Hesperian Health Guides

Kuanzisha asasi za kijamii

Katika sura hii:

Kuanzisha asasi za kijamiiUdhibiti wa maliasili wenye haki na usawa huhitaji sauti ya watu wote kusikika katika maamuzi kuhusu matumizi na mgawanyo wa maliasili hizo. Udhibiti wa maliasili wenye haki na usawa unaweza kuchukua sura nyingi, lakini msingi wake ni watu walio na elimu inayostahili na waliojipanga vizuri kufanya kazi pamoja ili kuleta mabadiliko.

Afya ya mazingira daima ni suala la jamii. Watu lazima wafanye kazi pamoja, kama jamii, kulinda rasilimali wanazomiliki pamoja. Ili waweze kufanya kazi pamoja kwa muda mrefu, watu kawaida huunda umoja wao au asasi ya kijamii.

Siyo rahisi serikali kutoa mahitaji ya msingi kwa watu wote. Hali hii ni dhahiri zaidi katika nchi zinazoendelea na hasa zenye utawala usiowajibika. Watu hulazimika kuunda asasi zao za kijamii ili kujihakikishia maisha bora. Mara nyingi jamii inapojipanga vizuri, serikali pia huanza kuwajibika kutekeleza majukumu yake kwa watu.

Hata hivyo, mahitaji tofauti ya rasilimali kwa makundi, mfano, wanaume na wanawake, wafanyakazi, wakulima, wawekezaji katika misitu, wafugaji, viwanda na wengine yanaweza kuwa chanzo cha migogoro katika jamii na asasi za kijamii. Kawaida, kunakuwa na ugumu kukidhi mahitaji ya muda mfupi ya pato na yale ya muda mrefu ya kiafya kwa wakati mmoja. Ujenzi wa asasi imara za kijamii kawaida huchukua muda mwingi hasa kwa sababu ya tofauti hizi. Hivyo, kuwa na lengo la kiafya la muda mrefu, na kutafuta njia za kumshirikisha kila mtu, kunaweza kusaidia kupunguza migogoro na kujenga asasi imara za kijamii ambazo zitalinda maslahi ya wote.

a man speaks

Baada ya kila kijiji kuunda kamati ya afya, waliweza kuamua matatizo ya kiafya ambayo yalitakiwa kupewa kipaumbele zaidi.
Mfano:

Wakati kipindupindu kilipoingia na kusambaa katika nchi ya Ekueda, taasisi ya afya ya jamii iliandaa kamati za kuelimisha na kuhamasisha jamii katika kupambana vilivyo na kipindupindu. Kamati hizo za afya zilitoa elimu kwa jamii jinsi ya kutengeneza kinywaji chenye mchanganyiko wa chumvi na sukari kwa ajili ya kuwasaidia wagonjwa wanaoharisha. Pia ziliwafundisha jinsi ya kujenga na kutumia vyoo bora, na kuboresha miundombinu ya maji. Kamati zilisaidia pia katika kukarabati na kujenga vituo vya afya na kutoa elimu ya afya shuleni na nyumbani.

Watu wengine walihamasika na kuunda vikundi vya afya ya mazingira.

Shirika la Afya ya Jamii lilifanya kazi na mashirika kutoka nje ya jamii kwa kupatiwa fedha, utaalamu, madawa na mahitaji mengine muhimu. Walihakikisha kuwa rasilimali zinatumika vizuri na kusimamiwa na wanavijiji wenyewe. Jamii zilihusika pia katika kupanga na kufanya maamuzi jinsi ya kuendeleza programu hiyo.


Ukurasa huu ulihuishwa: 04 Juni 2022