Hesperian Health Guides

Shimo maalum la kuhifadhi taka

Katika sura hii:

Shimo maalum la kuhifadhi taka ni shimo lenye tabaka la kinga lisilopitisha mvujo sakafuni na kupitia kuta zake, ambalo hujazwa taka na kushindiliwa na mashine (ili ziweze kugandamana ) na hatimaye kufukiwa. Shimo kama hili linaweza kupunguza madhara ya taka ambazo zimerundikana na ni salama kuliko dampo za taka zinazobaki wazi. Lakini hata mashimo maalum ya kuhifadhi taka hatimaye hujaa na, baada ya miaka mingi, yanaweza kuanza kuvuja. Hivyo, ili kukabiliana na matatizo ya taka, kimsingi, bado tunatakiwa kupunguza uzalishaji wa taka hizo.

Dampo za wazi zinaweza kubadilishwa na kuwa mashimo maalum ya kuhifadhi taka. Au jamii inaweza kujenga shimo maalum jipya na kusafisha eneo la zamani kwa kuhamisha taka na kuzipeleka kwenye shimo jipya. Shimo maalum la kuhifadhi taka hulinda afya ya jamii iwapo:

  • Limejengwa mbali na makazi ya watu.
  • Limefunikwa ili kuzuia wadudu na wanyama wengine wanaosambaza magonjwa kuzaliana.
  • Lina tabaka la udongo wa mfinyanzi mgumu au plastiki kuzuia kemikali, au vijidudu vya magonjwa kuchafua maji yaliyoko chini ya ardhi.


Kwa sababu ujenzi na utunzaji wa shimo maalum la kuhifadhi taka ni kazi kubwa, mara nyingi inatakiwa kufanyika kwa ushirikiano na jamii, serikali ya mtaa na asasi nyingine kama vile makanisa/misikiti, viwanda na biashara mbalimbali.

Shimo maalum la kuhifadhi taka hulinda afya ya jamii pale tu ambapo linasimamiwa vizuri. Usimamizi mzuri ni pamoja na:

  • mafunzo na misaada inayostahili kwa wanaofanya kazi kwenye kituo hicho, na
  • ushirikiano mzuri na vituo vya jamii vya usimamizi wa rasilimali taka, wakusanyaji wa taka sumu, na serikali za eneo husika.

Kuchagua sehemu inayofaa

Hatua ya kwanza katika kupanga shimo maalum la kuhifadhi taka ni kuchagua eneo au sehemu inayofaa. Mara nyingi, serikali hudai tathmini ya sehemu hiyo kabla ya kuanza ujenzi. Tathmini hii inajumuisha uchunguzi wa aina ya udongo na miamba, aina ya mimea ambayo inaota sehemu hiyo na umbali kutoka vyanzo vya maji na makazi ya watu. Kwa kuzingatia mahitaji ya afya na usalama wa jamii, eneo la shimo maalum la kuhifadhi taka linatakiwa kuwa angalau:

  • Mita 150 kutoka maji ya fukwe za bahari.
  • Mita 250 kutoka vyanzo vya maji baridi kama vile mito, mabwawa vinamasi au maeneo oevu.
  • Mita 250 kutoka hifadhi za misitu.
  • Mita 500 kutoka makazi ya watu na visima au chanzo chochote kingine cha maji ya kunywa.
  • Mita 500 kutoka kwenye maeneo dhaifu ambayo yanaweza kuathiriwa na tetemeko la ardhi.


Kina cha shimo kinapaswa kuwa angalau mita mbili juu ya tabaka maji.

Kutengeneza shimo maalum la kuhifadhi taka

Ukubwa wa shimo utategemea kiasi cha taka ambacho kinatakiwa kuhifadhiwa humo. Mashimo yote yanapaswa kuwa membamba chini kuliko juu ili kuzuia yasibomoke. Umbo hili pia husaidia ugandamizaji wa taka kwa sababu kuna uzito zaidi sehemu za juu kuliko za chini.

Bango nje ya Shimo linaloonyesha muda wa kufungua na kufunga husaidia wafanyakazi kwenye kituo hicho kudhibiti taka zinazotupwa ndani, muda gani na namna gani.

Illustration of the below: A landfill.

Shimo maalum la kuhifadhi taka ambalo limejengwa vizuri na lenye vifaa vya kutosha

Vifaa vya kuzima moto kama vile mchanga, udongo, au chanzo cha maji
Marundo ya taka za mboji yakiwa yamefunikwa
Banda la kuhifadhi vifaa vya kazi, kinga na nguo za wafanyakazi
Choo na sehemu ya kuoga au kunawa mikono baada ya kushika taka
Bomba kwa ajili ya kupitisha gesi kutokana na taka
Uzio kuzunguka eneo zima ukiwa na mlango wa kufunga eneo
Vyombo vya taka za kurejeshewa thamani
Kuta zenye mteremko kuzuia shimo lisibomoke

Tabaka la kuzuia mvujo lina safu tatu:

Safu ya juu- mita 1 udongo uliogandamizwa
Safu ya kati-nusu mita ya kokoto
Safu ya chini-angalau mita 1 ya udongo wa mfinyanzi uliopondwa pondwa

Kuweka tabaka la kuzuia mvujo kwenye shimo

Ili kulinda maji yaliyo chini ya ardhi yasichafuliwe, shimo maalum la kuhifadhi taka linatakiwa kuwa na tabaka la kinga ya kuzuia mvujo sakafuni. Tabaka la kuzuia mvujo linaweza kutengenezwa kutokana na mgandamizo wa udongo wa mfinyanzi, kifusi na udongo wa kawaida. Shimo hili likijengwa katika eneo lenye udongo mgumu wa mfinyanzi hurahisisha lengo hili.

Kama kuna uwezo wa kuweka kizuizi bora cha mvujo, matandiko mazito ya plastiki na vizuiaji vingine vinaweza kutoa kinga zaidi, na mfumo wa mabomba na pampu unaweza kujengwa ili kuondoa maji maji.

Kujaza shimo

Utaratibu wa kujaza shimo maalum la kuhifadhi taka hutegemea wingi wa taka, muda ambao watu wanao wa kuifanya kazi hiyo, na hali ya tabia nchi ya eneo husika.

Katika sehemu zenye mvua nyingi na taka kidogo kama vile miji ambayo inazingatia kanuni ya kutozalisha taka kabisa, kila wiki au kila mwezi unaweza kuchimba shimo jipya lenye tabaka la kuzuia mvujo la mfinyanzi na kifusi. Kunakua na mtu mwenye jukumu la kuleta taka, kuzijaza kwenye shimo, kuzishindilia na kuzifukia kwa udongo. Ufukiaji taka kidogo kidogo huzuia maji kujikusanya ndani ya shimo.

Kwa jamii inayozalisha mzigo mkubwa wa taka, ni bora zaidi kuchimba shimo kubwa la kuhifadhi taka hizo. Wafanyakazi kwenye shimo hilo hujaza taka kwenye shimo kadri zinavyoletwa. Kila mara taka zinapoongezwa hugandamizwa chini na kutengeneza tabaka linalolingana, halafu hufunikwa na majani makubwa (k.m. makuti, majani ya migomba) na tabaka la udongo, au udongo, majivu na mchanga. Hii itadhibiti harufu mbaya na kuzuia wadudu kuzaliana. Kuweka paa kubwa juu ya shimo huzuia mvua kuingia.

A dog chases a rabbit through a meadow.
Baada ya shimo kufunikwa kabisa, shimo ambalo limesimamiwa vizuri linaweza kugeuka eneo la kijani lenye kupendeza.

Kufunika shimo

Pale shimo linapojaa, linapaswa kufunikwa kwa tabaka kubwa la udongo, angalau lenye sentimita 90 kwenda chini. Maua pori na majani yanaweza kupandwa juu yake lakini siyo mazao ya kula kama vile mboga mboga au miti ya matunda. Hadi shimo litakapofunikwa kabisa na mimea, wanyama wanapaswa kulishwa mbali na hapo.

Baadhi ya changamoto kuhusiana na mashimo ya kuhifadhi taka

Shimo mahali ambapo taka hutupwa na baadaye kufukiwa kwa udongo, pale linapojaa, linaweza kutunzwa kwa usalama bila matatizo mengi. Lakini linaweza kuleta matatizo endapo maji maji kutokana na mchujo wa taka na gesi aina ya methani vitajikusanya kwenye shimo.

Taka maji (mchujo wa taka)

Maji ya mvua yanapopenya kwenye shimo la taka hutengeneza maji taka yenye harufu mbaya ambayo yanaweza kusafirisha sumu hadi kwenye maji yaliyo ardhini. Hii ndiyo sababu ya kuzungusha shimo la taka zima na tabaka la kuzuia mvujo, na kutojenga shimo hilo karibu na mto, ziwa au chanzo cha maji ya kunywa.

Njia bora kuzuia kuibuka kwa maji taka kwenye shimo ni kulifunika na paa, au maturubai au plastiki.

Gesi hatari

Katika mashimo ya kuhifadhi taka yenye mchanganyiko wa taka, bakteria wanaweza kuzaliana na kutengeneza gesi ya methani. Gesi ya methani inaweza kulipuka au kushika moto kama haitadhibitiwa. Vile vile gesi hiyo huchangia kuongezeka kwa joto duniani. Sehemu mbalimbali, gesi ya methani kutoka kwenye mashimo ya taka huvunwa na kutumika kuzalisha umeme. Kama hakuna rasilimali za kuivuna na kuitumia ipasavyo, njia bora ni kuweka bomba kwenye shimo na kuruhusu itoke.

EHB Ch18 Page 415-1-a.png
Bomba za kupitisha gesi katika shimo salama la taka

Bomba rahisi la kutolea gesi linajumuisha njia ya kupitisha gesi ambayo imetengenezwa na mawe madogo madogo ambayo yamewekwa katika wavu wa waya uliosimamishwa kwenye umbo la mduara. Unaweza pia kutumia mapipa ya chuma ya lita 200 ambayo yameondolewa vitako. Urefu wa bomba la kutolea gesi huongezwa kadri usawa wa taka katika shimo unavyoongezeka. Idadi ya bomba za kutolea gesi zinazohitajika zitategemea ukubwa wa shimo na aina ya taka katika shimo.

Shimo maalum la taka ambalo limefunikwa na kuna majani au mimea ambayo inaota juu yake linaweza kuwa bado linazalisha gesi ya methani. Kama kuna mafungu ya majani au mimea inayoota juu yake, inaweza bado kutoa methani. Kama kuna sehemu yenye majani yaliyooza au kunyauka, hasa ikiwa katika muundo wa mduara, hii ni dalili kwamba methani inatoroka kutoka kwenye shimo lililofunikwa. Weka matangazo ya tahadhari kwa jamii kukaa mbali, angalau mita 10, kutoka eneo hilo kwa sababu mlipuko unaweza kutokea. Wataalamu wanaweza kupewa taarifa ili kufanya uchunguzi na kuchukua hatua zinazostahili kuzuia mlipuko kutokea.




Ukurasa huu ulihuishwa: 04 Juni 2022