kote. Mara nyingi hutumika kwa dakika chache tu na kutupwa.
Mifuko ya plastiki huishia barabarani, viwanjani, na katika madampo ya taka. Huziba njia na mitaro ya maji na husababisha vifo vya wanyama. Ikichomwa huachia gesi yenye sumu. Ikifukiwa ardhini hakuna anayejua itachukua muda gani kuoza kabisa.Ukurasa huu ulihuishwa: 04 Juni 2022