Hesperian Health Guides
Upandaji miti
HealthWiki > Mwongozo wa jamii juu ya afya ya mazingira > Sehemu ya tano: Kuirudishia ardhi uhai wake na kupanda miti > Upandaji miti
Zipo njia mbalimbali za kupanda miti:
- Panda mbegu au kipandikizi moja kwa moja kwenye udongo
- Kusanya na kupanda mbegu pori
- Panda miche vitaluni na kisha kuihamishia mahali palipoandaliwa
- Pandikiza kipandikizi cha mti unaoutaka kwenye kishina cha mti mwingine.
Njia utakayoichagua itategemea na aina ya miti unayotaka kupanda, na mbegu au vipandikizi vilivyopo.
Yaliyomo
- 1 Kuchagua mbegu au vipandikizi
- 2 Maandalizi ya mbegu kwa ajili ya kupanda
- 3 Kuandaa vipandikizi - miche
- 4 Kupandikiza miche-pori
- 5 Kuotesha miti kwenye vitalu-miti
- 6 Kutunza miti michanga
Kuchagua mbegu au vipandikizi
Watu wengi wanaamini msemo kuwa “Kama alivyo mzazi na mtoto wake ndivyo atakavyokuwa”. Hivyo, mtoto ambaye wazazi wake ni warefu, naye hutarajiwa kuwa mrefu. Hivi ndivyo ilivyo hata kwa mimea. Mbegu kutoka mti mrefu ulionyooka huenda ikazaa mti ambao unafaa kwa ajili ya mbao. Mbegu kutoka kwenye mti wenye sifa za dawa pia hutarajiwa kuzaa mti wenye sifa hizo hizo. Hivyo, ni bora kuchagua mbegu au vipandikizi kutoka mti-mama wenye afya na sifa unazotaka. Iwapo huwezi kupata mbegu bora katika eneo lako, unaweza kupata mbegu hizo kutoka kwa wakala wa ugani, au vitalumiche katika maeneo ya jirani.
Maandalizi ya mbegu kwa ajili ya kupanda
Baadhi ya mbegu, hususan zile zenye ganda laini, unga au majimaji ndani yake, lazima zipandwe mara baada ya kukusanywa. Mbegu nyingine huhitaji kuhifadhiwa kwa miezi mingi kabla ya kupandwa.
Mbegu nyingi zinahitaji maji ili ziweze kuota. Mbegu inapokuwa imefunikwa na ganda gumu inaweza pia kuhitaji kulainishwa au kukatwa kuruhusu ufyonzaji wa maji. Baadhi ya mbegu zinahitaji maandalizi zaidi kabla ya kupandwa.
- Kama ganda la mbegu siyo gumu sana (iwapo unaweza kuitoboa na kucha zako za vidole) na siyo nene sana, basi panda moja kwa moja kwenye udongo uliolowa.
- Kama ganda ni gumu lakini jembamba, funga mbegu ndani ya kitambaa. Ziloweshe kwa muda wa dakika 1 kwenye maji yasiyo ya moto sana, ambayo unaweza kugusa na vidole vyako (hayajafikia kuchemka). Zitoe haraka kwenye maji ya moto na kuziweka kwenye maji baridi na zibaki humo usiku mzima. Zipandwe siku inayofuata.
- Njia nyingine ya kushughulikia mbegu zenye ganda gumu lakini jembamba ni kuziloweka kwenye maji baridi kwa muda wa siku nzima. Baada ya hapo, zifunge kwenye tambaa au gunia ambalo limelowesha na maji kwa muda wa saa nyingine 24. Rudia utaratibu huu kwa muda wa siku 6. Siku ya saba zipande.
- Kama ganda ni gumu na nene, sugua mbegu kwa kutumia kipande cha karatasi - mchanga (sand paper) au chochote kinachofaa hadi sehemu laini za ndani ya mbegu zionekane. Chukua tahadhari usisugue sana sehemu za ndani na kuharibu mbegu.
- Baadhi ya mbegu zenye ganda gumu huandaliwa kwa kulowekwa kwenye maji usiku mzima zikiwa zimechanganywa na samadi, halafu huanikwa juani kwa siku moja. Rudia utaratibu huu kwa siku 3 - 4. Mbegu nzuri zitachipua tayari kwa ajili ya kupandwa. Mbegu ambazo hazitachipua zisitumike.
Baadhi ya mbegu huhitaji maandalizi ya kina zaidi, kama vile kupashwa katika moto mdogo, kuwekwa kwenye ubaridi mkali, au kwanza kuliwa na wanyama na kutolewa kama sehemu ya kinyesi. Fanya majaribio kujua njia ipi inafaa. Baada ya majaribio kadhaa, unaweza kuwa mtaalamu wa kuanzisha vitalu-miche.
Kuandaa vipandikizi - miche
Baadhi ya miti huota vizuri kwa kupanda vipandikizi - miche ardhini na kuvimwagilia maji hadi kuanza kutoa mizizi na majani. Miti inayoota kutokana na vipandikizi - miche, kwa kawaida hutoa matunda au mbegu mapema zaidi kuliko ile inayooteshwa kwa kutumia mbegu. Baadhi ya vipandikizi-miche vinaweza kupandwa moja kwa moja ardhini sehemu unapotaka mti uote. Vingine huoteshwa kwenye kitalu mpaka vitakapochipua na kutoa majani na mizizi mingi na hivyo kuweza kuendelea kukua vyenyewe.
Kata vipande vya mti kutoka katikati ya tawi ambalo haliwezi kupinda sana wala kushindwa kupinda kabisa. Chagua kipande chenye fundo 6-10 (uvimbe kwenye tawi la mti mahali majani huota). Taratibu ondoa majani kwa uangalifu ili usiharibu fundo hizo. Kata tawi kwa pembe ya kuchonga na siyo pembe ya nyuzi 90 ili kuwezesha mizizi kuota vizuri.
Vipandikizi-miche, viwe vimepandwa kwenye kitalu-miche au moja kwa moja ardhini, vinapaswa kumwagiliwa maji mengi na kulindwa dhidi ya wadudu wasumbufu hadi vitakapokuwa vimeota mizizi ya kutosha kuweza kujitafutia maji vyenyewe.
Kupandikiza miche-pori
Njia nyingine ya kuanzisha msitu ni kuchimbua miche ya miti ya porini na kuipandikiza pale unapotaka iote. Tafuta miti -mama iliyostawi vizuri na chagua miche mizuri inayoota karibu na miti hiyo.
Chimbua miche midogo kwa uangalifu ili usiharibu mzizi mkuu. Iwapo mzizi mkuu utaharibiwa, mti hautakua vizuri. Chimba kwa kufuata mduara kuzunguka mche na nenda chini mpaka utakapofikia ule mzizi mkubwa ulikoishia. Tumia mkono au kifaa kingine kung’oa mche na bila kuondoa udongo unaozunguka mizizi.
Acha udongo huo kwenye mizizi ya mche hadi utakapopandwa kwenye udongo. Endelea kumwagilia maji hadi mizizi itakapoweza kujitafutia maji yenyewe.
Kuotesha miti kwenye vitalu-miti
Vitalu-miti huwezesha miche kuanza kuota vizuri kabla ya kuhamishiwa kwenye maeneo mengine. Lakini kuanzisha na kutunza kitalu-miti siyo kazi rahisi. Inaleta maana kuanzisha kitalu - miti pale tu:
- Mbegu au miche ambavyo unataka kupanda ni adimu.
- Wadudu wasumbufu wanaweza kuharibu miche kama haikutunzwa vizuri.
- Watu wana muda wa kutosha kuhudumia kitalu-miti.
Kupanda miti moja kwa moja ni rahisi zaidi kuliko kuipanda kwenye kitalu-miti kwanza na kuihamisha baadae. Hata hivyo, miche zaidi hufa inapopandwa moja kwa moja kuliko inapooteshwa kwenye vitalu.
Lini uanze kupanda miti?
Kipindi gani cha mwaka ambapo miti inapaswa kupandwa hutegemea muda ambao miche inastahili kubaki kwenye kitalu-miche. Kama eneo lako lina msimu wa masika na kiangazi, panda miti yako pale tu masika yanapoanza ili kuepuka kazi ya kumwagilia. Miti mingi inahitaji miezi 3-4 kuwa kwenye kitalu kabla haijakuwa tayari kupandwa sehemu nyingine.
Mahali pa kuweka kitalu-miche
Kitalu -miche kinapaswa kufikika kwa urahisi, na ku wepo muda wote ambao miche inahitaji kukua kabla haijahamishwa na kupandwa sehemu nyingine. Pia kitalu-miche kiweze kufikiwa kwa urahisi na wote wanaokihudumia.
Kila kitalu-miche kinahitaji mambo yafuatayo:
Kuotesha miche ya miti kwenye vyombo
Kuotesha miche ya miti kwenye vyombo hurahisisha kuisafirisha na kupanda. Vyombo vinatakiwa kuwa vipana na vyenye kina cha kutosha kuwezesha miche kukua na kujega tuta la udongo kwenye mizizi, lisilo kubwa sana kiasi cha kuzidi uzito, au kufyonza maji zaidi kuliko mahitaji ya mche.
Urefu wa muda ambao mche unahitaji kubaki kwenye kitalu-miti, ndivyo ukubwa wa chombo kinachotakiwa. Ukubwa mzuri wa miti mingi kawaida ni angalau inchi 6 upana na inchi 9 kwenda chini. Vyombo vinapaswa kuwa imara kuweza kusimama wima vitakapojazwa udongo, na viwe na matundu kutoa nje maji pale yanapozidi.
Vyombo ambavyo vimetengenezwa kutokana na malighafi ambayo inaweza kuoza, mathalan magazeti, majani, karatasi ngumu, vinaweza kuchimbiwa moja kwa moja kwenye udongo pamoja na mche uliopo kwenye chombo. Vyombo ambavyo vimetengenezwa kwa plastiki, udongo wa mfinyanzi, mchanganyiko wa mchanga na saruji, bilauri au mbao vinapaswa kuondolewa kabla ya kupanda, lakini vinaweza kutumika tena mara kadhaa.Miche michanga inahitaji kulindwa dhidi ya jua kali. |
Chimba mashimo ya pembe nne yenye kina cha mara moja na nusu ya vyombo vya miche. Mashimo ya mduara huzuia utanuzi wa mizizi hadi kwenye udongo unaozunguka. | Jaza shimo na udongo ili shina la mche lilingane na usawa wa ardhi baada ya shimo kujazwa udongo. Unaweza kuongeza viganja viwili vya mboji au udongo mweusi wenye rutuba kusaidia mche kuanza kuota vizuri. Baada ya kupanda, lowesha udongo unaouzunguka mche na maji. |
Kuhamisha miche kitaluni kwa ajili ya kupanda katika maeneo magumu
Katika maeneo kame, tengeneza shimo dogo lenye mduara kwa ajili ya kudaka maji. |
Kutunza miti michanga
Tengeneza uzio kulinda miti michanga. |
Mti mchanga unahitaji kulindwa mwaka mzima wa maisha yake. Miradi mingi ya upandaji miti hushindwa kufanikiwa kwa sababu hakuna anayeisimamia miti michanga.
Iwapo hali ya hewa ni joto au ya ukame, miche inahitaji kumwagiliwa angalau mara moja kwa siku na baadaye kila baada ya siku 2 au 3. Baada ya wiki chache, mizizi ya miti huanza kutafuta maji yenyewe. Lakini kama hali ya joto inaendelea, mwagilia kadri miti inavyohitaji.
Dhibiti magugu mpaka mti utakapokuwa mrefu kuliko magugu hayo. Endapo wanyama au watoto wanaweza kuharibu miti hiyo michanga, jenga uzio kuzunguka mti.
Kama mti haukui vizuri, au majani yanaonekana kuwa ya njano au hayana afya, sambaza mbolea ya asili kuzunguka mti kadri ya matawi yake.