Hesperian Health Guides
Kuirudishia uhai wake ardhi iliyoharibiwa
HealthWiki > Mwongozo wa jamii juu ya afya ya mazingira > Sehemu ya tano: Kuirudishia ardhi uhai wake na kupanda miti > Kuirudishia uhai wake ardhi iliyoharibiwa
Hakuna mtu anayeweza kulazimisha ardhi iweze kuzalisha. Hata mbolea za viwandani hufanya kazi kwa muda mfupi na hatimaye ardhi huishiwa uwezo wa kuzalisha. Lakini kama tutazingatia mzunguko wa asili, tunaweza kuchangia kutengeneza mazingira ambayo ardhi inahitaji kurejea hali yenye afya na rutuba.
Yaliyomo
Ardhi yenyewe kurejesha uhai wake kwa njia za asili
Wakati mwingine njia bora ya kuifanya ardhi yenyewe kurejesha uhai wake ni kuiacha ipumzike, au kutumia njia mbalimbali kuisaidia kurejea hali yake ya asili. Kwa mfano, kuizungushia uzio, kuweka matangazo yanayokataza shughuli za watu katika eneo hilo, au kupunguza idadi ya mifugo ni miongoni mwa mbinu zinazoweza kusaidia ardhi kurejea hali yake tena.
Ardhi inapolindwa na wakati huo huo hali ikawa inaruhusu, mimea inaweza kuanza kuota yenyewe. Ardhi yenyewe hurejesha uhai wake kwa njia za asili. Mchakato huu unaweza kuchukuwa miaka mingi au hata baada ya vizazi kadhaa kupita.
Ardhi yenyewe HAIWEZI kurejesha uhai wake iwapo:
- Hakuna vyanzo vya mbegu au mimea asilia karibu.
- Aina ya mimea inayoongezeka haraka imeshamiri na kufunika mimea inayohitajika.
- Ardhi imeharibiwa na kuchafuliwa kiasi kwamba hakuna chochote ambacho kinaweza kuota.
Mimea na miti ya asili na isiyo ya asili
Mimea ya asili (mimea ya eneo fulani) huota kwa urahisi katika mazingira yake ya asilia. Pia hutunza bioanuwai kwa kuvutia na kutoa makazi kwa wadudu, ndege na wanyama.
Wakati mwingine mimea au miti ambayo si ya asili kwa eneo husika hugeuka kuwa maarufu kwa sababu huota na kukuwa haraka, hutoa mbao nzuri au huchangia kuboresha udongo. Miti kama vile mikaratusi, misonobari, miarobaini, na lusina imeoteshwa sehemu nyingi duniani. Hata hivyo, kupanda miti na mimea ambayo siyo asilia katika eneo lako kunaweza kuleta matatizo kwa eneo husika:
- inaweza kufyonza maji mengi kutoka ardhini na kudhoofisha mimea na miti ya asili,
- inaweza kusambaa haraka hadi mahali ambapo haitakiwi,
- inaweza kusababisha wanyama na wadudu asilia katika eneo hilo kuhama na kutafuta makazi mengine.
Iwapo mimea ngeni itafunika eneo hilo, ni vigumu ardhi yenyewe kujirudishia uhai wake kwa njia za asili.
|
||||||||
3. Maji hutuama kwenye vidaka maji vilivyotengenezwa na mimea stahimilivu, yakileta mbegu na virutubisho. Lakini ndege huleta mbegu zaidi. | 4. Mimea mikubwa zaidi na miti midogo huota. Mizizi yao hutenganisha ardhi ngumu na kutengeneza udongo laini ambao unaweza kuhifadhi maji. | 5. Mimea mikubwa zaidi na vichaka huota na kukua na hatimaye ardhi inakuwa imejirejeshea uhai wake |
Jinsi ya kutengeneza mabonge ya mbegu
Njia rahisi ya kuotesha tena mimea katika eneo lililoathiriwa sana na mmomonyoko ni kutengeneza mabonge ya mbegu. Kila mwaka kusanya mbegu. Watoto hasa wana uwezo mkubwa wa kukusanya mbegu, na ni zoezi la kujifunza na burudani kwao. Kusanya mbegu nyingi kutoka miti asilia tofauti katika eneo lako, kadri iwezekanayo. Kwa kutumia mbegu hizi na udongo, tengeneza mabonge. Changanya: Mix:
Kipimo kimoja cha mbegu zilizochanganywa | Vipimo viwili vya mboji au udongo laini | Vipimo 3 vya udongo wa mfinyanzi uliochekechwa ili kuondoa mawe | Kiasi kidogo cha maji |
Changanya mbegu na mboji au udongo wa kupandia, kisha ongeza udongo wa mfinyanzi. Ongeza maji ambayo yanatosha tu kuulowesha. Ukiweka maji mengi mbegu zitajitokeza haraka. Viringa mabonge madogo kutokana na mchanganyiko huu na kuweka juani angalau kwa siku kadhaa.
Siku chache kabla ya msimu wa mvua au wakati wa msimu wa mvua, nenda mahali unapotaka miti iote na kurusha mabonge hayo. Ni muhimu kuweka vizuizi mapema kuhakikisha mbegu hizo zisisombwe na maji ya mvua yanayotirika juu ya ardhi.
Mvua ikinyesha mbegu zitachipua. Mboji husaidi kutoa virutubisho, na udongo wa mfinyanzi huzuia mbegu zisikauke, zisiliwe na panya au ndege na zisipeperushwe. Baada ya mwaka mmoja mimea hiyo itatengeneza mbegu zake, na mimea mingi zaidi itaota. Udongo utajikusanya kwenye mimea na kudhibiti mmomonyoko. Baada ya muda aina nyingi ya mimea itaanza kuonekana. Iwapo hali hii haitavurugwa, baada ya miaka mingi, eneo zima litarejea asilia yake.
Kusaidia miti kujiotea yenyewe
Katika nchi ya Somalia, kuna miti michache kutokana na hali ya ukame inayokaribia jangwa. Idadi hiyo ya miti huzidi kupungua siku hadi siku kwa kuwa hukatwa kwa ajili ya kutengeneza mkaa. Sehemu ya mkaa hutumiwa ndani ya nchi lakini kiasi kikubwa huuzwa nchi za nje. Mwanamke mmoja wa Kisomali Fatima Jibrell alipoliona tatizo hili, alianza kampeni kuhamasisha watu kuacha kuuza mkaa nchi za nje. Aliuliza, “Sisi wenyewe hatuna miti ya kutosha, tutawezaje kuruhusu kunyonywa rasilimali hiyo kidogo iliyopo.?”
Kampeni yake ilifanikiwa kiasi. Lakini kwa wakati huo, ni miti michache ilikuwa imebaki. Hivyo alianza kampeni ya kupanda miti nchini Somalia. Aliamini kwa njia bora ya kuwapunguzia umasikini watu wake ni kurejesha tena miti Somalia.
Ardhi ya Somalia ni kavu na yenye joto kali, ni vigumu kustawisha miti. Pia kwa kuwa watu wa Somalia huhama hama kutoka sehemu moja hadi nyingine kutegemea na hali ya hewa, ni vigumu kupanda miti na kuitunza. Hivyo, Fatima akaanza kuwafundisha watu kutengeneza vizuizi vya kuta fupi za mawe kadri walivyokuwa wakihama. Japokuwa ardhi ni tambarare, Fatima aliamini kuwa maji yangetafuta mahali pa kutuama, yakiambatana na viumbe hai vingine. Wakati wa msimu mfupi wa mvua, kuta hizi zilisaidia kuzuia virutubisho vya udongo, na mimea na miti kuanza kujiotea yenyewe. Hivyo, kutokana na kampeni hiyo, idadi ya miti nchini Somalia iliongezeka kuliko awali.