Hesperian Health Guides
Maji ya kutosha, maji salama vyote vina umuhimu unaolingana
HealthWiki > Mwongozo wa jamii juu ya afya ya mazingira > Sehemu ya tatu: Matatizo ya kiafya kutokana na maji yasiyo salama > Maji ya kutosha, maji salama vyote vina umuhimu unaolingana
Mzigo wa maji kwa wanawake
Kunapokuwa na uhaba wa maji, wachotaji na wabebaji wa maji - hasa wanawake na watoto - hulazimika kutembea umbali mrefu na kubeba mizigo mizito mno. Hali hii huwasababishia maumivu na hata majeraha shingoni, mgongoni na kwenye nyonga. Kazi ya kuchota maji mara nyingi huchukua muda na nguvu zao nyingi. Hata hivyo, wao na familia zao hutumia maji kidogo sana ikilinganishwa na mahitaji yao. Kazi ya utafutaji maji inaweza kuchukua muda mwingi sana kiasi kwamba shughuli nyingine ambazo akina mama hutarajiwa kufanya kwa ajili ya afya zao na familia zao, kama vile kuwahudumia watoto, kutafuta huduma za afya, au kutunza shamba hazifanyiki.
Maji huzuia na kutibu magonjwa mengi
Maji hutumika kupunguza homa na kusafisha vidonda na maambukizo kwenye ngozi. Kunywa maji mengi husaidia kuzuia na kutibu kuhara, maambukizi katika njia ya mkojo, kikohozi na kukosa choo. Kunawa mikono kwa maji na sabuni baada ya kutumia choo na kabla ya kula au kushika chakula pia husaidia kuzuia magonjwa mengi.
Kusafisha vidonda kwa maji husaidia kupunguza maambukizi. | Unaweza kutibu majeraha madogo ya moto kwa kuweka sehemu iliyojeruhiwa ndani ya maji ya baridi. | Unaweza kutumia maji ya moto na kitambaa kukanda uvimbe, majipu, vidonda, maumivu ya misuli na viungo. |