Hesperian Health Guides

Taka sifuri: Kutozalisha taka kabisa!

Katika sura hii:

Jamii nyingi duniani kote zinatafuta njia za kupunguza taka zao hadi sifuri, yaani kufikia lengo la kutozalisha taka kabisa. Taka sifuri humaanisha kupunguza uzalishaji wa taka, kuzirejeshea thamani taka zote zilizobaki na kuzirudisha katika asili yake au kwenye soko kwa njia ambazo zinalinda afya na mazingira.

Ili kufikia lengo la taka sifuri, viwanda lazima viwajibike kwa kuzalisha kidogo au hata kutozalisha kabisa bidhaa ambazo zinatumika mara moja tu, kwa mfano plastiki. Majiji na miji inaweza kuanzisha programu za kutumia taka ngumu zinazozalishwa kutengeneza mboji, urejesheaji taka thamani na kupunguza uzalishaji wa taka. Ili kufanikiwa zaidi, watu ambao wanaathirika zaidi na taka hawana budi kushirikishwa.

Jinsi mji ulivyopambana na taka ngumu na kufanikiwa

Kovalam, mji wenye mandhari nzuri katika mwambao kusini mwa India, ni sehemu inayopendwa sana na watalii. Lakini biashara ya utalii ilikaribia kufa kabisa kutokana na kuzagaa kwa taka.


Kwa miaka 30 ya utalii, mji wa Kovalam haukuwahi kuwa na njia salama ya kusimamia taka zake. Kulikuwa hakuna vyombo vya kukusanya taka, hakuna programu ya kuzirejeshea taka thamani, matumizi kidogo ya mboji, na maelfu ya watalii waliuhama mji huo, mwaka hadi mwaka, wakiuacha ukizama zaidi katika taka. Mifuko ya plastiki iliziba bomba na njia za maji, mbu wakizaliana katika marundo ya taka, na mji ukaendelea kuwa na sura mbaya na kuhatarisha afya.


Viongozi wa Halmashauri ya mji huo waliamua kuanzisha program ya ukusanyaji taka na kujenga tanuri la kuchoma taka. Lakini watu wengi walilalamika kwamba uchomaji ungebadilisha taka kuwa moshi na majivu yenye sumu ambavyo vingechafua hali ya hewa. Baada ya mjadala mrefu, tanuri la kuchoma taka halikujengwa, na serikali iliomba vikundi vilivyopinga mpango huo kupendekeza njia mbadala.


Wakiongozwa na asasi moja ya kiraia ya Ulinzi wa Maliasili, jamii ilipendekeza mpango wa Taka Sifuri. Watu kutoka jamii mbalimbali walitembeleana kubadilisha mawazo juu ya mikakati yao ya kufikia lengo la Taka Sifuri. Mama mmoja, kwa jina la Murali, alionyesha jinsi alivyotengeneza na kuuza bakuli, vikombe, vijiko, begi na vitu vingine vya maana kutokana na vifuu vya nazi, majani ya mnazi, na karatasi zilizotumika. Kwa kuhimiza matumizi ya taka kutengeneza mboji na njia mpya za kutumia tena vitu vilivyokwishatumika, asasi ya Kovalam Taka Sifuri ilizaliwa.


Baada ya miaka michache, Mji wa Kovalam, ulikuwa msafi, wenye mandhari nzuri na hali bora ya kiuchumi kuliko wakati wote ule. Hivi sasa mji una kivutio kipya cha utalii-Kituo cha Taka Sifuri. Migahawa mingi katika mji huo hivi sasa hutumia vikombe ambavyo vimetengenezwa kutokana na vifuu vya nazi na majani kutokana na majani ya mnazi. Akinamama wa Kovalam Taka Sifuri hivi sasa hulima mbogamboga na ndizi kwa kutumia mboji, na mji umejenga kituo cha kuzalisha umeme ambacho kinatumia vinyesi vya watu na wanyama.


Mji wa Kovalam umekuwa mfano kwa kuonesha jinsi ya Mkakati wa Taka Sifuri unavyoweza kurudisha uhai na kuboresha afya ya jamii, mandhari yake ya asili na kulinda mazingira kwa ajili ya vizazi vijavyo.Ukurasa huu ulihuishwa: 04 Juni 2022