Hesperian Health Guides

Kuzuia mmomonyoko

Katika sura hii:

Upotevu wa udongo, au mmomonyoko, husababishwa na upepo au maji ambayo huondoa na kuhamisha tabaka la juu la udongo. Kuilinda ardhi dhidi ya mmomonyoko, hususan katika maeneo yenye miinuko mikali, huboresha uwezo wa ardhi hiyo kuotesha mimea, kulinda vyanzo vya maji vilivyopo chini yake, na kuzuia mporomoko wa ardhi. Wakulima wanaweza kuzingatia kanuni tatu zifuatazo kuzuia mmomonyoko wa ardhi na upotevu wa maji yanayotirika juu yake:

  1. Punguza kasi ya maji kwa kutengeneza vizuizi asilia kuanzia juu ya mwinuko hadi chini yake.
  2. Wezesha maji kusambaa kwa kutengeneza mifereji kadhaa kuyagawa na kuyaelekeza mahali yanapokwenda.
  3. Wezesha maji kuingia ardhini kwa kutibuatibua udongo ili uweze kunyonya maji kwa ufanisi.


Wakati mwingine ni vigumu kubainisha dalili za mmomonyoko. Hata hivyo, dalili hizo zinaweza kujumuisha mazao au mimea ambayo haistawi kama zamani, mito iliyojaa tope kuliko ilivyokuwa awali (hasa baada ya mvua kunyesha), na udongo unaoonekana mwepesi.

Illustration of the below:2 men stand beside 2 gullies through a field: 1 narrow, 1 wide.
Mtaro uliosababishwa na mmomonyoko unaanza kujitokeza... ...kabla ya muda mrefu mtaro huo utaonekana hivi.


Mahali ambapo mmomonyoko haujaanza, unaweza kuzuilika kwa kutunza mimea na miti mingi kadri inavyowezekana, na kwa kuelekeza maji yanayotiririka juu ya ardhi kwenye mitaro, mabwawa na mikondo ya asili ya maji. Mahali ambapo mmomonyoko tayari umekithiri, inawezekana pia kuuzuia na kurejesha udongo katika hali yake ya kawaida. Hata kupanga mawe kwenye mstari au kujenga ukuta mfupi wa mawe kwenye maeneo yenye miinuko kunaweza kuzuia udongo kusombwa na maji au upepo na kutupwa bondeni. Mbinu za kilimo endelevu au kilimo bora kama vile matumizi ya mboji, mbadilisho mazao, kutandazia, na kupanda miti pamoja na mazao ni njia za kulinda ardhi na vyanzo vya maji.…

Wafanyakazi wa shirika lisilo la kiserikali wajifunza kuhusu mmomonyoko wa udongo kutoka kwa wakulima

A woman talks with a farmer in a stony field.

Katika wilaya ya Gulbarga, Karnataka huko India, shirika moja lisilo la kiserikali lilifanya kazi pamoja na wakulima kuzuia mmomonyoko wa udongo katika mashamba yao. Wakulima hapo zamani walikuwa wakijenga vizuizi virefu vya mawe ambavyo vilikusanya karibu udongo wote uliokuwa umemomonyoka na kuruhusu maji kupita kwenye matundu, hata wakati wa mvua kubwa kila mwaka.


Wafanyakazi wa shirika hilo waligundua kuwa vizuizi hivyo vya mawe vilikuwa vinaruhusu kiasi fulani cha udongo kuchukuliwa na maji. Hata vizuizi virefu vilipojengwa katika maeneo ya chini ya mwinuko, baadhi ya mawe yalirushwa na kupita vizuizi hivyo na ilibidi kuokotwa na kurudishwa tena kwenye nafasi yake. Hivyo, walipendekeza ujenzi wa vizuizi vya mawe imara zaidi ambavyo vingezuia kabisa udongo kupotea na ambavyo havingehitaji ukarabati wa kila mara.


Wakulima walisema kuwa hawaoni tatizo kwa kufanya matengenezo madogo ya kila mara kwenye vizuizi hivyo. Wafanyakazi wa shirika hawakulielewa suala hili. Wakulima walitumia nguvu nyingi kutengeneza vizuizi hivyo. Lakini havikuweza kuzuia kabisa mmomonyoko. Hivyo wafanyakazi wa shirika walipendekeza kufanya jaribio. Katika baadhi ya mashamba wangejenga kuta za mawe fupi na imara. Katika mashamba mengine, wangejenga vizuizi vya asili.


Mwisho wa msimu, wakulima na wafanyakazi wa shirika walikutana na kulinganisha matokeo. Wakulima wenye mashamba yaliyo upande wa chini ya kuta imara za mawe hawakuwa na furaha kabisa. Ng’ombe walizunguka tu ndani ya kuta hizo na mashambani, na baada ya msimu wa mvua kubwa, wakulima hao hawakupokea udongo mpya mwingi wala maji ya kutosha kwa ajili ya mpunga, kama ilivyo kuwa kawaida.


Matatizo haya yalisababisha malumbano kati ya wenye mashamba upande wa chini ya kuta hizo na wale wenye mashamba juu yake. Jaribio hili lilionyesha kuwa vizuizi vya mmomonyoko vya asili vilifanya kazi vizuri kuliko kuta za mawe zilizopendekezwa na wafanyakazi wa shirika. Wakulima waliwaeleza wafanyakazi wa shirika hilo kuwa kuta za mawe zilisababisha matatizo mengi sana. Kutokana na uzoefu huu, wafanyakazi wa shirika lisilo la kiserikali walijifunza kuwa vizuizi vya asili siyo tu kwamba vilizuia mmomonyoko wa udongo, lakini vilizuia pia ng’ombe kurandaranda. Kuruhusu udongo kiasi na maji kupita na kwenda mashamba ya chini kulizuia mmomonyoko wa maelewano kati ya wakulima hao jirani, ambalo lilikuwa jambo muhimu kwa kwao kuliko kazi ya ziada ambayo walistahili kufanya kila mara kukarabati vizuizi hivyo.Ukurasa huu ulihuishwa: 04 Juni 2022